MABADILIKO KWENYE BODI YA FCS

0 Comments

MARGARETH CHACHA AJIUZULU BODI YA FOUNDATION

Napenda kuwataarifu wadau wote wa Foundation for Civil Society kuwa Bi Margareth Chacha amejiuzulu kama Mwenyekiti na mwanachama wa Bodi ya Foundation kuanzia tarehe 9 Februari, 2018.

Wanachama wa Foundation, ambacho ndio chombo cha juu kabisa cha maamuzi ya Foundation, ndio huteua Bodi ya FCS. Wanapoteua Bodi, huzingatia vigezo kadhaa muhimu vikiwemo weledi na uzoefu wa kusimamia tasisi mbalimbali. Bi Chacha aliteuliwa Mwanachama wa Bodi tarehe 15Octoba, 2015 kutokana na ujuzi na uzoefu wake katika kusimamia sekta binafsi na uwezeshaji wa wanawake. Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi tarehe 29 Septemba, 2017 akichukua nafasi iliyoachwa na Mwenyekiti aliyetangulia Prof Honest Ngowi.

Kufuatia kujiuzulu kwa Bi Chacha, Bw. Sosthenes Sambua ameteuliwa kukaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi mpaka Wanachama wa Foundation watakapokaa kwenye Mkutano Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 12 Julai, 2018. Bw. Sambua amekua akihudumu kwenye Bodi ya Foundation tangu tarehe 1 Octoba, 2016. Ana uzoefu na weledi mkubwa kwenye majukumu na kazi za Bodi katika kusimamia na kuongoza Foundation, hivyo ni imani yetu sote kuwa ataingoza vyema Bodi hii.

Pia, napenda kuwatoa wasiwasi wadau wetu wote kuwa mabadiliko haya katika Bodi ya Foundation hayataathri hata kidogo utendaji na kazi za Foundation kwa sekta ya asasi za kiraia nchini. Bodi hii itaendelea kuwa chombo chenye weledi na umakini mkubwa katika kusimamia utendaji wa Foundation for Civil Society.

 

Dk Stigmata Tenga

RAIS

Foundation for Civil Society