CHAVITA yahimiza matumizi ya lugha ya alama

Serikali mkoani Mtwara imeshauriwa kuanza mchakato wa kuhamasisha jamii kujifunza matumizi ya lugha ya alama ili kuondoa vikwazo vya mawasiliano baina ya viziwi na watu wasio na ulemavu huo hatimaye kundi hilo liweze kutumia vyema fursa za kimaendeleo zinazowazunguka.


Ushauri huo ulitolewa juzi na mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) tawi la Mkoa wa Mtwara, Kasim Mchindula alipokuwa akizungumza na wanachama 30 wa chama hicho kwenye mafunzo  ya siku kumi ya  lugha ya alama, mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kanisa la Lutherani mkoani humo.


Alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano baina ya viziwi na jamii inayowazunguka katika kufanikisha shughuli mbali mbali za maendeleo na kwamba hali hiyo inatokana na jamii na baadhi ya viziwi kutofahamu matumizi ya  lugha ya alama hivyo kufanya kuwepo kwa ugumu wa mawasiliano.


Mchindula alisema CHAVITA mkoani Mtwara imeamua kutoa mafunzo hayo ya siku kumi kwa wanachama wake  kupitia mradi wake wa miaka mitatu unaofadhiliwa na Foundation for Civil SOCIETY ambao unalenga kuwajengea uelewa wa namna ya matumizi ya lugha ya alama ambapo itawasaidia kuondokana na vikwazo vya mawasiliano.


Alisema kutofahamika kwa lugha ya alama kunachangia kurudisha nyuma jitihada za maendeleo kwa viziwi hivyo kupitia mafunzo hayo wanachama hao 30 watakuwa na uelewa wa matumizi ya lugha hiyo ya alama na kuwaondolea adha ya mawasiliano na viziwi wengine.


“Hata kwa upande wa elimu viziwi wengi wamekuwa hawafanyi vizuri katika masomo yao kutokana na kutokuwa na ufahamu wa lugha ya alama.” Tunaomba serikali nayo iwe na utaratibu wa kutoa mafunzo ya lugha ya alama kwa jamii ili kuondoa vikwazo vya mawasiliano baina ya viziwi na wasio viziwi”, alisema Mchindula.


Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Ofisa Elimu mkoa, Mshauri wa utamaduni ofisi ya mkuu wa mkoa, Fatma Mtanda alisema lugha ya alama kwa viziwi ni msingi wa upatikanaji wa haki za msingi katika kuboresha mahitaji ya msingi ndani ya maisha yao ya kila siku.


Alisema matumizi ya lugha ya alama kwa viziwi pia kutawasaidia kuweza kuibua vipaji vyao ambapo kwa sasa havitambuliki katika jamii kutokana na jamii kushindwa kuwasiliana na viziwi kwa kutumia lugha hiyo.
“Serikali mkoani hapa tutahakikisha lugha hii inatambulika kwa jamii nzima ili kuwe na usawa wa mawasiliano rahisi kati ya viziwi na watu wasio viziwi hatua ambayo itasaidia kuleta mabadiliko ya maendeleo kwa kundi la viziwi”, alisema Fatuma.

Jamii ya watu wenye ulemavu washauriwa kufanya kazi

WATU wenye ulemavu wameshauriwa kuacha tabia ya kuombaomba, badala yake watumie vipaji vyao kufanya kazi ili kuondokana na umaskini wa kipato.


Ushauri huo ulitolewa Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo wa watu wenye ulemavu uliojadili ushawishi na utetezi kuhusu ujumuishaji wa haki za wenye ulemavu kwenye mipango ya maendeleo.


Akizungumza wakati wa kuchangia mada, mshiriki wa mdahalo huo, Ally Ngurungu, alisema pamoja na kuingiza masuala mbalimbali ndani ya Katiba mpya ni vema watu wenye ulemavu wenyewe wakajitathmini kwa kuacha kuombaomba, badala yake wajishughulishe ili kuondokana na umaskini.


“Sisi wenye ulemavu ni watu wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi, hivyo ni vema tukatumia vipaji vyetu katika kuhakikisha tunaondokana na umaskini na utegemezi,” alisema Ngurungu.


Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Flora Masue, aliyefungua mdahalo huo aliwataka wenye ulemavu kuhakikisha haki zao za msingi zinaingia kwenye Katiba mpya ili kuondoa dhana ya msaada katika kundi hilo.
Masue alisema umefika wakati kwa watu wenye ulemavu kupigania haki zao za msingi kwa kuhakikisha zinaingia ndani ya Katiba mpya ili kupunguza unyanyapaa uliopo sasa.


Alitaja mambo muhimu wanayotakiwa kupigania ili yaingie kwenye Katiba mpya ni elimu, afya na kilimo, ambayo kwa sasa yanaonekana sawa na hisani ya serikali kwao.


Alisema pia hakuna wajibu bila haki, hivyo aliwataka watu wenye ulemavu kujishughulisha kuliko kusubiri kusaidiwa kila wakati.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Chazi, alisema mdahalo huo ambao umefadhiliwa na Shirika la Foundation For Civil Society, utawasaidia kufikisha maoni yao panapostahili.


Chazi alisema wakati wa kukusanya maoni ya awali kwa ajili ya kutengeneza rasimu ya kwanza ya Katiba mpya watu wenye ulemavu zaidi ya 48,000 nchini kote walipaza sauti zao na kusikika kwa msaada wa shirika hilo, ambapo asilimia 70 ya maoni yao yaliweka kwenye rasimu ya awali.

Wadau wa kilimo watakiwa kufuatilia fedha za miradi

Wadau wa sekta ya kilimo kutoka kata nne za Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya wamekumbushwa wajibu wao wa kufuatilia fedha za miradi ya kilimo zinazotengwa kwa halmashauri ya wilaya ili kuwezesha miradi ya kilimo wilayani humo.


Akizungumza katika mafunzo ya siku nne yaliyowahusisha watendaji wa kata, maofisa ugani na wakulima wa kata nne za Myovizi, Ruanda, Nanyala na Ihanda, Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia ya Good Samaritan ya mkoani Mbeya, Daimon Swai alisema ni wajibu kwa wakulima kufuatilia fedha za miradi ya kilimo zinazotengwa katika maeneo yao.


Alisema mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Foundation for Civil Society yamelenga kuibua fursa za wakulima katika dhana shirikishi baina ya Halmashauri ya wilaya na wakulima ambao muda mrefu wamekuwa hawana uelewa juu ya fedha za halmashauri zinazotengwa kwa miradi ya kilimo.


Swai alisema kuwa kutokana na mafunzo hayo ambayo yamewashirikisha wadau wa kilimo wapatao 100 wa kata hizo yatasaidia kuimarisha sekta ya kilimo ambayo imekuwa ikikosa vipaumbele kutokana na wakulima wenyewe kutojua wajibu wao na kuhoji mikakati ya serikali juu ya dhana ya Kilimo Kwanza.


Naye Mkulima wa kijiji cha Ruanda, Sarafina Simfukwe alisema kuwa katika maeneo yao kumekuwa na matatizo ya mbolea ya ruzuku ambapo serikali imekuwa haieweki uwiano wa mahitaji ya mbolea kulinganana na idadi ya wakulima wa mazao ya chakula na biashara kwa wakati husika.


Ofisa ugani wa kata ya Ruanda, Clay Sarumbo alisema kuwa mgawanyo wa mbolea ya ruzuku unazingatia idadi ya wakulima wanaohitaji katika kata na kijiji na kwamba hata hivyo ucheleweshaji huo unatokana na mgawo kutoka wizara ya kilimo.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo, Daria Rugumira alisema kuwa dhana ya wakulima kujenga tabia ya ufuatiliaji wa fedha zinazotengwa kwa ajli ya sekta ya kilimo zinaamsha ari ya uwajibikaji kwa watendaji wa serikali katika kuendeleza falsafa ya kilimo kwanza. Alisema ni wajibu kwa wadau wa kilimo na wakulima kufuatilia mchakato wa kiutendaji na utoaji huduma hususani katika wakati huu wa kilimo ili kusaidia wakulima kufanya kilimo chenye manufaa na tija.

 

Wanawake watakiwa kugombea uongozi

Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Chamwino (Changonet) umetoa changamoto kwa wanawake wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanajitokeza na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ili kuondoa tatizo la ubaguzi wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi.


Ofisa Ustawi wa jamii Wilaya ya Chamwino, Jaina Msangi alisema hayo wakati wa mdahalo ulioandaliwa ma Mtandao wa Asasi hiyo katika Kijiji cha Majereko huku mada kuu katika mdahalo huo ilikuwa mgawanyo sawia wa rasilimali za nchi unaozingatia usawa wa kijinsia chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society.


Alisema ni vizuri kama wanawake wakagombea nafasi mbali mbali za uongozi katika chaguzi mbalimbali ikiwemo zile za Serikali za mitaa ili kuongeza idadi ya wanawake viongozi.
Alisema vitongoji 12 vya kata hiyo hakuna hata kiongozi mmoja mwanamke hali inayoonesha kuwa wanawake hawajitokezi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.


Pia alisema misingi ya utawala bora inaanzia katika ngazi ya familia ni muhimu kama watoto wakapata fursa ya kupata elimu ili waje kujitegema hapo baadae.
Aidha alisema jamii inatakiwa kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa bila kujali ni wa kike, wa kiume au mlemavu.
Kwa upande wake, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Chamwino, Juliana Kilasara alisema licha ya wanawake kujitahidi kujikwamua katika kujikomboa kiuchumi na kifikra, bado juhudi za makusudi za jamii zinazidi kuonekana kuendelea kuwatafutia wanawake fursa zaidi za kujitawala kwa maendeleo ya jamii.


Alisema ni wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na inayojali utu pasipo na kuwepo tofauti ya kijinsia, hata hivyo ndani ya jamii kuna makabila na makundi ya watu ambayo yanadhani kuwa mwanamke hana haki sawa na mwanaume katika kumiliki rasilimali mbalimbali.


Hata hivyo alisema fikra za aina hiyo ni potofu na hazina tena nafasi katika nchi hivyo inatakiwa kuwa na fikra chanya kuwa wanawake wana haki na sifa zote za kumiliki, kusimamia na kushauri juu ya matumizi bora ya rasilimali za nchi.

Pugu waanza kupata taarifa za maendeleo

WAKAZI wa Kata ya Pugu, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, hivi sasa wanapata taarifa za mapato na matumizi ya fedha za maendeleo kupitia mbao za matangazo kwenye ofisi za serikali za mitaa na kata.


Kupatikana kwa taarifa hizo kumetokana na elimu waliyopata ya namna wanavyotakiwa kushiriki katika kupanga bajeti ya serikali na kufuatilia rasilimali za umma zilizopo kwenye kata yao.


Wakazi wa Pugu waliipata elimu hiyo kupitia Asasi ya Hope Deprived People Action in Development (HDPAD) iliyopewa ruzuku na Foundation for Civil Society.Mkurugenzi wa asasi hiyo, Rehema Sembo, alisema mafunzo hayo yamewafumbua macho wakazi wa kata hiyo ambao awali hawakuwa wakifahamu lolote kuhusu fedha za miradi ya maendeleo.


“Tulikwenda Pugu kwa ajili ya shughuli za watoto yatima, tukiwa pale tukagundua kwamba sh milioni 18 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha Shule ya Msingi Pugu Kaijungeni zililiwa na mwalimu mkuu.
“Kwetu ikawa fursa ya kuwaelimisha wakazi wa eneo lile, kwamba serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kata, ambayo lazima wananchi wafahamu na wafuatilie.


“Hivi sasa wamefunguka, kila mtaa umetengeneza kamati ya watu wanne inayoshiriki kupanga bajeti ya mtaa na kufuatilia matumizi ya fedha wanazopewa,” alisema Rehema huku akiishukuru Foundation.
Foundation ilifadhili mradi kwa kutoa ruzuku ya shilingi milioni 44.9 zilizotumika kutekeleza mradi huo katika kipindi cha miezi 18 kuanzia Januari 2012 hadi Septemba, 2013.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari