WITO WA MAOMBI YA RUZUKU KWA ASASI ZA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA -MWISHO WA MAOMBI NI saa 10:00 Alasiri siku ya Jumatatu Tarehe 13 Februari 2017.

0 Comments
 1.  

  WITO WA MAOMBI YA RUZUKU KWA ASASI ZA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA 

  1. UTANGULIZI

  The Foundation for Civil Society (FCS) ni asasi huru iliyoanzishwa Tanzania mwaka 2002 na kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2003 kama Kampuni isiyogawana faida yenye dira ya kuchangia maendeleo endelevu kupitia kuimarisha uwezo wa asasi za kiraia Tanzania, ushawishi wa kisera na kuimarisha utamaduni wa kujifunza. FCS inafanya kazi nchi nzima (Tanzania Bara na Visiwani – Pemba na Unguja) katika kuhakikisha kwamba asasi za kiraia zinakuwa chachu kwenye michakato ya maendeleo yenye kulenga katika kuleta mabadiliko kwa wananchi. FCS imeandaa mpango mkakati mpya kwa mwaka 2016 hadi 2020 ambao unajumuisha Maeneo ya matokeo makuu manne (4) yanayohusisha Utawala bora, Kuboresha hali ya maisha ya jamii/ maendeleo ya kiuchumi, Kujenga uwezo na maendeleo ya kitaasisi kwa AZAKI. Taarifa Zaidi kuhusu dira, lengo mahsusi na kazi tunazofanya tembelea: http://www.thefoundation.or.tz.

  1. MALENGO MASHIES YA RUZUKU KWA ASASI ZA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA

  Ushiriki wa watu wenye ulemavu katika michakato mbalimbali ya maendeleo umekuwa ukikumbwa na vikwazo mbalimbali. Moja ya changamoto kubwa imekuwa ni ushirikishwaji duni katika kupanga matumizi ya rasilimali (Mgawanyo na usambazaji wa rasilimali za umma) pamoja na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali hizo hasa katika sekta za afya na elimu. Miongoni mwa sababu zinazopelekea ushiriki na ushirikishwaji duni ni pamoja na upatikanaji hafifu / mdogo wa taarifa za msingi kwa watu wenye ulemavu kuhusu mapato na matumizi ya rasilimali katika Afya na Elimu, miundo mbinu duni na isiyo rafiki katika vituo vya afya na shule, gharama kubwa za kupata huduma za afya na elimu kwa ujumla, mitazamo hasi kutoka kwa jamii kuhusu ulemavu na watu wenye ulemavu , kutokuwepo wakalimani wa lugha ya alama wakati wa mikutano ya ngazi mbalimbali za serikali.

  Kwa kutambua changamoto hizo, FCS imekuwa ikifanya kazi na asasi za watu wenye ulemavu ili kuchangia katika utatuzi wake. Ili kukuza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika usimamizi wa rasilimali za umma, FCS inakaribisha maombi ya ruzuku kutoka katika asasi za kiraia za watu wenye ulemavu zilizosajiliwa, ambazo hazifungamani na vyama vya siasa, na hazitengenezi faida kutoka mikoa yote Tanzania kushiriki katika utekelezaji wa shughuli zinazolenga kuimarisha sauti na ushiriki mkubwa wa watu wenye ulemavu katika usimamizi wa rasilimali za umma.

  2.1 Lengo kuu la kutekeleza programu hii ni: 

  • Kukuza/ kuongeza sauti na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwa watu wenye ulemavu. 

  2.2 Matokeo yanayotarajiwa

  • Kuongezeka kwa kiwango cha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma kwa watoa huduma na maamuzi kwenye shughuli zinazowalenga watu wenye ulemavu. 

  2.3 Shughuli zitakazofadhiliwa 

  • Kufanya ufuatiliaji wa mapato na matumizi ya rasilimali za umma katika sekta za Afya na Elimu zenye mlengo wa kunufaisha watu wenye ulemavu. 

  1. Kiwango cha ruzuku na Muda wa utekelezaji 

  FCS itatoa kiwango kisichozidi shillingi milioni ishirini (20,000,000) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa miezi nane (8). 

  1. Vigezo vitakavyo zingatiwa katika kuidhinisha miradi

  Kigezo kikuu kitakachozingatiwa katika kuidhinisha na kuthibitisha mradi wowote ili kupewa ruzuku kutoka FCS ni ubunifu wa mradi wenye tija na unaopimika pasipo shaka kuwa utawanufaisha (moja kwa moja au kwa njia nyingine) watu wenye ulemavu katika eneo la mradi na sio vinginevyo.

  Vigezo vingine mahsusi ambavyo vitazingatiwa katika uidhinishaji wa mradi ni pamoja na;

  1. Ni kwa jinsi gani shughuli zilizopangwa katika andiko la mradi zinaendana na vipaumbele pamoja na Mpango mkakati wa FCS kama ilivyoelezwa kwenye tangazo.

  2. Uchambuzi mzuri wa tatizo na mikakati ya kulitatua wenye mankiti

  3. Ni kwa jinsi gani utekelezaji wa andiko mradi unaweza kupimika na kuchangia katika kupelekea ufanisi, uwazi, uwajibikaji, urahisishaji wa upatikanaji wa huduma na utendaji wa Serikali.

  4. Uwezo na ubunifu wa miradi yenye kuleta tija kwa gharama nafuu.

  5. Nafasi ya jamii, kama vile, uwakilishwaji na ushirikishwaji, kiwango cha uhusishwaji wa jamii ya wanufaikaji katika kuandaa, kuitambua na kutekeleza miradi inayowahusu.

  6. Kwa jinsi gani mradi utaweza kuinufaisha jamii hadi katika ngazi ya chini kabisa kwa uthibitisho wa takwimu na ushahidi.

  7. Uwepo wa nyaraka zote za muhimu zinazohitajika katika fomu ya maombi, zikiwemo fomu ya bao mantiki, mpango kazi, na bajeti, zinazopatikana kwenye tovuti ya Foundation.

  Kumbuka:Orodha ya viambatanishi vyote muhimu imeambatanishwa katika fomu mpya ya maombi.

  1. Taasisi zinazoalikwa kuleta maombi 

  Taasisi na Asasi za watu wenye ulemavu tu zenye vigezo vinavyohitajika, zinaweza kushiriki katika utekelezaji wa programu hii. Kila mwombaji atatakiwa kuomba utekelezaji mradi katika sekta moja tu yaani ama sekta ya elimu au sekta ya afya. 

  1. Taasisi ZISIZOLENGWA kupata ruzuku. 

  Ruzuku hii inalenga taasisi za watu wenye ulemavu tu. Hata hivyo, FCS itatoa ruzuku kwa Taasisi za watu wenye ulemavu ambazo zimesajiliwa kufanya shughuli ambazo hazizalishi faida. Hivyo, hata kama mwombaji anaweza kuwa ameomba kuendesha shughuli isiyo ya kujipatia faida lakini hatoweza kufuzu kupata ruzuku mpaka athibitishe kupitia katiba yake kuwa Taasisi yake si ya kuzalisha faida. Kama maelezo na ufafanuzi zaidi vitahitajika juu ya kigezo hiki, basi wasiliana na FCS kabla haujafanya maombi yako ya ruzuku.

  FCS haitatoa ruzuku kwa:

  • Udhamini na ufadhili

  • Miradi au shughuli zitakazo fanyika nje ya Tanzania

  • Miradi au shughuli ambazo zimeshawahi kufanyika na kukamilika.

  • Miradi ambayo imekwisha wezeshwa ruzuku na mashirika mengine.

  • Kutumika kama Malipo ya ziada kwa wafanyakazi wanaolipwa na taasisi husika

  • Kipato cha mtaji kwa taasisi ndogondogo za fedha

  • Maombi toka kwa wataalamu wa ushauri au watunisha mifuko kwa niaba ya taasisi.

  • Watu binafsi

  • Vyama vya siasa

  • Miradi ambayo inalenga kuinufaisha dini/dhehebu Fulani, kabila Fulani au kikundi Fulani chenye mlengo wa kikabila.

  • Sekta binafsi (isipokuwa kama haipo kwa ajili ya manufaa ya kuzalisha faida)

  • Taasisi zenye madeni

  • Waendesha Semina, warsha, na mikutano tu, isipokuwa kama ni sehemu ya shughuli zilizounganishwa na tokeo mahususi.

  • Gharama kubwa zisizo tarajiwa (dharura)

  • Utoaji wa huduma za jamii

  • Maombi ya mkakati wa ruzuku katika utekelezaji wa miradi ya UKIMWI

  1. Tarehe ya mwisho wa kupokea maombi

   Maombi yote yaliyokamilika yanatakiwa kuwasilishwa na kumfikia Mkurugenzi Mtendaji kabla ya saa 10:00 Alasiri siku ya Ijumaa Tarehe 13 Februari 2017. Andiko la mradi litakalowasilishwa baada ya muda na tarehe husika kupita halitapokelewa wala kufanyiwa kazi na FCS.

  1. Fomu ya maombi ya ruzuku

  Kila Mwombaji atatakiwa kujaza fomu mpya ya maombi ya ruzuku ambayo inapatikana katika tovuti ya FCS ambayo ni; http://www.thefoundation.or.tz/index.php/en/notice-board .Waombaji wanashauriwa kujaza fomu hiyo moja kwa moja kwa njia ya kielektoniki. 

  Waombaji wanaruhusiwa kuwasilisha maombi yao kwa Kiingereza au Kiswahili. 

  1. Jinsi ya kuwasilisha maombi ya ruzuku

  Andiko la mradi lililokamilika linatakiwa kuwasilishwa kwa nakala halisi (Hard Copy na siyo kwa njia ya kielektroniki au kwa barua pepe). Kwa mantiki hiyo fomu zote zilizojazwa vizuri zinatakiwa kuletwa moja kwa moja Ofisini au kutumwa kupitia sanduku la barua/posta kwa anuani ifuatayo;

  Kwa Mkurugenzi Mtendaji

  The Foundation for Civil Society

  7 Madai Crescent, Ada Estate Plot Na. 154

  S.L.B 7192

  Dar es Salaam 

  Simu ya mezani +255 22 266 4890-2

  Simu ya mkononi +255 754 005708

  Tovuti: www.thefoundation.or.tz 

  1. Angalizo muhimu kwa waombaji wote wa asasi za watu wenye ulemavu.

  The Foundation for Civil Society (FCS) ni asasi huru inayoendeshwa kwa misingi ya uwazi na uwajibikaji na isiyovumilia vitendo vya rushwa. Tunawaasa waombaji wote wa ruzuku na asasi za kiraia kwa jumla kufuata utaratibu ulioelezwa na wakati wote kufuata njia sahihi za mawasiliano. Tafadhali tumia mawasiliano yetu: Simu ya mezani +255 22 266 4890-2, Simu ya mkononi +255 754 005708 au barua pepe:  Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.  kuwasiliana nasi. 

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

 • Namba ya simu: +255 22 - 2138530

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.