Watendaji wa serikali za mitaa wadaiwa kupinga mradi wa PETS

Watendaji katika idara za kiserikali huona mradi wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma (PETS) kama mwiba kwao ingawa mtandao wa Asasi zisiszo za Kiserikali wilayani Nkasi mkoani Rukwa (NKANGO) umesema utaendelea kutoa elimu ya mradi huo.

Mwenyekiti wa NKANGO, Victor Sadalla amesema watendaji wengi katika idara za Kiserikali, hawaupendi mradi wa PETS kwakuwa wanaamini ni mradi unaolenga kufichua maovu yao kwa jamii wanayoitumikia kwa kuwafumbua macho wananchi.

Haya yamesemwa kwenye warsha ya siku mbili ya mafunzo ya mwongozo wa PETS chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society, kwa viongozi wa asasi zinazounda mtandao wa NKANGO na Maofisa Watendaji katika ngazi za vijiji na kata za wilaya hiyo. Sadalla amesema mradi huu unalenga kuboresha utendaji kazi wa idara za kiserikali.

Amesema pamoja na changamoto za kutokubalika kwa mradi wa watendaji, mtandao utaendelea kutoa elimu hiyo na kuwataka watendaji katika idara za kiserikali kutambua kama kichocheo cha maendeleo.

Ofisa Tawala wa wilaya ya Nkasi, Mwanaisha Luaga akifungua warsha hiyo, amesema PETS haipo kumuhukumu mtu bali kufichua mambo yasiyo sawa katika utendaji na wanaochukia hawatambui umuhimu wake.

“PETS haimuhukumu mtu, ipo kutoa changamoto kwenye utendaji kazi wetu wa kila siku. Sisi kama watendaji kwenye  Serikali za Mitaa tunapaswa kuona mradi huu kama chombo chenye manufaa kwakuwa kinatukumbusha hata pale baadhi yetu tunapojisahau,” amesema Mwanaisha.

“Ni Imani yangu kuwa kadiri elimu inavyoendelea kutolewa, kama vile wananchi wanavyotambua umuhimu wa kufuatilia matumizi ya rasilimali zilizopo ndivyo na sisi watendaji tutaendelea kutambua umuhimu wa mradi huu na kuanza kutoa ushirikiano,” amesema.

AZAKi zatakiwa kuhamasisha mtangamano wa Afrika Mashariki

Mgeni Rasmi katika Tamasha la tatu la Asasi za Kiraia Tanzania, Dk. Josephat Kweka, amezitaka Asasi za Kiraia (AZAKi) katika ukanda wa Afrika Mashariki kutumia nafasi zao vizuri kuhamasisha mtangamano wa Afrika ya Mashariki kwa kuelimisha wananchi juu ya fursa zinazoweza kupatikana kupitia mtangamano huo.

Dk. Kweka ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark EastAfrika, amesema taasisi yake inathamini sana mchango wa Asasi za Kiraia katika kuhamasisha kukuza mazingira ya biashara na hatimaye mtangamano wa Afrika ya Mashariki, kwa kuwa zipo karibu zaidi na wananchi.

“Tuna imani sana na kazi za AZAKi kwa kuwa zipo karibu zaidi na wananchi na zina uwezo wa kipekee katika kukuza uelewa hasa inapokuja suala la mtangamano wa Afrika Mashariki,” amesema Dk. Kweka.

Kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ni: “ Nafasi ya Asasi za Kiraia katika Kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Tamasha la AZAKi Tanzania limeandaliwa kwa mara ya tatu mfululizo na Foundation for Civil Society (FCS) chini ya ufadhili wa TMEA na kufanikiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 120 kutoka nchi zote tano za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Waziri Sophia Simba akaribisha ushirikiano bora zaidi na AZAKi

Waziri wa Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Mh. Sophia Simba, amesema Serikali inazitegemea sana Asasi za Kiraia (AZAKi) kusaidia kuleta maendeleo ya jamii nchini ili kufanikisha malengo yanayokusudiwa.

Mh. Sophia Simba ameyasema hayo wakati akifungua Tamasha la 11 la Asasi za Kiraia nchini, linaloandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS) kuanzia Decemba 1 hadi 3, 2014.

“Kazi hii ya kuleta maendeleo ni ngumu, na ni wajibu wetu sote kwa pamoja kati yetu Serikali na AZAKi ili kujenga taifa letu kwa ufasaha,” amesema Waziri Simba.

Mada kuu ya Tamasha hili la 11 la AZAKi nchini Tanzania ni: “Nafasi ya Asasi za Kiraia katika Kuimarisha Umoja wa Kiaifa.”
 
“Wana-AZAKi chukueni nafasi yenu, na hii ni kazi yenu. Waelimisheni wananchi haki na wajibu hasa tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ujao na michakato mingine ya kidemokrasia kama vile kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa,” alisema Waziri Simba.

Aidha, Mh. Sophia Simba ameahidi kwa niaba ya Serikali kudumisha ushirikiano na AZAKi ili wote kwa pamoja kutekeleza vizuri kazi zinazokusudiwa.

Naye Rais wa Foundation for Civil Society (FCS) Dk. Stigmata Tenga amefarijika kwa FCS kuandaa tamasha la 11 mfululizo. “Hii ni heshima kubwa kwetu,” amesema Dk. Tenga.

 

CHAWATA yahimiza wananchi kutowatenga walemavu

Jamii imetakiwa kutowaficha watu wenye ulemavu na badala yake wawasaidie kwa kuwapeleka kwenye vituo husika pale wanapoonekana kushindwa.

Katibu wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Tanzania (CHAWATA) mkoani Mwanza, Vincent Ludomya anasema wadau pamoja na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya vijiji pia wanatakiwa kuwasaidia walemavu na kujua matatizo yao yanayowakabili.

Chama cha Watu wenye Ulemavu Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali linalopigania maslaHi ya watu wenye ulemavu na kwa miaka kadhaa limekuwa likifadhiliwa na The Foundation for Civil Society.

Ludomya anasema kutokana na kikundi cha madaktari kutoka nje kwa kushirikiana na CHAWATA taifa unaonesha kuwa historia kubwa ya watu wenye ulemavu  hapa nchini ipo kwenye kaya maskini.

Anasema kuwa  kaya maskini zipo hatarini kujifungua watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mitindio ya ubongo, matege ulemavu wa akili kutokana na hali ya uchumi kuwa mbaya hivyo kushindwa kuwapeleka hospitalini mapema ili wapate matibabu.

Amezitaja sababu zinazosababisha kuwepo kwa watu wenye ulemavu kuwa ni pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya kwa wazazi, uvutaji wa sigara, magonjwa ya kurithi kutoka kwenye familia au ukoo na kuugua maradhi kama kisonono na kaswendwe kwa mama mjazito.

Anasema takwimu zinaonesha kuwa Zaidi ya watoto 216 kutoka sehemu tofauti mkoani Mwanza kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 wameripotiwa kwenye kituo cha walemavu.
 

Wanawake Pemba wapatiwa mafunzo juu ya sheria ya umiliki wa ardhi

Wanawake wilaya ya Chakechake mkoani Pemba wapatiwa mafunzo juu ya ushawishi na utetezi wa haki za wanawake na sheria ya umiliki wa ardhi ya mwaka 1999.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Vitongoji Environmental Conservation Association (VECA) chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society. Mafunzo haya yametolewa kufuatia uelewa mdogo wa sheria za umiliki wa ardhi na sheria ya ardhi kwa ujumla.

“Nimekaa zaidi ya miaka 20 bila ya ardhi yangu iliyokuwa mikononi mwa mama yangu wa kambo , hivi sasa tayari ardhi yangu nimeshaikomboa kutoka mikononi mwa familia yangu na nimeshaanza kuitumia kwa kilimo cha mahindi. Hii ni baada ya kupata uelewa juu ya sheria ya umiliki wa ardhi kupitia mafunzo yaliyoandaliwa na VECA”, anasema Bibi Mauwa Khamis Saateni mmoja wa wanufaika wa mafuzo hayo.

Anaendelea kusema kuwa, “baada ya kuikomboa ardhi yake kupitia mahakama ya ardhi, safari hii niko tena mahakamani juu ya madai ya nyumba yake ya urithi na hii imetokana na ujasiri alioupata kupitia mafunzo ya VECA”.

Hakimu wa mahakama hiyo, Salim Hassan Bakari anasema,” mafunzo haya yameamsha idadi kubwa kesi za ardhi na tayari zaidi ya kesi 93 za ardhi za wanawake pekee tayari zimeshafikishwa kwenye mahakama yangu. Kesi 43 zimeshafanyiwa kazi na kutolewa maamuzi ambapo kesi 17 wanawake waliweza kushinda na zilizobakia kushindwa kutokana na kukosa vidhibitisho ingawa kimantiki inaonekana wamedhulumiwa na ndugu wakiume ikiwamo baba, kaka na hata waume zao”.

Naye mratibu wa mradi huo Mohamed NajiM Omar anasema, “wanawake wengi hawakuwa na uelewa kwamba suala la umiliki wa ardhi ni haki yao ambapo walidhani mwenye jukumu hilo ni mwanaume pekee.Wanawake walikuwa na dhana potofu kwamba kwakuwa mwanaume ndio msimamizi wa familia, basi umiliki wa ardhi ni haki yake”.

“Tunajivunia kwa sasa kuona  walengwa wa mradi huu ambao ni wanawake na jamii kwa ujumla wameanza kupata muamko kupitia mafunzo haya na kuanza kudai haki zao, anaongeza Omar.

Watu 120 kutoka vijiji 36 vya mashariki mwa Pemba ikiwa ni pamoja na Uwandani, Ole, Kangagani, Furaha, Vitongoji na Pujini wameweza kunufaika na mradi huu.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari