Foundation yawezesha mafunzo Juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa Watu wenye Ulemavu Kilombero

Watu wenye ulemavu nchini Tanzania wametakiwa kushiriki katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo kwa mujibu wa uwezo wao.

Akizungumza katika warsha ya siku mbili mjini Ifakara wilayani Kilombero hivi karibuni mwenyekiti wa Chama cha Wasioona (TLB) taifa Mwalimu Greyson Mlanga amesema kuwa ni vyema watu wenye ulemavu wakashiriki katika shughuli hizo ili kusaidia jamii kuondokana na dhana ya kuwa walemavu ni watu omba omba.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa ushirikiano wa vyama vya watu wenye ulemavu ndio njia pekee ya kujikwamua katika maisha huku akisisitiza upatikanaji wa takwimu sahihi za watu wenye ulemavu ili ziweze kusaidia maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Madiwani, Watendaji wa Wawakilishi wa Vyama vya watu wenye Ulemavu, mwenyekiti huyo alielezea umuhimu wa kupata elimu na kujua Haki za watu wenye Ulemavu.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa  na Chama cha Wasioona (TLB) wilaya ya Kilombero yameshirikisha wadau kutoka kata za Ifakara, Kibaoni, Kibegere na Kisawasawa yalifadhiliwa na Taasisi ya Foundation for Civil Society.

Asasi zatakiwa kuelimisha utawala bora

Asasi za kiraia mkoani Ruvuma zimetakiwa kupeleka elimu hususani ya utawala bora na ufuatiliaji wa sheria ya manunuzi ya umma katika maeneo yaliyo pembezoni kwakuwa yako nyuma kiuchumi, kiutawala bora na kwasababu hiyo wananchi wananyanyasika.Wito huo uliotolewa na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mkongotema, Polycarp Malekela wakati akifungua Mafunzo ya Utawala bora na ufuatiliaji wa sheria ya manunuzi ya umma kwa washiriki 50 wa Kata hiyo yaliyoandaliwa na Asasi ya Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Utamaduni (YOCUWODE) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society.
Mratibu wa mafunzo hayo , Margreth Melkion alisema kuwa katika mafunzo hayo wamelenga kutoa kwa Kata sita za Wilaya ya Songea na kwamba wameshafanya kwa Kata nne katika vituo vya Peramiho na Maposeni huku wananchi 100 wakinufaika na mafunzo hayo ambao ni wananchi wa kawaida, viongozi wa Serikali za vijiji na kata.
“Mafunzo haya yanafanyika baada ya kuonekana kuna changamoto ya kutofahamika kwa sheria ya manunuzi ya umma huku kukiwa na rushwa huku Halmashauri za Wilaya ya Songea zikionekana kupata hati chafu,” amesema na kuongeza kuwaq ipo haja ya wananchi kupata mafunzo ili kujua yanayoendelea ili waweze kulinda rasilimali za nchi zisiporwe na mafisadi na kwamba kwa mafunzo hayo watazilinda rasilimali hizo.

‘Wananchi nendeni kwenye mikutano ya vijiji’

Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanashiriki mikutano ya vijiji kama njia ya kuweza kusukuma maendeleo katika ngazi za vijiji na kata.

Mbali na hilo, imebainika kuwa uelewa mdogo walionao wananchi wengi, hasa waishio vijijini, umekuwa ukisababisha ushiriki mdogo katika mikutano ya serikali za vijiji.

Hayo yamebainika wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wananchi, viongozi wa serikali za vijiji, wakulima wadogo na viongozi wa ngazi za vitongoji, yaliyoendeshwa na Mtandao wa wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) wilayani Mkuranga kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society.

Akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sada Mwaruka, aliwataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo kama njia ya kuwaongozea uelewa na kusambaza elimu kwa wananchi wengine.

“Kama viongozi wa vijiji hawafanyi mikutano ya vijiji, basi watambue kuwa wanawanyima fursa wananchi kujadili maendeleo yao na kuibua vipaumbele vyao katika miradi itakayotatua kero zao. “Viongozi wenye dhamana kuitisha mikutano na kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kujadili na kusomewa taarifa za matumizi katika vijiji vyao, kama sheria na taratibu za serikali za mitaa zinavyoagiza,” alisema Mwaruka.

Waomba uharakishwaji kanuni Sheria ya Ukimwi 2008

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeombwa kuharakisha kutunga kanuni za Sheria ya Kuzuia na Kumbambana na Ukimwi ya mwaka 2008 ili iweze kutekelezwa kupambana na unyanyapaa na kupunguza maambukizi mapya nchini.

Aidha, baadhi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wametaka elimu zaidi itolewe  kwa jamii kuhusu Ukimwi ili kuiwezesha nchi kufikia malengo sifuri ya unyanyapaa, vifo na maambukizi mapya ya Ukimwi ifikapo 2015.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya siku mbili kwa watu wanaoishi na VVU na wadau wengine kuhusu sheria hiyo ya Ukimwi, Mwezeshaji wa mafunzo, Japhes Baitan, alisema sheria hiyo haiwezi kutekelezwa kwa kuwa mpaka sasa haijatungiwa kanuni.

“Ili itekelezeke, irudishwe kwa wadau wanaoishi na VVU na jamii, ichambuliwe na Waziri mwenye dhamana atungie kanuni, lengo ni kuwezesha mpango wa kufikia sifuri tatu katika unyanyapaa, maambukizi na vifo vitokanavyo na Ukimwi mwakani, alisema Baitani.

Alisema sheria hiyo inavifungu vizuri vinavyokataza watu kujitangaza wanatibu Ukimwi bila kuthibitishwa na mamlaka husika, inakataza usiri wa wana ndoa kuhusu Ukimwi lakini alisema haijamlenga vya kutosha mtu asiye na maambukizi ajilinde, jambo ambalo wadau katika mafunzo hayo wamegundua kuwa ni moja ya changamoto.

Kwa upande wake, Katibu wa Asasi ya Kijamii ya Kupambana na Ukimwi na Kifua Kikuu (Maukita) iliyoandaa mafunzo hayo na kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society, Juma Garaba, alisema watu wanaoishi na VVU wanahitaji kujua sheria ili kutambua wajibu na haki zao na kuendeleza mapambano dhidi ya unyanyapaa.

Kwa Upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wanaoishi na VVU, Maimuna Hamis (49) na Athumani Mwirangi (40) kwa nyakati tofauti walisema unyanyapaa bado ni tatizo katika jamii na kushauri elimu zaidi itolewe na kuhamasisha watu kupima afya zao ili kujua waishije.

Tangu mwaka 2008 sheria ilipotungwa na kusainiwa na Raisi Jakaya Kikwete, Wizara ya Afya imeeleza kuwa katika mchakato wa kutunga kanuni hizo.

Wananchi Pwani watakiwa kushiriki mipango ya afya

Wananchi wa kata ya Mjawa wilayani Rufiji mkoani Pwani wametakiwa kushiriki katika mipango ya maendeleo katika sekta ya afya na kueleza changamoto walizonazo, ili kuwasaidia wadau na serikali kutatua matatizo yao.


Akizungumza wakati akifungua semina kuhusu utekelezaji wa mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Taasisi ya Chem Chem ya Mabadiliko (Chechema), Daudi Saidi, alisema wananchi wanajukumu la kusim amia na kufuatilia miradi ya umma, hasa katika sekta ya afya. “Wananchi wa Mjawa hawajui umuhimu wa kushiriki katika mipango hiyo, ili wahusike wajue changamoto zilizopo katika sekta hii muhimu”, alisema Saidi.


Alisema, viongozi wa vijiji pia hawajui wajibu wao katika kusimamia rasilimali za umma na kusababisha wananchi kupata huduma mbovu maeneo ya vijijini.Alisema mradi wa wa ufuatiliaji wa matumizi ya pesa za ruzuku utaendeshwa katika vijiji vitano vya kata ya Mjawa kwa miezi mitatu na utatumia sh milioni saba, fedha zilizotolewa na Foundation for Civil Society.


Alisema, Chechema iliamua kutambulisha mradi huo baada ya kugundua kuwa, huduma za afya zilizopo haziridhishi pamoja na kuwa na zahanati ya kata.Alisema, zahanati hiyo ina upungufu mkubwa wa vipimo, dawa pamoja na tiba.

 

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari