FCS yatoa ruzuku mpya kiasi cha Sh. Bilion 5.8 kwa AZAKi

The Foundation for Civil Society (FCS) ndani ya Mpango Mkakati wake mpya wa mwaka 2016-2020 imetoa ruzuku kwa Asasi za Kiraia (AZAKi) 120 zinazofanya kazi sehemu mbalimbali nchini huku msukumo ukiwa katika eneo la Utawala Bora na Uwajibikaji. Ruzuku hizi mpya zinazofikia jumla ya Sh. bilioni 5.8 na zinalenga kusaidia utekelezaji wa miradi kwa kipindi cha miezi sita.
AZAKi zilizopata ruzuku zinatarajiwa kuwafikia mamilioni ya Watanzania sehemu mbalimbali nchini na kuchochea matokeo bora katika maeneo ya: Ushiriki wa wananchi; Uimarishaji michakato ya Sera; Ufanyaji Maamuzi kwa Uwajibikaji; na Utoaji bora wa Huduma za Kijamii.
Sekta/ maeneo lengwa yatakayowezeshwa na ruzuku hizi kwa AZAKi ni pamoja na: Elimu; Maji; Haki za Umiliki Ardhi; vita dhidi ya Ukatili wa Kijinsia; Watu wenye Ulemavu; Uwezeshwaji wa Vijana na Wanawake.
Kwa mujibu wa taratibu za FCS, wanaruzuku wote lazima kwanza washiriki mafunzo ya usimamizi wa miradi (MYG) ili kuwawezesha kuboresha viashiria vya miradi yao, matokeo tarajiwa, pamoja na bajeti zao. Pia mafunzo ya MYG yanawapa nafasi wanaruzuku kuandaa mipango kazi na nyenzo za ufuatiliaji na tathmini ili kuweza kupata matokeo vizuri. Mafunzo ya MYG yanafanyika kuanzia tarehe 26-28 Septemba mjini Dodoma.
Baada ya kukamilisha mafunzo ya MYG, wawakilishi wa wanaruzuku wapya watasaini mikataba na FCS kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi iliyofadhiliwa.
Muhimu:
•    Wanaruzuku wapya wa FCS hulazimika kupitia mafunzo ya usimamizi miradi (MYG) – maalum kwa ajili ya kuimarisha uwezo wao wa kutekeleza miradi, kufuatilia na kuripoti vizuri matokeo ya kazi zao. Mafunzo pia huwapa fursa wanaruzuku kuielewa mikataba ya utekelezaji miradi na usimamizi wa fedha.
    ▪    Wadau wa Maendeleo wanaochangia mfuko wa maendeleo wa FCS ni Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC); Ubalozi wa Denmark/DANIDA and NORAD.


FCS yasaini mkataba mwingine mpya wa maendeleo na NORAD

Foundation for Civil Society (FCS) imesaini mkataba mwingine mpya wa maendeleo kutoka Norwegian Agency for Development Cooperation (NORAD) unaofikia kiasi cha Kroner za Norway milioni 10, sawa na Dola milioni 1.2 kwa kipindi cha miaka miwili hadi 2018.

Msaada huu ni nyongeza katika mfuko wa pamoja wa Wadau wa Maendeleo kupitia FCS wenye lengo la kuchangia maendeleo endelevu nchini Tanzania kupitia kujenga uwezo kwa Asasi za Kiraia, ushawishi katika sera na kukuza utamaduni wa kujifunza.

FCS ina dira kuu ya kufikia uwepo wa watanzania waliowezeshwa kupata haki za kijamii na kiuchumi, pamoja na kuboresha hali zao za maisha.

Uchangamfu wa AZAKi katika uundwaji wa Mipango ya Maendeleo ya Taifa

Asasi za Kiraia (AZAKi) zimeshauriwa kuchangamkia michakato ya uundwaji wa mipango ya maendeleo ya taifa ili kuweza kuchochea ushawisi wa pamoja wa mabadiliko na maendeleo katika jamii.

Haya yamesemwa na Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society, Bw. Francis Kiwanga, katika mkutano wa siku moja wa mashauriano lililoandaliwa na FCS kupitia mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/17-2021.

Amezipa changamoto Asasi kushiriki mijadala na kuwa mstari wa mbele katika uundwaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo ya taifa ili kuhakikisha maoni na mapendekezo yao yanajumuishwa katika mipango hii kuliko kuishia kulalamika mara baada ya mipango husika kuwa tayari imekwisha kuundwa.

“AZAKi ni wadau wa muhimu katika mafanikio ya mipango ya maendeleo hususani katika utekelezaji na ufuatiliaji kuanzia ngazi za chini. Kwa hiyo ni muhimu kwa AZAKi kuungana na watunga sera ili kushawishi maboresho na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo hasa huu wa miaka mitano,” amesema Bw. Moses Kulaba, Mwezeshaji wa jukwaa hilo.

“Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, ambao tayari umeshawasilishwa bungeni haukupata maoni kutoka sekta ya Asasi za Kiraia kama mojawapo ya wadau muhimu wa maendeleo Tanzania. Hivyo, jukwaa hili limezitaka Asasi kutoa maoni yao haraka ili kuhakikisha kuwa maoni muhimu ya wananchi ambayo kimsingi bado hayaja ainishwa katika mpango huu, yanaingizwa  katika maoni ya mwisho ya mpango wa maendeleo.

Bw. Zaa Twalangeti, mshiriki kutoka Tanzania Association of NGOs (TANGO) amesema serikali haina budi kuendelea kutambua maoni ya Asasi za Kiraia kwa kuwapa nafasi kutoa maoni yao kwenye mapendekezo ya mwisho ya mpango huo.

FCS yaandaa mchanganuo wa miradi kwa Watu wenye Ulemavu

Foundation for Civil Society (FCS) imewaalika wawakilishi kutoka Mashirika ya Watu Wenye Ulemavu ili kubainisha maeneo maalumu yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kupatiwa ufadhili kutoka FCS kwa mwaka ujao.

Akizungumza katika mkutano huo uliokuwa na lengo la kukusanya maoni ya watu wenye ulemavu juu ya maeneo maalum ambayo FCS inaweza kuyaangalia katika miradi inayokusudia kwa ajili Watu wenye Ulemavu, Bw. Dickson Mveyange, mdau aliyeshiriki kikao hicho alipendekeza maeneo ambayo yatalenga kujenga jamii jumuishi ambapo Watu wenye Ulemavu wataweza kufurahia kutambuliwa kwa kupata haki sawa ya elimu, afya na mahitaji mengine muhimu.

Amependekeza pia kukuza ufahamu kwa jamii kutambua haki za Watu wenye ulemevu na kuondoa unyanyapaa. Pia kama mdau anadhani ushawishi utaamsha Watu wenye Ulemavu kusimama na kukuza mchango wao kwenye jamii.

Kwa upande wake,Luis Benedict kutoka Chama cha Viziwi Tanzania amesema, “Sheria na Sera za Watu wenye Ulemavu zinatakiwa kuangaliwa kwa sababu bado zinakinzana. Pia kuna umuhimu wa kuimarisha na kujengea uwezo wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu, kuviimarisha ili vikue na hata kuweza kujiendesha, mbali ya kukuza ushirikiano baina ya vyama husika.”

Suala la jinsia na afya kwa watu wenye ulemavu ni jambo jingine lililogusiwa ili kupewa mkazo zaidi hususani kwenye masuala ya wanawake na watoto wenye Ulemavu.

 

Ushirikiano wa AZAKi, Umoja wa Ulaya, na nchi wanachama Tanzania waoneshwa

Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society (FCS), Francis Kiwanga ameungana na Mkuu wa Ujumbe wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania, Balozi Roeland van de Geer katika uzinduzi wa kipeperushi kinaonesha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya (EU) na Asasi za Kiraia (AZAKi) Tanzania, kikifafanua azma ya EU kushirikiana na sekta ya AZAKi.

Wakati wa tukio hilo mwanzoni wa mwezi Aprili, jijini Dar es Salaam, Balozi Roeland van de Geer alisema: “Asasi za Kiraia ni muhimu sana na zinaweza kupaza sauti zao kwenye masuala ya utawala bora na demokrasia, kuanzia ngazi za chini na ngazi za kitaifa.”

Mara nyingi, Umoja wa Ulaya umekuwa ukitoa msaada kwa Asasi za Kiraia barani Ulaya na katika nchi nyingi nyingine duniani kote. Kwa kipindi cha mwaka 2014 na 2020, Umoja wa Ulaya pamoja na nchi wanachama imekuwa ikitoa ufadhili wa moja kwa moja kwa kazi za Asasi za Kiraia pamoja na mamlaka za chini kama taasisi za mitaa kwa zaidi ya Sh. Trillioni 50 duniani kote. 

Katika tukio hilo lililohudhuriwa pia na wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), Asasi za Kiraia na pia wadau kutoa sekta binafsi na serikalini, ilitamkwa bayana kwamba Asasi za Kiraia zimekuwa zikiangaliwa kwa jicho la kipekee na hata kupatiwa misaada kutoka Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.

Kwa miaka mingi sasa, Ujumbe wa Umoja wa Ulaya pamoja na nchi wanachama zimekuwa zikijihusisha mara kwa mara na watendaji wa Asasi za Kiraia, kwani AZAKi mahiri zinawakilisha jamii na zinakuza ushiriki na hata kusaidia sana katika kuunda na kusimamia sera kwa ajili ya maendeleo endelevu na ukuaji jumuishi.

Kipeperusi hicho kilichozinduliwa, ambacho kinapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, kinaihabarisha jamii kwa ujumla na hususani Asasi za Kiraia Tanzania juu ya fursa zilizopo kutoka Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake ili kushirikiana zaidi.

Msaada kutoka Umoja wa Ulaya unahamasisha watendaji wa asasi za kiraia kufanya kazi katika kuhakikisha utawala bora na maendeleo jumuishi. Ili kukuza uhusiano baina ya asasi za kiraia na taasisi za mitaa na mamlaka zake chini, Umoja wa Ulaya umetoa nafasi ya majadiliano na hata nyenzo ili kufanikisha mahitaji hayo maalumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Asasi za Kiraia na taasisi za mitaa katika Tume ya Ulaya, Bi Rosario Bento Pais amesema, “Asasi za Kiraia na taasisi za mitaa zinatakiwa kutambulika kama wadau wakuu wa utawala bora. Maendeleo yoyote huanzia ngazi za chini kama inavyoainisha katika Malengo ya Maendeleo Endelevu (MME).

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari