Naibu Spika azipongeza AZAKi katika maonyesho Dodoma

Asasi za Kiraia nchini (AZAKI) zimepongezwa kwa kazi nzuri ya utoaji elimu kwa umma wa Watanzania kuhusu masuala mbalimbali ya ya muhimu kwa jamii ikiwemo mchakato wa Katiba Mpya.

Pongezo hiyo imetolewa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai, wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Saba ya Asasi za Kiraia (AZAKI) yaliyoanza Juni 16 katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.

Naibu Spika Ndugai, amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na AZAKI kupitia The Foundation for Civil Societies, katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo kupitia maonyesho ya AZAKi Bungeni, kwa kuwawezesha wadau mbalimbali kukutana, kubadilishana uzoefu, kujifunza na kutafakari mambo mbalimbali kwa lengo la kuboresha maisha na kuleta maendeleo.

Aidha, ametoa changamoto kwa AZAKi kutokazania kuinyooshea Serikali vidole kana kwamba kila kitu ni jukumu la Serikali, na hivyo kutambua kuwa AZAKi pia ni sehemu ya jamii ya Watanzania na zina wajibu mkubwa wa kuchangia maendeleo ya taifa kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo, likiwemo Bunge.

Naibu Spika alisema: “Uwepo wa Asasi za Kiraia ni muhimu kwa ukuaji wa demokrasia na utawala bora katika nchi yetu, hivyo nawapa changamoto ya kujitafakari namna bora zaidi ya kufikisha ujumbe kwa walengwa kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Wabunge na AZAKI, badala ya migongano.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufugua maonyesho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maonyesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TACOSODE, Bibi Theofrida Kapinga, alisema kauli mbiu ya Maonyesho hayo ni “Majadiliano Makini baina ya AZAKI na Bunge ni Msingi Imara wa Maendeleo.” Imejikita katika mtazamo kwamba, mijadala yenye tija baina ya wabunge na wana AZAKI, ni nguzo muhimu na imara katika kuharakisha michakato ya maendeleo nchini kwa kuhakikisha mahusiano na mashirikiano hayo yanazidi kuimarika kwa maendeleo ya taifa.

Bibi Kapinga alisema wana AZAKI, wanafarijika sana kuona Bunge limetambua umuhimu wa AZAKI kwa kuwashirikisha katika mijadala mbalimbali, wa utungaji sera mfano, UKIMWI, MKUKUTA, GESI ASILI, na mapitio ya miswaada ya Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT, Usimamizi wa Kodi, na Muswada wa Fedha.

Maonyesho haya ya saba ya AZAKI Bungeni, yamedumu Kwa siku mbili na yaliratibiwa na TACOSODE kwa kushirikiana kwa karibu na Policy Forum, SIKIKA na HAKI ELIMU, na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society (FCS).

Asasi Busega yasaidia mtoto yatima kuondolewa kwenye ajira mbaya

Huenda mtoto Kaswahili Mathiasi (12) anayeishi katika kijiji cha Busami Wilaya ya Badugu mkoani Simiyu, hubaki akiyakumbuka malezi mazuri aliyowahi kuyapata kutoka kwa marehemu wazazi wake enzi za uhai wao. Ni maisha ambayo hayakudumu sana kwani mambo yalianza kubadilika taratibu baada tu ya wazazi wake kufariki na hatimaye alianza kuuona ulimwengu kuwa katili kwake na maisha kuwa magumu zaidi kutokana na manyanyaso kutoka kwa walezi wake.

Kutumikishwa mashambani na kuchunga mifugo kwa muda mrefu kuliweza kumfanya apoteze haki yake ya msingi ya kujiendeleza na masomo kwa kuwa muda mwingi alikuwa akiutumia katika shughuli hizo.

“Sipendi kukumbuka wakati mateso haya yalipoanza kurindima. Wakati mwingine nilitamani kutoroka na kuondoka kabisa kijiji kwetu, nisirudi tena. Ilikuwa wazi kwamba sikuwa na kitu chochote baada ya ndugu wa marehemu baba kugawana mali za wazazi wetu na kutuacha mikono mitupu,” anasema Kaswahili.

Kaswahili anasema, kitu kilichokuwa kikimpa wakati mgumu ni pale alipokuwa akinyimwa chakula, na wakati mwingine ilimlazimu atoroke shule kwa ajili ya kutafuta ajira ndogondogo ili aweze kujipata chakula.

“Nilikuwa nikilima mashamba ya watu na kulipwa Sh.1000 na wengine waliweza kunipa chakula baada ya kuwa nimemaliza shughuli zao. Kupitia ajira hii niliweza kujipatia kipato kwani sikuwa na mtu wa kumueleza shida zangu wala kunisaidia,” anasema.

“Hapakuwepo na mtu wa kututetea, kwani manyanyaso yalizidi hadi kiasi cha dada yangu kuozeshwa angali akiwa mdogo na mahari kugawana wenyewe kwa wenyewe. Nilikuwa nikijifikiria ninini hasa kilichopo mbele yangu,” anaongeza.

Lakini sasa kuna matumaini mapya katika maisha ya mtoto Kaswahili baada ya kufikiwa na kazi za asasi ya Busega Children & Development Services Assistance (BCDSA) chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS).

Anasema aliweza kukutanishwa na watoto wenzake na kuwa mwanachama wa klabu za watoto zilizoendeshwa na asasi ya BCDSA na kunufaika na huduma mbalimbali zilizorandana na Sera ya Mtoto ya mwaka 1996 na Sheria ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2009.

Kupitia klabu za watoto taarifa zake ziliweza kufikishwa kwa Mtendaji wa Kata ili aweze kuzifanyia kazi. Mtendaji aliweza kufika nyumbani kwao na Kaswahili na kufanya mazungumzo na shangazi yake (jina limehifadhiwa) ambapo walizungumza waziwazi juu ya haki za mtoto, na hatimaye shangazi huyo alikiri makosa na kubadirika.

Wanajamii wengi pia sasa wameanza kulaani vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto na kuonesha kutoridhishwa kwao na vitendo ambavyo  vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wazazi na walezi. Jamii sasa imeanza  kubadilika na kuogopa klabu za watoto ambazo zimekuwa makini kufuatilia watoto wanaonyanyasika.

“Nimejifunza mengi kupitia semina zilizoendeshwa na klabu za watoto. Ushirikiano wa viongozi wa klabu za watoto, viongozi wa asasi na wa Kata katika kuhakikisha wananitembelea katika kijiji ambacho nilikuwa nikiishi ni jambo la kuigwa. Kwa kweli nashukuru kupata mabadiliko katika familia yangu,” anasema kaswahili.

Anaongeza ushirikiano wa klabu hizo na viongozi wa vijiji uliweza kuhakikisha anaweza kwenda shule kama njia moja ya kumpa ahueni kutokana na majeruhi ya kisaikolojia aliyokuwa ameyapata. Wananchi pia walihamasika na kumchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vyake vya shule zikiwemo sare na madaftari.

Hata hivyo uongozi wa kijiji uliamua kufungua kesi katika Baraza la Kata na kuwashitaki walezi wa mtoto Kaswahili juu ya kitendo chao cha kutumia vibaya miradhi iliyoachwa na marehemu wazazi wake pamoja na kutaifisha mahari ya dada yake wakati harusi. Vitu vyote waliweza kuvirudisha yakiwemo mashamba na kulipa fedha za mahari. Viongozi wa kijiji baada ya kuhamasishwa waliweza kupeleka shauri hilo katika Mahakama ya Mwanzo na dada yake Kaswahili akateuliwa kuwa msimamizi wa mirathi pamoja na mali mpaka mdogo wake atakapofikisha umri wa miaka 18.

“Nashukuru klabu za watoto hususani asasi ya BCDSA. Mimi kama yatima sasa naona maisha yangu yamekuwa mazuri kulingana na jamii kuanza kunithamini tena. Najivunia kufika darasa la saba bila matatizo,” anasema mtoto Kaswahili.
Afisa Mtendaji wa kata ya Busame, Mussa Bwiru anasema: “Walezi na wazazi wengi wamekuwa wakiwatishia watoto wao kuwa watawatenga katika ukoo pale wanapobaini kuwa mtoto katoa taarifa juu ya vitendo ya unyanyasaji ambavyo wanamfanyiwa. Hali hii tumeweza kuibadili kwa ushirikiano wa asasi na klabu za watoto baada ya kuwachukulia hatua wale ambao wamebainika kufanya ukatili dhidi yao.”

Kupitia uhamasishaji wa klabu za watoto, watoto 65 wameweza pia kupelekwa shule za sekondari na msingi kutokana na michango ya wananchi pamoja kamati za maendeleo za kijiji na hivyo kufanikiwa kuikabili changamoto kubwa ya tatizo la watoto kutopelekwa mashuleni.

Watoto kutoka kata ya Badugu, wameeleza kunufaika na mradi kutokana na mafunzo waliyofundishwa, wameweza kutambua haki na wajibu wao kwa jamii, sheria zinazomlinda mtoto, wajibu wa wazazi na walezi na pia endapo ukiukwaji wa haki za binadamu utatokea sasa wamejua ni wapi wataanzia kutoa taarifa.

“Mtoto mwenzetu amekuwa akikoseshwa haki kwa muda mrefu. Kupitia klabu hizi zinazosimamiwa na BCDSA tulipata ujasiri wa kuweza kuliripoti jambo hili kwa viongozi wa kata kwa lengo la kumsaidia mwenzetu,” anasema Mtoto Mathias Jackson.
Gadlord Deuli, ambaye ni mratibu wa BCDSA anasema: “watoto 60 waliohudhuria katika semina kupitia klabu zao tayari wamepata haki zao. Sasa wote wanasomeshwa bila ya kuwepo kwa ubaguzi, ndoa za umri mdogo hususani kwa watoto wa kike sasa zimekomeshwa katika eneo letu.”

Mbali na ushawishi uliokuwa ukifanywa, klabu hizo ziliundwa kwa ajili ya kutetea haki ya watoto na kuunda kamati ambazo ziliendeshwa na kusimamiwa na watoto wenyewe ili kupaza sauti za wenzao. Kupitia klabu za wa watoto, watoto sasa wameanza kupata haki zao na wanaweza kushiriki kubainisha kasoro mbalimbali zinazotatiza upatikanaji wa haki zao za msingi.


Walemavu wa macho wapatiwa mafunzo juu ya Haki zao

Watu 50 wenye ulemavu wa kutokuona katika wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wamepatiwa mafunzo kuhusu rasimu ya Katiba mpya, sheria ya watu wenye elmavu na mkataba wa umoja wa mataifa.

Katibu wa Chama cha Wasioona (TLB) wilaya ya Bukoba, Novah Mwijage, amesema walemavu hao wamepatiwa mafunzo hayo kupitia mradi wa mwaka mmoja wa kuwajengea uwezo.

Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Februari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Februari, 2015 ambapo umegawanyika katika awamu nne tofauti.

Amesema kuwa Shirika la Foundation for Civil Society kwaajili ya kutekeleza mradi huo wa kupatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo Rasimu mpya ya Katiba.

Mwijage amesema kuwa katika awamu ya kwanza wanapatiwa mafunzo kuhusu rasimu ya Katiba mpya, awamu ya pili mikataba ya Umoja wa Mataifa (UN) na sheria ya watu wenye ulemavu namba sita ya mwaka 2006.

 


Amesema kuwa idadi ya wasioona wanaohitaji kupatiwa mafunzo hayo ni wengi na kuwa kulingana na ufinyu wa bajeti wameamua kutoa mafunzo kwa idadi ndogo ambao watafundisha wenzao katiaka maeneo wanakotoka.


Mwijage ametaja baadhi ya masuala yaliyobainishwa na watu hao baada ya kupatiwa mafunzo ya rasimu ya Katiba Mpya kuwa katika ibara ya 42 suala la afya na miundo mbinu yao kutoongelewa na kuwa na upungufu huo unatakiwa kufanyiwa marekebisho.

“kuhusu suala la elimu, rasimu hiyo ilitusahau, kwahiyo ombi letu ni serikali kuwapatia elimu bure walemavu ili waweze kujitegemea katika maisha yao badala ya kuendelea kuwa tegemezi kila wakati,” alisisitiza.

Hata hivyo amesema kuwa kama wazee wanapewa dawati lao la kupatiwa matibabu bure, hata watu wenye ulemavu wanatakiwa kufanyiwa hivyo kwa madai kwamba nao ni kundi maalum ambalo idadi kubwa ya watu wasio na uwezo wa kujitegemea. Kwa mujibu wa katibu huyo, kuna wasiiona 115 katika wilaya ya Bukoba.


 

Imani za ushirikina zashamiri Songea

Imani za ushirikina zimetwaja kuchangia kuongezeka kwa matukio ya uhalifu na umaskini ndani ya jamii.

Hayo yamesemwa na Ofisa wa Polisi wa Tarafa ya Songea Magharibi, Alfred Mwanisungule,wakati akifungua mdahalo wa wazee ulioshirikisha watu wa kada mbalimbali ukiwa umeandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Wazee Mfaranyaki kwa ufadhili Wa Foundation for Civil Society.

Amesema matukio ya ushirikina katika Wilaya ya Songea hasa ya kuwatuhumu wazee kuwa washirikina yameshamiri katika Kata za pembezoni mwa Songea kiasi cha kusababisha umaskini ndan ya jamii.


Pia amesema Katika Kijiji cha Subira kuna mganga alikiua akiwagombanisha wanandugu kwa ramli zake na hivyo kuleta uvunjifu wa amani katika jamii na kwamba waganga wa jadi hawataki kupiga ramli bali kutoa matibabu.

Kwa upande wake mmoja wa wazee waliohudhuria mdahalo huo ambaye ni mwathirika wa matukio ya ushirikina, Dafrosa Nyingo, alisema kuwa yeye anaumia sana kwa kugombanishwa na na ramli za waganga wajadi na kuiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria waganga hao.

Nao vijana waliohudhuria katika mdahalo huo wakiongozwa na Frank Fusi, wamesema kuwa wakati mwingine matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana huchangia imani za kishirikina kwani kijana hafanyi kazi na anakuwa maskini na kuanza kuhisi kuwa karogwa.

Maendeleo yatapatikana kupitia PETS

Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya Pugu Poverty Alleviation and Development Agency (PPDA), Bw. Abrahim Silumbu, amesema wananchi wamekuwa chanzo cha kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha kutoka kwa watendaji kutokana na kushindwa kufuatilia matumizi ya Fedha na Rasilimali za Umma (PETS).

Hayo yamebainika wakati mkurugenzi huyo akizungumzia juu ya dhana ya msingi ya ufuatiliaji wa PETS katika kata mbalimbali nchini.

Anasema kuwa ili wananchi waweze kuwa na maendeleo ni wakati sasa wa kuhakikisha kuwa wanafuatilia fedha zinazotolewa na serikali na si kukaa kimya kwani kwani kwa kufanya hivyo ni kurudisha nyuma maendeleo.

Anasema kuwa kuwepo kwa ufuatiliaji wa PETS kutaweza kusaidia kubaini ukweli na kuwasaidia kufanya maamuzi kwa kuwawajibisha watendaji wasio waadilifu na kuimarisha hali ya uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali zingine za umma.
Anasema kuna kila sababu ya kuilaumu jamii kwa kutoshiriki katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha na rasilimali zao na kuchangia kuwepo kwa viashiria vya matumizi mabaya ya rasilimali zao.

Bw.Silumbu anasema serikali imekuwa wazi kwa wananchi wake hasa kwa kutoa mwongozo elekezi wa jinsi ya kufanya ufuatiliaji huo lakini wananchi wamekuwa kikwazo.

Anasema kuwa mwongozo huo umetolewa na Ofisi ya Waziri Mikuu- TAMISEMI Desemba, 2009, ambao unawataka jamii wafanye ufuatiliaji wa matumizi ya fedha na rasilimali zao.


Bw.Silumbu anasema jamii imekuwa ikilalamika juu ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya rasilimali zao lakini hakuna jitihada zozote wanazofanya ili kuweza kupata haki zao.

Anasema kuwa asasi imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kupitia ufadhili kutoka The Foundation for Civil Society (FCS) ambapo mpaka sasa tayari kata za Kitunda, Kivule Msongola na pugu zimefikiwa na mradi huu kwa awamu ya kwanza.  

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari