Vijiji kumburuza kortini Kamishna wa Ardhi

MGOGORO wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji unaoitesa Wilaya ya Kilosa kwa muda mrefu unaingia katika hatua nyingine baada ya Kijiji cha Mfulu, Mambegwa na Mbigili kumburuza mahakamani Kamishna wa Ardhi nchini kwa kukaidi amri ya Mahakama ya Rufaa.

Uamuzi wa vijiji hivyo kumburuza mahakamani Kamishna huyo Januari 15 ulitolewa wilayani humo  katika mafunzo ya sera na sheria za ardhi yaliyotolewa na asasi ya Greenbelt Schools Trust Fund-GSTF kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mambegwa, Said Naga, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi katika kesi ya madai namba 23/2006 ilibatilisha hati na usajili wa Kijiji cha Mabwegere cha wafugaji kwa kukiuka njia za upatikanaji wa kijiji, ambapo wafugaji walikata rufaa Mahakama ya Rufani kwa kesi ya madai namba 53/2010 na kushinda.

“Sasa baada ya kukaa vijiji hivi tumeamua Januari 15 kumburuza mahakamani Kamishna wa Ardhi nchini kutokana na kutunyang’anya ardhi bila  kutushirikisha. Alitoa hati juu ya hati na kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi, kapuuza agizo la mahakama la kuchunguza mipaka na kutoa taarifa ndani ya siku 90,” alisema Naga.

Kwa mujibu wa baadhi ya tarifa ambazo gazeti hili limezipitia ikiwemo barua ya Januari 26 kumb. namba KDC/cl.2/4/Vol.1/5 ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwenda kwa mkuu wa wilaya hiyo, kuna mchanganyiko wa taarifa za uhalali wa kijiji hicho kinachokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 10,234 wakati kijiji mama cha Mfulu ni kidogo mara mbili.

Aidha, mgongano mwingine ni kijiji kupewa hatimiliki mwaka 1990 wakati kiliandikishwa mwaka 1999, mkuu wa wilaya kipindi hicho, Sosthenes Kasapila, aliagiza kung’olewa vigingi vya mipaka ya kijiji  bila kuwashirikisha wananchi, nayo Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutoa hukumu kwa ramani ya kijiji iliyofutwa kisheria.

 

Mwanaruzuku wetu asifiwa kwa kuhamasisha jamii kutumia rasimali zao kwa maendeleo

Asasi ya Integrated Rural Development Organisation (IRDO) iliyoko wilayani Ileje, mkoani Mbeya imesifiwa kwa mchango wake wa kuhamasisha jamii kutumia razilimali zao kuibua miradi ya kimaendeleo badala ya kukaa na kusubiria Serikali ama vyavyo vingine.

 IRDO ilipata kupongezi hizo wakati wa ziara ya pamoja ya Foundation for Civil Society (FCS) ya kutathmini utekelezajiwa miradi yake pamoja na Wadau wake wa Maendeleo iliyofanyika mkoani Mbeya mwanzoni mwa mwezi Disemba.

 “Nimefurahishwa na mfumo wenu mnaoutumia wa kuzijengea uwezo jamii zinazowazunguka ili kutumia rasilimali zao binafsi na hivyo kuyaboresha maisha yao. Nafikiri hata Foundation watakubaliana nami kwa hili na kupanua wigo wa mfano mzuri kama huu wa IRDO,” alisema mwakilishi kutoka Shirika la Misaada la Uingereza (DFID) Zabdiel Kimambo, ambaye pia alishiriki katika ziara hiyo ya pamoja ya kutathmini miradi inayofadhiliwa na Foundation.

 Safari hii washiriki katika ziara ya pamoja ya kutathmini miradi inayofadhiliwa na Foundation walikuwa ni baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Foundation, wakuu wa idara mbalimbali za Foundation na wawakilishi kutoka nchi na mashirika ya Wadau wa Maendeleo wa Foundation. Wadau wa Maendeleo waliowakilishwa katika ziara hii ni pamoja na DFID, Ubalozi wa Norway and Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).

 Akifafanua juu ya matokeo yaliyotokana na mradi wao unaofadhiliwa na Foundation wa kuzijengea uwezo Asasi na vikundi vya kijamii wilayani Ileje mratibu wa IRDO, Patrick Mwalukisa, alisema asasi yake imekwisha kuvipatia mafunzo jumla ya vikundi vya kijamii (CBOs) 42 juu ya usimamizi wa mapato na vile vile juu ya kuratibu miradi ya kimaendeleo.

 Alisema kupitia mafunzo hayo moja ya CBOs lengwa iitwayo, Mkombozi, ilipata hamasa na kuanza kuhamasisha jamii ya kijiji cha Mswima wilayani humo kwa kutumia njia ya tumbuizo la ngoma asilia na kuibika na mradi wa kukarabati barabara ndogondogo pamoja na madaraja ya kiasili kwa kutumia rasilimali zao wenyewe.

Mwalukisa alisema kutokana na ujuhudi hizo, wanakijiji cha Mswima wameweza kujinasuru na changamoto za kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda masokoni na pia kuweza kuwasaidia wanakijiji wenzao wanaougua (hasa wajawazito) kusafiri kiurahisi kwenda katika zahanati ya jirani – takribani kilometa 10 au hata kuvuka na kwenda kijiji cha jirani cha Isoko.

 “Kupitia hizi CBOs, mbali na mambo mwngine, tumeweza kuhamasisha jamii kutambua thamani ya rasilimali zao na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo yao na ya wale wote wanaowazunguka,” alisema Simon Mwang’onda, Mkurugenzi Mtendaji wa IRDO.

Foundation yahitimisha ziara ya pamoja ya utathimini miradi mkoani Mbeya kwa wito

Ziara ya pamoja ya utathimini miradi kati ya Foundation na Wadau wake wa Maendeleo ilikamilika mapema mwezi huu mkoani Mbeya huku Asasi ya Kuratibu Ushiriki wa Wakulima katika Ufuatiliani wa Matumizi katika Sekta ya Kilimo (MIICO) ikipewa changamoto.

MIICO imetakiwa kuvijengea uwezo vikundi vyake vya mabaraza ya wakulima, ili hapo baadaye viweze kuwa asasi kamili zitakazoweza kujiendesha zenyewe na kuweza hata kuomba ufadhili kutoka Foundation ili kutekeleza miradi.

Wito huu ulitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation, Bw. John Ulanga, wakati akitoa hotuba yake fupi kabla ya kuagana na watendaji wa MIICO mkoani Mbeya. MIICO ilikuwa ni Asasi ya kumi na ya mwisho kutembelewa kwa ajili ya utathinimi wa pamoja na Wadau wa Maendeleo mkoani Mbeya.

“Ningewashauri kujizatiti pia katika kuyajengea uwezo mabaraza yenu ya wakulima ili ifikapo mwisho wa mradi wenu (baada ya miaka mitatu) mabaraza haya yakuwe kama Asasi kamili za Kiraia yatakayoweza kutekeleza miradi na hata kuomba ufadhili kutoka Foundation na nyie mkiwa pembeni kuwapa ushauri wa kuitendaji.

“Haya yatakuwa mafanikio yenu makubwa mengine, endapo mtawajengea uwezo wengine watekeleze mradi wa Kufuatilia Matumizi katika sekta ya kilimo, na endapo nyie kama MIICO mtakuwa mmeamua kufanya kitu kingine hapo baadaye,” alisema Bw. Ulanga.

Tayari MIICO imeweza kuwafikia wanufaika 12, 198 kupitia mtandao wa mabaraza yake ya wakulima katika mikoa ya Mbeya na Njombe katika mradi wa Kufuatilia Matumizi katika sekta ya kilimo ili kuboresha utoaji huduma katika kilimo.

Safari hii washiriki katika ziara hii ya ya pamoja ya utathimini miradi kati ya Foundation na Wadau wake wa Maendeleo walikuwa: baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Foundation, watendaji wa kuu wa idara mbalimbali za Foundation na wawakilishi wa mataifa mbalimbali ambao ni Wadau wa Maendeleo wa Foundation. Wawakilishi wa Wadau wa Maendeleo walitoka katika Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID), Ubalozi wa Norway na Shirika la Misaada la Uswisi (SDC).

Ziara ya pamoja ya utathimini miradi kati ya Foundation na Wadau wake wa Maendeleo huandaliwa ili kuwapa Wadau wa Maendeleo fursa ya kujionea jinsi miradi mbali mbali inayofadhiliwa na Foundation kupitia misaada yao inavyotekelezwa.

AZAKI zatakiwa kuwa vinara kufanikisha utangamano imara Afrika ya Mashariki

Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetakiwa kuwa vinara na mstari wa mbele ili kufanikisha uwepo wa utangamano imara wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Wito huo umetolewa jijini Arusha Novemba 27 na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Bw. John Ulanga, alipokuwa akifunga kongamano la siku mbili la Asasi za Kiraia juu wa wajibu na mchango wa AZAKI katika kuimarisha utangamano wa Afrika ya Mashariki.

“Sisi kama Asasi za Kiraia, wajibu wetu mkuu ni kuwa vinara wa hufanikisha mijadala na utoaji wa elimu katika jamii zetu ili kuwa na utangamano imara, unaotokana na kuongozwa na wananchi wenyewe,” alisema Bw. Ulanga katika hotoba yake fupi ya kufunga kongamano.

Awali, mwendeshaji mada katikakongamano hili, Mwl. Basiru Ally, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema endapo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) inataka kuwa na utangamano imara ni lazima kuwepo na mabadiliko ya kimtazano na kuachana na dhana ya viongozi wakuu wa nchi kuwa vinara wa utangamano na badala yake uwe ni utangamano unaowashirikisha wananchi kuanzia ngazi za chini katika jamii zetu.

Aidha, katika maazimio yao washiriki wa kongamano la AZAKI juu ya utangamano wa Afrika ya Mashariki walikubaliana kwa sauti moja kuzitaka mamlaka husika kuhakikisha uundwaji wa utangamano ulio imara, wenye kutokana na kuendeshwa na wananchi wenyewe.

WanaAZAKI washiriki katika kongamano pia wameitaka Tanzania kuirudia nafasi yake tena na kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha utangamano wa Afrika ya Mashariki imara zaidi.

Kongamano la AZAKI lataka Utangamano wa Afrika Mashariki ulio imara, unaotokana na wananchi

Kongamano la Asasi za Kiraia Tanzania juu ya Utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofanyika jijini Arusha hivi karibuni limeafiki wito wa kuwa na utangamano wa Afrika Mashariki imara na sio legelege, unaotokana na unaoongozwa na wananchi wenyewe.

Ikiwa ni sehemu ya hitimisho la kongamano la siku mbili la wana AZAKI liliandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS) na kumalizika Novemba 27 mwaka huu, washiriki walikubaliana kwa ujumla wao na kuzitaka nchi wanachama kuhakikisha Jumuiya inakuwa na utangamano imara ambao utatokana na kuongozwa na wananchi ili kuleta maendeleo endelevu.

Kongamano hilo la AZAKI pia lilifikia maazimio yake juu ya nafasi ya Tanzania katika kufanikisha utangamano wa Afrika ya Mashariki ambao wanautaka. Kwa makubaliano ya pamoja pia, washiriki kutoka Asasi za Kiraia wameitaka nchi ya Tanzania kuwa kinara na mstari wa mbele katika kuhakikisha utangamano imara wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, unaotokana na kuongozwa na wananchi wenyewe unafanikiwa.

“Hata kama tukirudi nyuma na kuangalia historia, Tanzania ndio ilikuwa kinara katika ukanda huu iliyochukua uongozi madhubuti wa kufanikisha uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo kwa bahati mbaya ilivunjika mwaka 1977. Kwa hiyo hakuna haja ya Tanzania kusita kuichukua nafasi yake tena kama kinara wa kuhakikisha utangamano imara wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki unapatikana,” alisema mmoja ya watoa mada katika kongamano hilo, Dk. Kitila Mkumbo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Pia mhadhiri mwingine, Dk Azaveli Lwaitama, ambaye pia alitoa mada katika kongamano hilo alisema: “Endapo tunahitaji kuwa na utangamano imara, tunahitaji kufikiwa mapema kwa hatua ya Ushirikiano wa Kisiasa ili uweze kuwa chachu ya kudhibiti hatua nyingine zote muhimu za utangamano imara, kama vile Umoja wa Ushuru, Soko la Pamoja na uwepo wa Sarafu Moja.”

“Sisi kama Asasi za Kiraia, wajibu wetu mkuu ni kuwa vinara wa hufanikisha mijadala na utoaji wa elimu katika jamii zetu ili kuwa na utangamano imara, unaotokana na kuongozwa na wananchi wenyewe,” alisema Bw. John Ulanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society.

 Kongamano hilo la AZAKI ilikutanisha washiriki takribani 130 (30 kutoka nchi nyingine wananchama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki) huku mada kuu ikiwa ni: “Wajibu wa Asasi za Kiraia katika kuimarisha utangamano wa Afrika ya Mashariki.”

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari