Asasi yagusia umuhimu wa sheria ya kinga ya Hifadhi ya Jamii kwa Walemavu

Furaha ya Wanawake Wajasiriamali kwa Viziwi Tanzania (FUWAVITA) imeiomba serikali kutilia mkazo suala la kinga ya hifadhi ya jamii kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujikwamua kiuchumi pamoja na kujua haki zao.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa mradi wa kinga ya jamii Aneth Gerema alipokuwa akizungumza kuhusu ugawaji wa vitabu vya sheria ya Kinga ya Hifadhi ya jamii kwa walemavu ili kujua haki yao pamoja na kuboresha maisha yao.

Amesema kuwa serikali inatakiwa kuwapatia ruzuku kila mwaka ili waweze kuelimisha walemavu wanawake ili waweze kijitambua pamoja na kujua haki zao katika maeneo mbalimbali.

“Tunaomba serikali itusaidie kwa kutupatia ruzuku pamoja na kuboresha vyombo vya dola katika kulinda walemavu na sheria zao kufuatwa katika nyanja mbalimbali,” amesema Aneth.

Pia wamekuwa wakisambaza vitabu hivyo kwa walemavu wanawake ili waweze kujua haki zao kisheria kutokana na sheria hiyo ya kinga ya walemavu ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho.

“Tumetoa mafunzo kwa walemavu wanawake ili waweze kujua haki zao wanazotakiwa kuzipata pamoja na kuelewa sheria ya kinga ya hifadhi ya jamii kwa walemavu iliyotolewa mwaka 2010” amesema Aneth.

Amesema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ambapo wameweza kufikia wanawake walemavu zaidi ya 450 ambapo walibaini changamoto mbalimbali moja ikiwa walemavu wengi wa pembezoni mwa mji hawajui lugha ya alama.

Hata hivyo amesema mpaka wameweza kusambaza vitabu vya sheria ya kinga ya hifadhi ya jamii kwa wanawake 200 katika wilaya ya Mkuranga na Kisarawe kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society.

Wasichana wapatiwa mafunzo juu ya Sera ya maendeleo ya Wanawake

Wasichana zaidi ya 50 wanaoishi katika kata za Vikindu na Tambani, Wilaya ya Mkuranga imefanikiwa kupata mafunzo yatakayowasaidia kujua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000.

Hayo yamesemwa na mratibu wa mradi unaotoa mafunzo kutoka asasi ya Harakati za Vijana katika Kujiletea Maendeleo kwenye Jamii (YOSSADO), Fatuma Waziri wakati wa kufungua mafunzo hayo.

Amesema lengo la mafunzo ni kuwafundisha wasichana hao kuhusu sera hiyo ambayo awali hawakua wakiijua na kwamba, anaamini mara baada ya kupata elimu hiyo wataweza kufanya shughuli mbalimbali zitakazowasaidia katika kujikwamua na umaskini na kufanya mambo ya kujiletea maendeleo kwenye jamii husika.

Amesema kuwa lengo la taasisi yake kutoa mafunzo kwa wasichana  wa maeneo ayo ni baada ya kubaini kuwa, bado wako nyuma hasa katika masuala ya maendeleo na kwamba wanatakiwa kupata msaada kama huo.

Tumeona tujikite zaidi katika maeneo ya vijijini na kutoa elimu kwa wasichana kutokana na kwamba mwanamke ndio kioo cha jamii lakini pia tumegundua kuwa, mabinti hawa hawajapata elimu kama hii ,” amesema Waziri.

Amesema kuwa , pamoja na kwamba wamepata wakati mgumu siku za mwanzo, lakini wanachoshukuruni kwamba, baadae wasichana hao wamekuwa waelewa na kwa wakati huu wameweza kupata elimu nzuri itakayowasaidia hapo baadae.

“Tunataka baada ya mafunzo haya, hawa ndio wawe mabalozi waelimisham rika wakuu kwa wenzao ambao hatukuweza kuwafikia kwa haraka huko vijijini, wawaelimishe na mwisho wa siku tuwe na watu wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali pamoja na jamii iliyochangamka zaidi”, amesema.

Mradi huo wa kuwapatia mafunzo wasichana umefadhiliwa na The Foundation for Civil Society.

Aidha, amesema YOSSADO ina mpango wa kuwafikia wasichana wengi zaidi katika kata mbalimbali za Wilaya ya Mkuranga, lengo likiwa ni kuwapa mafunzo ya uelimishaji rika ambayo yataweza kuwasaidia kujikwamua Kiuchumi.


 

Jamii yatakiwa kusaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu

Jamii imetakiwa kuwasaidia watoto waishio katika mazingira magumu na kutambua kuwa suala la kuhudumia watoto wa kundi hilo sio la mtu mmoja bali jamii nzima kwa ujumla.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mratibu wa Shirika la Imara Youth Development Centre, Peter Simon katika mafunzo ya siku nne ya kusaidia watoto waishio katika mazingira magumu yalifanyika katika kata ya Kibedya wilayani Gairo mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na washiriki kutoka makundi mbalimbali ya jamii.

Simon amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu ya stadi za maisha na utetezi kwa watoto na vijana ili kujikwamua na umaskini na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kutambua kuwa jamii ina wajibu mkubwa wakukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto waisho katika mazingira magumu.

Washiriki wanatakiwa kufuatilia kwa karibu mambo muhimu kwa watoto hao kama kutoa taarifaya vitendo vya unyanyaswaji kwa watoto pasipo kuoneana aibu katika vyombo husika ambavyo vinatoa huduma za kisheria hasa kwa watoto wafanyao kazi migodini na magulioni alisema.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Peter Kisima  amesema jamii haitilii maanani suala la kuwasidia watoto walio katika mazingira magumu na matokeo yake inaona suala la kuhudumia wazazi na walezi pekee. 

Naye mshiriki wa mafunzo hayo, Davidi Magasha amesema kuwa ili kutoa kipaumbele kwenye suala la kusaidia watoto wa kundi hilo lazima kuwepona mpango wa uanzishaji wa makongamano la kuwasaidia watoto hao ambapo mafunzo hayo yamefadhiliwa na The Foundation for Civil Society.

Wazee waitaka Serikali kutatua kero Zao

Serikali wilayani Nkasi mkoani Rukwa imesema kuwa inatambua changamoto mbalimbali hapa nchini ambazo wazee wanakabiliana nazo na kuwa kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa za kuhakikisha wazee wanaishi katika mazingira ambayo ni salama na uhakika.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Idd Hassan Kimanta alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wazee wilayani Nkasi na kuijua vizuri katiba yao ya asasi ya Wazee na Maendeleo wilayani Nkasi (WAMANKA) chini ya ufadhili wa The foundation for Civil Society.

Amesema kuwa moja ya changamoto kubwa ambayo wazee wanakabiliwa nayo ni suala la matibabu na kuwa licha ya wazee hao kupewa vitambulisho vitakavyowawezesha wao kutibiwa bila malipo bado mpango huo hauonyeshi tija na kuendelea kuwapatia usumbufu wazee wetu na kutopata matibabu halisi na kuendelea kusumbuliwa na maradhi ambayo kimsingi yangepata tiba ya uhakika wazee wangekuwa salama.

Kimanta amesema yeye kama kiongozi wa serikali wilayani Nkasi amekwishaliona hilo na kuwa sasa atafanya mazungumzo na viongozi wenzake wa Halmashauri akiwemo mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ili kuona namna wanavyoweza kuwasaidia wazee hao kwa kuwakatia bima ya afya ya jamii badala ya vitambulisho hivyo ambapo mwisho wa siku huambiwa kuwa dawa hazipo hospitalini.

Amesema kuwa watakaa na kuangalia kama kuna uwezekano wa wazee hao wakatibiwa na bima ya afya ya jamii na serikali kuwachangia kupitia mpango wa tele kwa telena kuwa hilo ndilo litakalokuwa suluhisho la matatizo ya matibabu kwa wazee.
“Hakuna suluhisho katika matibabu ya wazee kama bima ya afya ya jamii maana bima itawasaidia hata kwenda kupata dawa katika maduka yaliyoidhinishwa na hilo nitalipigania ili wazee wote wawe na bima hiyo,” alisema Kimanta.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa changamoto nyingine ya pensheni ya wazee wote lilikwisha fika serikalini na kulitazama kwa kina na kuwa mchakato wake bado upo na serikali bado inafanya utafiti wa kuona ni  namna  gani wao wanavyoweza kufanikisha zoezi hilo la kuwapatia wazee wote pensheni hiyo.

Amewataka wazee kuendelea kuwa na mshikamano ndani yao kwa kujenga umoja wenye nguvu na kuwa wakiwa na sauti ya pamoja ni rahisi kwa serikali kuweza kusikia kilio chao na kukitafutia ufumbuzi wa haraka.

Awali, mwenyekiti wa asasi ya Wazee na Maendeleo (WAMANKA), Victor Sadala amemweleza mkuu huyo wa wilaya changamoto hizo na kuwa serikali wamekuwa wazito sana katika kutatua changamoto mbalimbali walizonazo na ambazo wameipelekea serikali kiasi cha wao kujiona kana kwamba hawana faida tena katika jamii baada ya kuzeeka wakati wao wamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleoya taifa hili.Tanzania inaweza kuwa Kinara wa Uchumi – mdahalo wa AZAKI, Wabunge

Waziri Mkuu Mstaafu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa, amesema Tanzania inaweza kuwa kinara wa Uchumi Ukanda wa Afrika Mashariki kama utajiri wa rasilimali na amani iliyopo vitatumika vyema.

Bw. Lowassa aliyasema hayo Mjini Dodoma Juni 17 kwenye mdahalo kati ya Wabunge na Asasi za Kiraia nchini AZAKI na kusisitiza kuwa, utajiri wa amani na rasilimali zilizopo ni vitu vinavyoweza kuifanya Tanzaniakuwa kinara katika eneo hili.

“Tanzania tuna bahati kubwa ya kuwa na vitu ambavyo wenzetu hawana hususani amani, wenzetu hawana amani kama tuliyonayo, amani hii inatoa nafasi ya kuweza kufanya biashara na shughuli nyingine za kiuchumi bila wasiwasi,” alisema Bw. Lowassa.

Anasema rasilimali nyingi zilizopo kama gesi na madini, kama zitatumika vizuri, zitakuza uchumi wa nchi kwa kiwango  kikubwa ambapo kama kutakuwa na mgawanyo sawa wa matumizi ya rasilimali hizo, Taifa litakuwa na uwezo wa kujiimarisha kielimu na miundo mbinu.

Bw.Lowassa ambaye alikuwa mwenyekiti katika mdahalo huo ambapo wachangiaji wengi walieleza wasiwasi wao na jinsi Tanzania inavyoweza kuingia katika soko la ushindani la Jumuiya ya Africa Mashariki.

“Mimi nasema kuwa, Tanzania tunaweza kuongoza katika soko la ushindani la Afrika Mashariki..hatuna sababu ya kuwa na wasi wasi kama changamoto hizi zitafanyiwa kazi,” alisema Bw. Lowassaambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje ya Bunge.

Semina imeandaliwa ili kuwapa ufahamu Wabunge juu ya shughuli na changamoto ambazo asasi hizo za kiraia inakabiliana nazo ambapo asasi hizo pia zinafanya Maonesho katika Viwanja vya Bunge yakihusisha kazi za mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari