Asasi Njombe yasaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu

Mtoto Petro Kayombo (5) anayetoka kwenye kijiji cha Boimanda, Kata ya Matola katika Halmashauri ya Mji Njombe ameokolewa maisha baada ya mama yake mwenye matatizo ya akili kubebeshwa mimba na hatimaye kujifungua mtoto huyo.

Kupitia kituo cha kulelea watoto wasiojiweza cha The Compassion Foundation kilichopo mkoani Njombe katika hali isiyotarajiwa kimefanikisha kuokoa maisha ya mtoto Petro kayombo aliyekuwa kwenye hali mbaya kiasi cha kutapakaa funza mwilini mwake.

Baada ya kuzaliwa mtoto Kayombo, familia ya mama yake mzazi iliamua kumchukua na kumlea katika mazingira magumu sana, baada ya bibi yake ambaye ni kipofu na babu yake kuwa mgonjwa mwenye matatizo ya kuvimba tumbo kwa muda kukosa uwezo wa kumhudumia mtoto huyo, jambo ambalo lilipelekea wazee hao kumfungia ndani ya nyumba yao kwa muda mrefu huku akiwa mwenye afya iliyodhoofika sana na kukosa lishe.

Familia iliyokuwa ikiwazunguka wazee hao haikuweza kubaini hali hiyo, licha ya kwamba walichukulia kuwa hakukuwa na tatizo lolote ambalo wangepaswa kuisaidia familia ya mtoto huyo.

Akisimulia mkasa huo, Mratibu wa mradi wa kituo hicho, Lucia Mlowe ameeleza kwamba, “mara baada ya kugundulika kwa walezi wa Kayombo kuwa kwenye maisha magumu, waliamua kumchukua babu wa mtoto Kayombo na kumpeleka katika hospitali ya Consolata Ikonda iliyopo wilayani Makete, mkoani Njombe kwa ajili ya matibabu”.

Mratibu huyo amesema mtoto Kayombo amekutwa wakati asasi hiyo ya The compassion Foundation chini ya ufadhili wa The Foundation For Civil Society inatekeleza mradi wa kuijengea jamii uwezo juu ya kuunda mitandao ya usalama ili kurahisisha utoaji misaada kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Mlowe amesema kuwa kupitia mradi huo wa miaka mitatu , mikutano 18 ilifanyika katika kata za Lugenge, Matola, Luponde, Makoo, na Iwungilo ambapo kamati ziliundwa katika vijiji na zilizokuwepo basi ziliendelea kujengewa uwezo wa kujua kinachotakiwa kufanyika.asasi pia imeweza kutoa mafunzo ya uwajibikaji kutoka idara mbalimbali za halmashauri ya mji wa Njombe ili kutambua nafasi ya Halmashauri katika kuwatunza watoto waishio katika mazingira magumu.

Katika mikutano hiyo kamati hizo zilipata pia nafasi ya kujifunza namna ya kuanzisha mifuko kwa ajili ya kusaidia watoto hao, si kwa chakula na mavazi tu, lakini pia katika kuwaendeleza kielimu kwa ajili ya kujisimamia wenyewe na kwa ajili ya manufaa yao ya baadae.

“Jamii zilizopata mafunzo haya tayari zimekwishabuni miradi mbalimbali ambayo ina wasaidia watoto kwa mfano kufuga kuku au wanyama wadogowadogo ambao watauzwa na fedha itapatikana,” alisema Mlowe.

Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Venance Msungu alikiri kuwepo kwa semina hiyo na kueleza kuwa imeleta manufaa makubwa watumishi wa halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwaona watoto hao kama sehemu ya majukumu ya halmashauri hiyo.

 “Tumeshatoa tamko katika Kata zote kuwataka wananchi kujitolea kuwalea watoto hawa na kubuni njia mbalimbali zitakazowasaidia kuendelea kielimu,” alisema Msungu.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo yaliyotolewa na asasi hiyo Menrad Mgaya alisema kuwa kwa ujumla, jukumu la kuwatambua watoto waishio katika mazingira magumu kwa muda mrefu limekuwa likiachwa mikononi mwa familia bila kujua kuwa jamii pia ina nafasi yake katika hilo.

Kwa upande wake mwalimu wa Shule ya Compasion, Emmanuel Ndengea alisema kuwa tayari shule hiyo ina wanafunzi 22  na wanne wameshamaliza ambao walipatikana kutokana na mradi huo na kwamba tayari wameshaanza masomo na kwa kiasi kikubwa wamebadilika sana tofauti na walivyofika shuleni hapo.

“Tunashukuru wazazi wachache wanaoleta watoto wao shuleni hapa kwa sababu wanachokileta ndicho wanafunzi hawa wanagawana na wenzao, hatuna mfadhili mwingine kwa ajili ya malezi ya hawa watoto kwa hiyo ni kuguswa tu kuwasaidia,” alisema Dengea.

Mtoto Kayombo na dada yake wanaendelea kupata malezi ikiwemo ya kuwezeshwa kielimu katika shule ya Compassion iliyopo mjini Njombe huku taratibu nyingine zikifikiriwa kufanywa ili kuweza kuisaidia familia yao, akiwepo na mama yao ambaye hivi sasa anaishi kijijini kwao Boimanda.

Wananchi wahimizwa umuhimu wa kuandika Wosia

Ili kupunguza unyanyasaji wa wanawake, watoto na migongano ya wanafamiliakugombea mali kiwemo ardhi kuna haja kwa jamii kujengewa uwezo ili kuona umuhimu wa kuandika wosia.

Wito huo umetolewa hivi karibuni wilayani Korogwe na Mratibu wa shirika la WOWAP Tanga, Neema Mwanga alipozungumza na wasaidizi 40 wa kisheria vijijini kwenye warsha yakubadilishana uzoefu kuhusu Mradi Haki, unaolenga kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kuzingartia kanuni mbalimbali  za kisheria ikiwemo uandishi wa wosia.

Amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo unaotekelezwa kwa mwaka mmoja kwenye vijiji unaofadhiliwa na The Foundation for Civil Society mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwemo upatikanaji wa hatimiliki za kimila za kumiliki ardhi.

“Kutokana na hali ilivyo sasa ni wazi kwamba kuna kuna kila sababu kwa jamii hasa viongozi wa kaya kuelimishwa kwa kujengewa uwezo katika masuala haya ya uandishi wa wosia kabla ya kufariki ndipo tutapunguza migogoro inayohusu masuala ya mirathi miongoni mwa jamii zetu,” amesema.

Wasaidizi hao wakisheria waliteuliwa na wananchi wenyewe kutoka kwenye maeneo yao ili kuweza kupatiwa mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kutumika kushughulikia migogoro mbalimbali ya familia na jamii kwa ujumla inayoibuka mara baada ya mmiliki wa mali kufariki.

Mdahalo wahamasisha wananchi Kasulu kudai hati za kimila za ardhi

Kutokuwepo kwa hati miliki za ardhi katika maeneo mbalimbali katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kumesababisha wananchi wengi hasa vijijini kunyang’anywa maeneo yao na serikali au wawekezaji bila ya kulipwa fidia stahiki.
 
Lakini mara baada ya muungano wa asasi za kiraia kupitia Kasulu Non-Government Organisation Network (KANON) kuingilia kati na kufanya midahalo juu ya sheria za ardhi katika baadhi ya vijiji wilayani humo wananchi wengi sasa wameanza kutafuta hati miliki za ardhi za kimila.

Mmoja wa wanufaika wa mdahalo huo, Thobias Mhanuzi, anasema kupitia midahalo iliyoendeshwa na Kanon chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) wananchi wameweza kufahamu umuhimu wa kuyahalalisha maeneo yao kisheria kwa kutumia hati za kimila, na hivyo kutambua wajibu na haki yao katika umiliki wa ardhi pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi.

Anasema awali sheria ya ardhi namba nne na tano ya mwaka 1999 haikufahamika vizuri miongoni mwao lakini mara baada ya kupata uelewa kila mwananchi amejitambua na kuanza kufuatilia masuala mbalimbali yanayohusiana na ardhi katika eneo lao.

Naye Neema Maulid, mnufaika mwingine wa mdahalo ulioendeshwa na KANON anasema: “Utakuta wananchi tunamiliki maeneo lakini baadaye inakuja serikali au mwekezaji anapewa maeneo na sisi tunaamuliwa kuondoka au kulipwa fidia kidogo. Sasa hili limetuvunja moyo sana. Ni muhimu sasa wananchi tukapatiwa hati za kimila za kumiliki maeneo yatu ili kuepuka matatizo kama hayo.”
 
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa KANON Bw.Gerald Nkona anasema lengo la midahalo hiyo ambayo ilifanyika katika wilaya ya Kasulu na wilaya ya Buhigwe ilikuwa ni kuwaelimisha, kuwashirikisha na kuwahamasisha wananchi wa kawaida, viongozi wa kuchaguliwa na watumishi wa serikali kushiriki kikamilifu katika kutambua wajibu wao katika masuala ya umiliki ardhi.

Anasema takriban wananchi elfu moja wamenufaika na mpango huo, hali ambayo imeifanya serikali kupitia baraza la madiwani kuona umuhimu wa kutoa hati za kimila za umiliki wa ardhi kwa wananchi.

Anasema KANON imejifunza mengi kutokana na midahalo hiyo ikiwa ni pamoja kubaini kuwa viongozi wengi hasa wa vijiji na kata walikuwa hawatambui vizuri wajibu wao kwa wananchi katika kuwasaidia kupata suluhu ya matatizo yao yanayohusu umiliki wa ardhi.
 
Naye afisa mazingira katika wilaya ya Kasulu, Edwin Kunyekwa, anasema halmashauri imeanza utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi kijijini anamiliki kisheria eneo lake na anaweza kulitumia eneo hilo kujiendeleza. Lakini pia anasema mpango huo utawezesha kupangwa kwa maeneo ya maalumu kwa ajili ya kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za umma na hivyo kuepusha mwingiliano na migogoro.                                                                 

Asasi yalaani wananchi kujitwalia ardhi bila kufuata sheria

Tabia ya kujitwalia ardhi kwa nguvu bila kufahamu hatia yake kisheria, inayofanywa na wananchi wengi hasa vijana, imetajwa kuwa moja ya sababu kuu za migogoro ya ardhi mkoani Pwani.

Utafiti mdogo uliofanywa hivi karibuni na asasi ya Youth Partnership for Health Environmental Conservation (YOPAHEDO), umegundua kuwa migogoro ya ardhi inayoendelea mkoani humo inatokana na wananchi wengi hasa vijana kutofahamu haki zao za msingi juu ya umiliki wa ardhi pamoja na sheria ya ardhi kwa ujumla.

Akizingumza mjini Mlandizi, Kibaha katika semina ya kukuza uelewa wa Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 – namba 4 na 5, iliyofadhiliwa na Foundation for Civil Society, mratibu wa YOPAHEKO, Frank Samson amesema uelewa mdogo wa masuala ya ardhi kuanzia ngazi ya familia ndio chanzo kikuu cha migogoro katika jamii.

“Watu wamekuwa wanapoteza muda mwingi kufuatilia migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Migogoro hii ingeweza kuepukika endapo kungekuwa na ufahamu juu ya suala hili nyeti,” amesema.

Akichangia kwenye mdahalo huo, mkazi wa kata ya Mlandizi, Zuhura Sesema, aliibua suala la migogoro kati ya wakulima na wafugaji, na kisha kuiomba Serikali kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya makundi haya mawili.

“Mpaka sasa kuna vijiji ambavyo bado havijaingizwa katika mpango wa matumizi maalum ya ardhi, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa huchochea migogoro hii kati ya wakulima na wafugaji,” alisema Zuhura.

Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo na mkazi wa kata ya Ruvu, Nae Namnyaki, alisema wazawa wamekuwa wakiuza ardhi kiholela na matokeo yake kukosa maeneo hata ya kuhifadhi mifugo yao, na hivyo kuchochea migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji.

Washiriki wengine wa mafunzo ya sheria ya ardhi mkoani Pwani wameomba mipaka ya ardhi iheshimiwe na pia Serikali kuwashirikisha kikamilifu wakulima na wafugaji katika kusuluhisha migogoro ya ardhi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa asasi wa miezi mitatu juu ya Sheria ya Ardhi kwa wakulima na wafugaji wa kata ya Mlandizi, Ruvu na Pangani itakayogharimu kiasi cha shilingi milioni saba.

 

NGOs zisizosajiliwa, kufuata utaratibu kuchukuliwa hatua

Serikali itawachukulia hatua za kisheria watu wote wanaoendesha shughuli za Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) bila usajili ama kufuata utaratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Idara ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Marcel Katemba, amesema mashirika yote yanayoendesha shughuli za kijamii kwa tafsiri ya NGOs yanapaswa kusajiliwa au kupata cheti chini ya sheria husika.

Amesisitiza kuwa ili asasi iweze kufanya kazi nchini inatakiwa kwanza kupata usajili na idhini yenye mamlaka kisheria.

Bw. Katemba amesema asasi yeyote ambayo bado inafanya kazi kinyume na taratibu inatakiwa kusimama mara moja la sivyo itakumbana na mkondo wa sheria.

Pia amezitaka asasi za kiraia kuhakikisha kuwa kila mwaka zinawasilisha taarifa zao za mapato na matumizi kwa msajili wa NGOs wizarani kwa mujubu wa sheria, na kuongeza kuwa asasi yeyote itakayoshindwa kutimiza utaratibu huo kwa miaka miwili mfululizo itakuwa imejifuta yenyewe.

“Kila asasi inatakiwa kufuata sheria bila kufungamana na imani za kidini au chama cha siasa kwa kuwa hayo yote pia ni kinyume na muongozo wa sheria za NGO,” alisema na kuongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakao kiuka maagizo – ikiwa ni sambamba na kuzifungia mara moja asasi zote zitakazoenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Bw. Katemba amesema kwa kuhakikisha usimamizi imara wa kazi za asasi, Maafisa Maendeleo wa Wilaya na Mkoa watakabidhiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa kila asasi katika maeneo yao inajiendesha kwa mujibu wa taratibu hizo zilizowekwa.

Aidha, amesema NGOs/ Asasi za Kiraia zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii kwa ujumla na hivyo Serikali inashirikiana nazo ili kuzijengea mazingira wezeshi katika shughuli zake.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari