Asasi Mtwara yahimiza Wazazi kufuatilia Mahudhurio, Maendeleo ya watoto Shuleni

Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kushirikiana na walimu katika kuhakikisha wanafuatilia  maendeleo na mahudhurio ya watoto wao shuleni.

Wito huo umetolewa na mwezeshaji, Baltazar Komba, katika mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na taasisi ya Volunteeer for Youth in Health Development (VAYOHEDE) ya kuwajengea uwezo watendaji kutoka sekta ya elimu kata ya Vigaeni , yakiwahusisha maofisa wa elimu wa kata , watendaji wa mitaa, Ofisa Mtendaji wa Kata, Wajumbe wa bodi ya shule ya sekondari, wazazi na wanafunzi yaliyofadhiliwa na The Foundation for Civil Society.

Komba, amesema ili mwanafunzi aweze kufanya vizuri shuleni au kujifunza vizuri, ni wajibu wa wazazi na walezi kushirikiana na walimu vizuri kuhakikisha anafika shule na anashiriki katika ufuatiliaji wa watoto wao.

“Wazazi ama walezi, wamesahau jukumu la kuwafuatilia watoto wao maendeleo ya shule ila wao wanajua jukumu muhimu la kumnunulia mahitaji ya shule tu, kazi zote za kujua maendeleo ya mwanafunzi wanawaachia walimu peke yao.

“Kinachotakiwa sasa wazazi na walezi kuona umuhimu wa kuwafuatilia watoto wao kwa kuwa nao karibu na mtoto anaporudi nyumbani, aangalie maendeleo yake kama leo mtoto ameandika nini na katika mambo hayo aliyoandika je ni vitu gani ambavyo amesahihisha kwa mwalimu au amekutana na mwalimu moja kwa moja” ameongeza Komba.

TAS yaomba ulinzi zaidi kwa Albino

Chama cha Maalbino (TAS), kimeiomba serikali iongeze ulinzi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kutokana na maisha yao kuwa hatarini.

Haya yamesemwa  hivi karibuni jijini Dar es Salaam na katibu mkuu wa TAS,  Zakia Nsembo juu ya vitendo vya kinyama vilivyoripotiwa kufanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Tabora na Simiyu ambako watu wasiojulikana waliwakata baadhi ya viungo vyao na kutokomea navyo na wengine kuuawa.

Chama cha Maalbino (TAS) ni shirika lisilo la kiserikali linalopigania maslahi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kwa miaka kadhaa iliyopita limekuwa ikipatiwa ruzuku kutoka Foundation for Civil Society ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi nchini. 

Zakia amesema vitendo hivyo vimeanza kushika kasi tena kama ilivyokuwa kipindi kilichopita hali inayowafanya albino washindwe kufanya shughuli zao zinazowapatia riziki huku watoto wenye ulemavu wa ngozi pia kushindwa hata kwenda shule.

Hivi karibuni Susan Mungi (35) ambaye ni albino mkazi wa kijiji cha Buhelele kata ya Nsimbo wilayani Igunga, alikatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho.

Katika tukio hilo mume wa Susan, Mapambo Mashili, aliuawa kikatili kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.

Tukio hilo limekuwapo wiki moja baada ya mtoto Upendo Sengerema (15) mkazi wa kijiji cha Usinge kata ya Uganza wilayani Kaliua mkoani Tabora kukatwa mkono na wahalifu ambao pia walitokomea kusikojulikana.

Mdahalo waibua udhaifu wa uongozi vijijini

Kutokuwapo kwa uadilifu miongoni mwa watendaji wa vijiji, uelewa mdogo wa wananchi juu ya masuala ya utawala na wanasiasa kutoshiriki katika mikutano ya vijiji ni miongoni mwa mambo ambayo yanafanya dhana ya utawala bora kutofikiwa.

Hayo yameelezwa na wakazi wa kata ya Nanyamba mkoa wa Mtwara walipokuwa wakichangia mada katika mdahalo wa utawala bora na uwajibikaji uliofadhiliwa na The Foundation for Civil Society ambapo zaidi ya wakazi 250 walihudhuria na kutoa maoni yao.

Akichangia mada katika mdahalo huo, Mohamed Mwalimu mkazi wa kijiji cha Namkuku, amesema kuwa wananchi wengi vijijini hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa mikutano ya vijiji au vitongoji, jambo ambalo linafanya washindwe kuhudhuria hata pale viongozi wanapoitisha mikutano hiyo.

Shamte Ahamad  mkazi wa kijiji cha Dinyecha alisema kuwa kutokuwapo na uaminifu kwa baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji ni sababu ya wananchi kuamua kususia mikutano ya vijij na vitongoji na kwamba elimu inapaswa kutolewa kwao na watendaji wawajibishwe pale inapobainika kutumia rasilimali za umma kinyume na utaratibu.

“Utakuta wananchi wanakwenda katika mikutano lakini inapofika ajenda za kusomewa mapato na matumizi mizengwe inaanza na hapo vurugu hutokea na kwasababu hiyo wananchi wanaona haina haja ya kushiriki katika miktano hiyo ingawa ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo yao na utekelezwaji wa dhana ya utawala bora,” amesema Shamte.

Hadija Lyangunde, mkazi wa kijiji cha Nanyamba, anasema kuwa kutoshiriki kwa wanasiasa katika kuhamasisha wananchi kwenda kwenye mikutano ya vijiji na vitongoji ni moja kati ya sababu zinazochangia wananchi kutohudhuria katika mikutano hiyo.

Hadija amesema iwapo wanasiasa watashiriki vema na kutimiza wajibu wao wa kuhamasisha wananchi mahudhurio katika mikutano hiyo yatakuwa mazuri na kasi ya maendeleo vijijini itaongezeka na hivyo ile dhana ya utawala bora kukamilika.


Akitoa mada katika mdahalo ulioandaliwa nashirika la Saidia Jamii Kuishi (SAJAKU), Said Swallah, amesema kutekelezwa kwa dhana  ya utawala bora kunakamilika kwa viongozi kuitisha mikutano na wananchi kushiriki ipasavyo.

Swallah amesema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana mahali ambapo utawala bora hautekelezwi hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kulingana na majukumu aliyonayo kiutekelezaji katika kutimiza dhana ya utawala bora.

Akifungua mafunzo hayo, diwani wa kata ya Nanyamba, Hassan Mauji, amewakumbusha wenyeviti wa vijiji juu ya umuhimu wa kuitisha vikao na mikutano mikuu ya vijiji na kuweka mihutasari ambayo itafikishwa katika vikao vya kamati ya maendeleo ya kata ili kuwezesha mipango ya vijiji kutekelezwa na halmashauri ya wilaya.

Mauji amesema kuwa kutoitisha mikutano si tu ni ukiukwaji mkubwa wa utawala bora, lakini pia kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

“Kimsingi hili jambo limekuwa ni tatizo kubwa katani kwetu, tumeshuhudia wananchi wakiwatimua viongozi wao kwa madai ya kutoitisha mikutano sasa hili si jambo jema.... nimekuuwa nikiendesha mikutano ya maendeleo ya kata mimi kama mwenyekiti wa kamati hiyo, lakini utakuta kijiji hakina mihtasari hii maana yake ni kwamba hawajafanya mkutano” amesema Mauji.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi akifungua mafunzo hayo katibu mtendaji wa SAJAKU, Nashiri Pontiya, amesema kuwa lengo ni kuibua mijadala juu ya dhana ya utawala bora.


Semina yawaamsha wadau wa elimu Ruangwa

Wadau wa elimu Wilayani Ruangwa mkoani Lindi,wamesema kuwa haikuwa rahisi kwao kufika katika ofisi za serikali na kuhoji matumizi ya rasilimali za umma zikiwemo fedha zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu kwasababu ya kukosa elimu.

Hayo yamesemwa wakati wa semina ya mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wananchi, AZAKI na viongozi wa dini kutoka kaika kata saba za mradi wa mwaka mmoja wa Kuwajengea Uwezo Wananchi na Bodi za Sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa unaoratibiwa na Asasi ya Kuunganisha Vijana Kimaendeleo Ruangwa (AKUVIKIRU) unaofadhiliwa na The Foundation for Civil Society.

Wananchi hao kutoka katika kata saba za Namichinga, Nambiranje, Nkowe, Likunja, Chinongwe, Makanjiro na Ruangwa walikiri kuwa hawakujua kama wana  haki ya kikatiba ya kuhoji, kufuatilia na kusimamia miradi yote ya maendeleo katika sekta ya elimu ya Sekondari ili ijengwe kwa ufanisi na ikamilike kwa wakati.

Mussa Mchupila amesema kabla ya kuhudhuria mafunzo mafunzo hayo wananchi wengi hawakuwa na uwezo wa kuwakabili wajumbe wa bodi za sekondari hasa wakuu wa shule na kuwauliza kinachoendelea katika miradi inayojengwa katika shule zao.


“Sasa nina uhakika baada ya hapa kila mmoja wetu atakuwa na faida ya kutambua wajibu wake katika kusimamia rasilimali za umma (PETS), kuhoji maendeleo ya taaluma ya wanafunzi na wajibu wa walimu katika kufundisha,” amesema Mchupila kutoka kijiji cha Nandandara kata ya Matambarale (zamani Nachingwea).

Mshiriki mwingine Paulina Mmuya kutoka kijiji cha Likangara kata ya Namichinga amesema mafunzo yamewafumbua wengi ikiwemo kujua kiasi cha fedha kilichopangwa kwaajili ya maendeleo ya sekta ya elimu ya sekondari ambacho ndiyo chimbuko la mradi wenyewe.

“Tumejua kuwa katika kipindi cha mwaka 2011 na 2013 wakati mradi huu unaombewa fedha, elimu ya Sekondari Wilayani Ruangwa ilitengwa sh. 67,000,000 sawa na asilimia 4 tu ya bajeti nzima ya maendeleo ya mwaka huo ambayo ni shilingi bilioni 2 ili kujenga nyumba moja ya mwalimu na matundu ya vyoo katika shule tatu,” alisema.

Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Moris Lyimo aliwataka washiriki kuacha woga na kutambua kua wanao wajibu kisheria na kufuatilia na kuhoji mambo mbalimbali ili shule zao zipate maendeleo.

Mratibu wa mradi huo, Abdul Mitumba amesema ni muhimu wajumbe wakatambua kuwa siyo lazima fedha zinazoelekezwa katika shule zao zinaliwa, lakini wanaweza kubaini endapo watajua kama serikali imetenga kiasi gani cha fedha za maendeleo zilizotengwa kwaajili ya shule zao vinginevyo itakuwa vigumu kukubaliana na ubadhirifu kama utatokea.

“Ufuatiliaji wenu makini  utakaotoa majibu ya kama waliopewa madaraka ya usimamizi wanatenda haki katika matumizi ya fedha na mali nyingine za umma kwa faida ya wote au la,” aliongeza Mitumba.

Haiwezekani wananchi na mnaona ujenzi usiozingatia ubora wa maktaba, madarasa au nyumba za walimu katika shule zenu, halafu mnanyamaza kimya, hapo umuhimu wa uwepo wenu utakuwa wapi?!alihoji.Watoto 160 wapewa elimu ya malezi bora

Asasi ya Elishadai Children Foundation kupitia ufadhili wa The Foundation for Civil Society imefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa watoto 160 kutoka wilaya ya Simanjiro, kata ya Sokoni na Terrat  kuhusiana na suala zima la malezi.

Hayo yameelezwa na mratibu wa asasi hiyo William Mwenda wakati akiongea na wafanyakazi,wadau wa asasi wakati wakipewa mafunzo maalum ya kuweza kulea.

Mwenda amesema kuwa watoto hao wamefanikiwa kupewa elimu kwa kipindi tofauti tofauti ambapo malengo makuu ilikuwa ni waweze kufahamu mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Amesema kuwa elimu waliyopewa ni pamoja na maadili mema,kujitambua, wajibu wao kwa jamii na ambapo mpaka sasa wapo baadhi ya watoto ambao wamepata elimu hiyo na kubadilika.

“Tangu tumetoa elimu hii kwa watoto wa kata hizi mbili kuna mabadiliko hata wazazi wenyewe wanakiri hilo lakini pia tunajivunia kwenda mbali zaidi na hata ikiwezekana kwa kanda hii kwani wakati mwingine ukosefu wa elimu kwa watoto ni chanzo cha mahangaiko na mmomonyoko wa maadili,” aliongeza Mwenda.

Katika hatua nyingine amesema kuwa ili nchi iweze kuwa na maadili mazuri kwa watoto na vijana ni lazima jamii kwa kushirikiana na asasi binafsi ziweze kujenga utaratibu wa kuwasaidia hasa kwa kuwapa elimu mbalimbali ikiwemo elimu ya maadili.

Awali mwezeshaji wa mafunzo hayo, Javes Sauni alisema kuwa ili asasi mbalimbali ambazo zinahusika na malezi ya watoto na jamii kwa ujumla zisonge mbele ni lazima asasi hizo ziwe na mwongozo ambao unakubalika kuanzia ngazi ya serikali hadi kwa wafadhili.

Amedai kuwa wakati mwingine asasi zinashindwa kufikia malengo yake hasa ya kutoa elimu kwa jamiii kwa kua wanakosa miongozo pamoja na utumiaji mbaya wa misaada kutoka kwa wafadhili.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari