WITO WA MAOMBI YA KUTEKELEZA MIPANGO YA MIRADI YA UTAWALA BORA NCHINI TANZANIA, 2017

0 Comments

1.     Utangulizi

 

The Foundation for Civil Society (FCS kwa ufupi) ni shirika huru la kimaendeleo, la Kitanzania lisilolenga kupata faida, ambalo hutoa ruzuku na huduma za kuzijengea uwezo Asasi za Kiraia za Tanzania. Tangu kuanzishwa kwake FCS imechangia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha uwezo wa sekta ya kiraia nchini Tanzania, hivyo, kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja, imeziwezesha asasi za kiraia na wananchi kuwa nguvu muhimu inayoleta chachu ya ukubali wa utawala wa kidemokrasia nchini Tanzania na kuhakikisha uwepo wa utoaji wa huduma za hali ya juu, hasa katika ngazi za chini za jamii, hivyo kuchangia uwepo wa hali bora ya maisha kwa Watanzania.

 

Azma hii hufanikishwa kwa njia ya utoaji wa ruzuku, uwezeshaji wa mafungamano (linkages), sambamba na kuleta utamaduni wa mafunzo endelevu ndani ya asasi za kiraia na Tanzania kwa ujumla. Hivi sasa, FCS inatekeleza Mpango Mkakati mpya wa 2016-2020. Mkakati huo una maeneo muhimu manne (4) ya matokeo ambayo yanajumuisha Utawala Bora, Maendeleo ya Kimaisha/Kiuchumi, Kuimarisha Uwezo wa AZAKI na Uboreshaji wa Taasisi. Iwapo utapendelea kupata habari zaidi za FCS, waweza kuitembelea tovuti yetu: www.thefoundation.or.tz

 

2.     Kuhusu wito huu wa maombi

Wito huu wa maombi unazialika asasi za kiraia (za Tanzania Bara, Unguja na Pemba) kutuma maombi ya ruzuku inayohitajiwa ili kutekeleza miradi ya utawala bora kwenye maeneo mahalia.  Mradi wa Utawala Bora umebuniwa kwa kuzingatia ukweli kwamba upo mfungamano mkubwa wa dhana na wenye changamoto, baina ya umaskini, ukosefu wa usawa na utawala. Msingi wa dhana hii ni kwamba ufanisi wa utawala wa raia/ umma, kwa upande mmoja, unasaidia kuhamasisha mafanikio ya kiuchumi na utangamano wa kijamii, kupunguza umaskini na utunzaji wa mazingira. Kwa upande mwingine, dhana hii inaimarisha imani ya watu kwa serikali. Kwa hiyo, ni vyema kutambua kuwa bila uwepo wa utawala bora, maamuzi ya sera mbovu yatafanyika, wananchi watakosa sauti na madaraka, na bila shaka uchumi utatetereka. Vilevile, pale ambapo umaskini na ukosefu wa usawa unaposhamiri, unapunguza ushiriki wa wananchi, kutishia uwepo wa amani na mshikamano, kudhoofisha mikakati ya kisiasa na  kuimarisha utawala wenye mapungufu.

 

3.     Matokeo makuu

 

Matokeo I:              Viongozi wa serikali za mitaa wanatoa huduma bora zaidi.

Matokeo II:            Utoaji wa maamuzi na michakato ya kisiasa inaonyesha picha nzuri zaidi ya haki za wananchi, hasa ya makundi yaliyotelekezwa, watu wenye ulemavu, makabila madogo na wanawake.

4.     Maelezo kamili ya matokeo na maeneo yaliyolengwa

 

Matokeo I: Viongozi wa serikali za mitaa wanatoa huduma bora zaidi

 

Uwajibikaji na utoaji wa maamuzi unahitaji nguvu ya pamoja ya serikali na asasi zisizo za kiserikali ili kukuza/ kuongeza uwazi, uwajibikaji na matumizi ya utawala wa sheria kama vile maadili na uadilifu (kutokomeza rushwa) katika ngazi zote za serikali, sekta binafsi na vyama vya kiraia. Ushirikiano kati ya AZAKI na jamii utazihamasisha Serikali za Mitaa (LGAs) kuchapisha na kusambaza taarifa za fedha,  kulingana na miongozo ya uwazi na uwajibikaji, vilevile kuheshimu na  kuzingatia taratibu husika pamoja na utawala wa sheria.

 

Lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma litatimia pale tu  michakato ya maamuzi katika serikali za mitaa na matumizi ya rasilimali yatadhihirisha uwepo wa uwajibikaji na uwazi zaidi,.  Hivyo basi FCS inatarajia kwamba, asasi za kiraia zitakuwa na uwezo wa kubuni miradi kwa ufanisi, itakayohakikisha kwamba jamii imehamasishwa, imewezeshwa na kuelimishwa jinsi ya kudai haki zao kupitia njia sahihi. Vile vile, viongozi wa mitaa watakuwa wasikivu zaidi kuhusu madai, mahitaji na kero za wananchi, hivyo kuanza kutumia mbinu shirikishi katika mikutano yote itakayofanywa kwa mujibu wa sheria, yenye athari kwa maendeleo ya wananchi.

 

Maombi yatakayotumwa eneo hili la matokeo yatahusu miradi inayohusiana na Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma. Kwa hiyo, FCS inakaribisha maombi kutoka asasi za kiraia ambazo zitatekeleza miradi inayohusiana na:

 

a)     Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii auMatumizi ya Fedha za Umma kwenye sekta ya elimu katika mikoa ya  Lindi, Mtwara, Manyara, Tanga na Morogoro.

b)     Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii au Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma katika sekta ya maji kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Tanga.

c)      Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii au Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma kwenye sekta ya kilimo katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Songwe.

d)     Kusaidia ushiriki wa wananchi katika mipango na michakato ya bajeti,pamoja na upatikanaji wa taarifa muhimu za umma (kuhusu mgao wa rasilimali na usambazaji wake) pamoja na taarifa za matumizi ya rasilimali za umma / usimamizi katika ngazi ya mitaa na kitaifa. Mikoa lengwa ni Kigoma, Geita, Kagera, Mwanza and Singida.

 

Matokeo II: Michakato ya maamuzi na ya kidemokrasia inaonyesha uwepo wa haki za wananchi, hasa makundi ya pembezoni , Watu Wenye Ulemavu, makabila ya madogo( Ethnic Minorities) na wanawake.

 

Utawala Boraunahitaji ushiriki wa wananchi katika michakato muhimu ya utawala na demokrasia. Pia unahusu kuwawezesha wananchi kufahamu haki, wajibu wao na kutekeleza majukumu yao. Pale ambapo wananchi wanaelewa haki na wajibu wao ndipo watajua jinsi ya kujihusisha katika kupigania maslahi yao na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa viongozi wa umma wanawajibika. Utawala wa Sheria kwa mantiki hii, ni sehemu muhimu ya utawala bora na unatoa pamoja na mambo mengine nafasi kwa mtu ambaye amedhulumiwa haki zake kuweza kuzidai. Kadhalika, kutoa fursa kwa jamii kushiriki katika michakato ya utungaji na utekelezaji wa sera na sheria pamoja na kuondoa mifumo kandamizi inayowanyima fursa na haki za ushiriki makundi yaliyo pembezoni, kama vile watu maskini, vijana, wazee, watu wenye ulemavu, makabila ya wenye watu wachache na kadhalika.. Chini ya matokeo haya, FCS itatoa fedha kwa asasi za kiraia ambazo mapendekezo yao ya miradi, miongoni mwa masuala mengine yataonesha  kwamba hatimaye:

 

·       Makundi yaliyo pemebezoni yanawezeshwa, yanapata huduma za kijamii tena yanashiriki kwa kujiamini katika michakato ya maamuzi.

·       Wananchi wanadai haki zao tena wana ushawishi unaoleta mabadiliko.

·       Wanawake wanaamini kwamba unyanyasaji wa kijinsia haukubaliki, tena wanaulaani, mila mbaya zinakomeshwa, desturi zenye madhara zinasitishwa, sheria mbovu zinarekebishwa na wanawake wanaweza kupata, kumiliki na kufaidika na ardhi sambamba na mali nyingine.

·       Maofisa wa serikali za mitaa na vyombo vya dola wanaitikia kwa wakati kuhusiana na mahitaji ya wanawake na makundi ya pembezoni.. .

·       Ulemavu unatambuliwa, unazingatiwa na kujumuishwa kwenye ajenda na katika majukwaa muhimu.

·       Kupitishwa na kuingizwa kwa hatua maalum zinazohusu mahitaji ya Watu Wenye Ulemavu katika ngazi zote za serikali.

·       Watu Wenye Ulemavu, wanawake, vijana na makundi ya makabila madogomadogo daima wanalindwa, wanatetewa, tena wanafurahia haki zao.

 

Kwenye eneo hili, FCS inakaribisha maombi kutoka kweye Azaki za Kiraia ambazo zitatekeleza miradi kwenye maeneo yafuatayo:

 

a)     Kuanzisha majukwaa ya vijana katika ngazi ya wilaya ili kuongeza sauti za vijana na ushiriki wao katika utekelezaji na maendeleo ya sera za umma . Mikoa lengwa ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Zanzibar (Pemba na Unguja) Dodoma, Tanga na Mbeya.

b)     Utetezi dhidi ya mila potofu kama ukeketaji wa wanawake na udhalilishaji wa kijinsia. Mikoa lengwa ni  Arusha, Shinyanga, Simiyu, Mtwara Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida na Mara.

c)      Kufanya kampeni na utetezi dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.  mikoa lengwa ni Shinyanga, Mwanza, Geita, Katavi, Simiyu, Tabora na Rukwa.

d)     Utetezi wa Watu Wenye Ulemavu ili kuongeza ushiriki wao kwenye michakato ya uwajibikaji kwa umma na serikali za mitaa, ambayo ni mahsusi kwa Mashirika na Mitandao ya Watu Wenye Ulemavu kutoka mikoa yote ya Tanzania. 

e)     Kukuza upatikanaji wa ardhi na haki nyingine za kumiliki mali, hasa kwa wanawake. Mikoa lengwa ni Arusha (Arumeru) Manyara (Kiteto) Morogoro na Iringa.

 

5.     Fursa ya Ruzuku kwenye wito huu wa maombi

 

Wito huu wa maombi ni kwa waombao ruzuku za kati, ruzuku za ubunifu, na ruzuku za kimkakati. Maelezo ya kila fursa yanaainishwa hapo chini:

 

Fursa 1:  Ruzuku za Kati: Ruzuku zinazofikia 100 zitatolewa – Ukubwa wa ruzuku ni kati ya shilingi za Tanzania 50,000,000 hadi 120,000,000 kwa mwaka 1 hadi miaka 3,  kikomo kikiwa shilingi za Tanzania 360,000,000.

 

FCS itatoa ruzuku ya ukubwa wa kati kwa AZAKi ili kutekeleza miradi kwenye maeneo ya matokeo iliyoainishwa hapo juu. Kipindi cha utekelezaji wa mradi kitakuwa cha mwaka mmoja kwa kiasi kinachoanzia shilingi 50,000,000 hadi shilingi 120,000,000. Hata hivyo mwombaji anaweza kuomba hadi upeo wa shilingi 360,000,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.

 

Fursa 2: Ruzuku za ubunifu (Ruzuku zinazofikia 35 zitatolewa). Ukubwa wa ruzuku unaanzia shilingi za Tanzania 20,000,000 hadi shilingi za Tanzania 49,000,000 kwa mwaka mmoja tu.

 

Ruzuku za ubunifu zinalenga asasi ambazo zitatekeleza ubunifu wao wenyewe dhidi ya changamoto zinazoikabili jamii. Kipindi cha utekelezaji wa mradi kitakuwa mwaka mmoja. Asasi itaweza kuomba kati ya shilingi 20,000,000 hadi shilingi 49,000,000. Asasi zinazolengwa na dirisha hili ni kubwa na ndogo, lakini zile ambazo zitakuwa na ubunifu wa kipekee wa kuzisaidia jamii zao kwa kuzingatia maelezo ya matokeo kama ilivyoelezwa hapo juu. Dirisha hili pia linatoa mwanya kwa asasi ndogo, mpya na zenye mawazo chanya ya kutatua changamoto za kiutawala kwenye maeneo yao kupata ruzuku kutoka FCS. Hivyo, chini ya dirisha hili, FCS inakaribisha mapendekezo kutoka asasi za kiraia nchini kote ya kutekeleza miradi ya ubunifu / fikra, inayohusu utawala bora kama ilivyofafanuliwa na maeneo ya matokeo yaliyoainishwa hapo juu.

 

Fursa 3: Ruzuku Mkakati (Ruzuku zinazofikia 8 zitatolewa. Kiwango cha ruzuku itakayotolewa—Ukubwa wa ruzuku shilingi za Tanzania 250,000,000 kwa mwaka hadi miaka 3, kikomo shilingi za Tanzania 750,000,000)

 

Hii ni ruzuku kubwa kuliko zote ambazo FCS itakuwa ikitoa, inayolenga mitandao ya azaki, mashirika mwavuli, na asasi za kiraia zinazofanya kazi kwenye ngazi ya taifa, ambazo zina rekodi ya kuvutia na zenye ushahidi wa wazi wa utendaji wa kitaifa. Mashirika ya aina hii yatapewa ruzuku  kama “mashirika kiongozi” mathalani, azaki ambayo itapata ruzuku itakuwa kiongozi katika sekta iliyoombakwa mfano – asasi kiongozi katika Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii au Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma; asasi kiongozi katika utetezi dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na mila potofu n.k.. Azaki kama hizi shurti zibuni mipango yao ya namna ambayo zitashirikiana na AZAKi ndogo za mahalia, zinazofanya shughuli kama zao, hivyo kutumia mbinu watakazojifunza kwenye ngazi mahalia kuongeza ushawishi wao wa utetezi kwenye ngazi ya taifa; hapohapo kutumia ujuzi walionao ili kuongeza nguvu ya matokeo ya kazi kwenye eneo mahalia. Katika eneo hili, FCS inakaribisha maombi kutoka kwenye asasi za kiraia zenye ufanisi, ambazo zitatekeleza miradi huku zikizingatia mojawapo ya maeneo ya ufanisi, kama ilivyoainishwa kwenye Matokeo 1 na Matokeo 2. .

****************************************************************************

6.     JAMBO MUHIMU KWA WAOMBAJI WOTE

 

a)     Chini ya wito huu wa maombi, asasi itaweza kutuma maombi ya mapendekezo ya mradi kwenye aina moja tu ya dirisha. Kwa kufafanua zaidi, ni kwamba iwapo asasi hiyo itaomba kwenye dirisha la kwanza - la Ruzuku za Kati,   Asasi hiyohiyo haiwezi kutuma maombi kwa kupitia dirisha jingine la Ruzuku za Ubunifu au Ruzuku za Mikakati, au kinyume chake. Azaki  zinashauriwa kuchagua dirisha linalowafaa kabisa kulingana na maslahi na uwezo wao.

b)     Wito huu wa maombi ya mapendekezo ya mradi ni kwa asasi za kiraia zilizosajiliwa, ambazo zinaendesha shughuli zake ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mashirika ya kimataifa au maombi yoyote kutoka nje Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayatapokelewa.

c)      Kwa Azaki ambazo hivi sasa zina mikataba ya ruzuku na FCS, iwapo maombi yao ya ruzuku yalikuwa ni ya miaka mitatu (3), na shughuli zao zinaangukia kwenye maeneo ya wito wa sasa wa ufadhili, zinashauriwa kuboresha mapendekezo ya awali ili yaendane na wakati, zikizingatia mambo waliyojifunza wakati wa utekelezaji; na mabadiliko ya mazingira wakati wa kipindi cha utekelezaji, kisha kuwasilisha tena mapendekezo kamili yakiwa mwendelezo wa mipango ya mwaka 2017. Tafadhali onyesha wazi kwenye fomu ya maombi kwa kuangalia sanduku sahihi, mathalani, la wanaofadhiliwa hivi sasa. Zingatia kwamba waombaji wote wa ruzuku watapitia mchakato uleule kabla ya ruzuku kuidhinishwa.

d)     The Foundation for Civil Society, ni asasi ya kiraia inayojitegemea kimamlaka. Tunayo sera ya  kuendesha shughuli zetu zote kwa uaminifu na kimaadili. Katu hatuvumilii hongo na rushwa, kwani tumejitoa kuendesha mambo yetu kitaalamu, kwa haki, na uadilifu katika shughuli zetu na mahusiano yote. Kwa hiyo tunawasihi waombaji wote kufuata utaratibu uliowekwa wa kupata ruzuku kutoka FCS, kwa kutumia daima njia sahihi za mawasiliano. Ili kuwasiliana nasi, piga simu kupitia nambari+255 22 266 4890-2, simu ya mkononi  +255 754 005708 au barua pepe: Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona. . 

 

7.     KANUNI ZA JUMLA ZA UTEUZI WA MIRADI

 

Kanuni inayoongoza uteuzi wa mradi wowote unaopewa ruzuku ni kwamba hatua zinazotegemewa kuchukuliwa na mradi shurti zilete manufaa yanayoonekana kwa wananchi wa maeneo yaliyochaguliwa ya hapa nchini.

 

Kanuni nyingine mahsusi zaidi, ambazo zitaoongoza uteuzi wa mradi, ni pamoja na:

 

a)     Mashirika yenye mifumo thabiti ya utawala na utaratibu imara wa usimamizi wa fedha.

b)     Kiwango ambacho shughuli za mradi uliopendekezwa zinaendana na Mpango Mkakati wa FCS na vipaumbele vyake.

c)      Kiwango ambacho hatua za mradi zaweza kupimika na kuchangia kwenye ongezeko la uwazi, uwajibikaji, ufanisi na mwitikio wa serikali.

d)     Tashwira  ya kijamii, mathalani uwakilishi, kiwango cha kuhusika kwa jamii pamoja na kueleweka kwa mradi, maendeleo na utekelezaji wake.

(e) Kiwango ambacho mradi unalitatua tatizo kwenye mazingira mahalia kikiungwa mkono na ushahidi/   

tarakimu za uhakika.

(f)     Uzingatiaji wa kuambatanisha nyaraka zote zinazoendana na maombi kama ilivyoainishwa kwenye fomu ya maombi.

 

Angalia: Orodha ya viambatanisho imo kwenye Fomu ya Maombi ya Mwaka 2017.

 

8.     NANI ANAYETAKIWA KUTUMA MAOMBI

 

Taasisi zifuatazo zina sifa za kuomba ruzuku kutoka FCS:  

1.      Asasi za kiraia.

2       Mashirika yaliyojikita kwenye jamii (CBOs)

3       Mashirika ya Wataalamu

4       Vyama vya wafanyakazi

5       Vyombo vya Habari[1]

6       Taasisi za kidini[2]

7       Vyama vya ushirika[3]

 

1       YALE AMBAYO HATUTAYADHAMINI

 

FCS yaweza kutoa ruzuku kwa mashirika ya ndani, ambayo ni imara, tena hayakuanzishwa kwa madhumuni ya kupata faida binafsi. Hata kama shughuli ambayo umeiombea ruzuku ni ya kufanya hisani, haitakuwezesha kustahili kupata ruzuku, isipokuwa kama katiba ya taasisi yako inaelezea waziwazi aina ya hisani iliyosababisha kuanzishwa kwake. Iwapo unadhani kwamba asasi yako yaweza kuathirika na masharti haya, tafadhali tafuta ushauri kutoka FCS kabla ya kufanya maombi.

 

FCS haitatoa ruzuku kwa/kwa ajili ya:

 

·       Ufadhili & Udhamini.

·       Miradi au shughuli zilizopo nje ya Tanzania.

·       Miradi au shughuli ambazo zimeshakamilika 

·       Miradi inayotoa ruzuku kwa mashirika mengine

·       Malipo ya ziada kwa wafanyakazi wa shirika wanaolipwa mshahara

·       Ukuzaji wa kipato kwa asasi ndogondogo za kifedha

·       Maombi kutoka kwa wataalamu wa kuchangisha pesa au washauri wa kitaalamu wanaofanya kazi kwa niaba ya mashirika

·       Watu binafsi

·       Vyama vya siasa

·       Miradi inayopigia debe dini fulani, kabila au watu wa rangi fulani

·       Biashara za sekta binafsi (ilimradi ziwe zisizokusudia kutengeneza faida)

·       Mashirika ambayo yana madeni makubwa

·       Waendesha Semina, warsha, na mikutano  tu, isipokuwa kama ni sehemu ya shughuli zilizounganishwa na tokeo mahususi.

·       Semina, labda zile ambazo ni sehemu ya shughuli pana zaidi, ambazo zinaunganishwa na matokeo dhahiri

·       Gharama zisizotegemewa (dharura).

·       Utoaji wa huduma za jamii.

·       Maombi ya Ruzuku Mkakati ili kutekeleza miradi ya Ukimwi.

 

2       TAREHE YA MWISHO YA KUTUMA MAOMBI

 

Maombi yote yaliyofanyiwa tafakari ya kina na mapendekezo ya miradi yaliyoandikwa vema yanatakiwa yatumwe na kumfikia Mkurugenzi Mkuu kabla ya saa 10.00 jioni mnamo tarehe 7 Aprili 2017. Mapendekezo ya mradi yatakayotumwa baada ya tarehe ya mwisho ya kutuma maombi hayatafikiriwa kwa ajili ya kupewa ruzuku na FCS.

 

3       JINSI YA KUTUMA MAOMBI

 

Zipo njia mbili za kukamilisha maombi yako. Ya kwanza ni kujaza fomu ya maombi kwa njia ya mtandao kupitia hifadhidata yetu ya ruzuku http://www.smartgrants.co.tzna kutuma maombi yako kwa njia ya mtandao au kwa kupakua fomu na viambatanisho vyake kutoka kwenye tovuti ya FCS http://www.thefoundation.or.tz,  kuijaza fomu, kisha kuituma FCS kwa njia ya rejesta pamoja na viambatanisho vyake au kuituma kwa mkono. FCS haitapokea maombi yoyote yale yatakayotumwa kwa njia ya barua pepe. Kwa aina tatu tofauti za ruzuku, ona masharti ya kutuma maombi hapa chini.

 

S/N

Aina ya Ruzuku

Mfumo wa Maombi

1.      

Ruzuku za Ubunifu

Kwa njia ya mtandao au kwa kupeleka nakala halisi kama ilivyoelezwa hapo juu.

2.      

Ruzuku za Kati

Kwa njia ya mtandao au kwa kutuma nakala halisi kama ilivyoelezwa hapo juu.

3.      

Ruzuku Mkakati

Kwa njia ya mtandao tu.

 

 

Maombi Kamili ya Miradi yanayotumwa kama nakala halisi (hard copy) yapelekwe kwa:

 

Mkurugenzi Mtendaji

The Foundation for Civil Society

7 Madai Crescent, Ada Estate Plot No. 154

P. O. Box 7192

Dar es Salaam

Simu ya Mezani +255 22 266 4890-2

Simu ya Mkononi: +255 754 005708

Tovuti: www.thefoundation.or.tz

 

 [1] FCS inaweza kutoa ruzuku kwa vyombo vya Habari ili mradi ruzuku itakayotelewa haitachangia, gharama au kupunza madeni kwenye shughuli iliyolenga manufaa ya umma

[2]Makanisa na misikiti si sehemu ya Asasi za Kiraia. Hata hivyo, FCS yaweza kutoa ruzuku kwa Taasisi za Kidini ambazo shughuli zake hazielekezwi kwenye kutangaza imani/ uinjilishaji.

 

3 FCS yaweza kutoa ruzuku kwa vyama vya ushirika ilimradi ruzuku itakayotolewa haitachangia kwenye faida, gharama au kupunguza madeni bali kwenye shughuli iliyolenga manufaa ya umma.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.