Wananchi Tandahimba watakiwa kuunga mkono elimu

Wakazi wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, wamehimizwa kujitokeza kuunga mkono jitihada zinazofanywa na shirika la Mchichira Shangani Association (MRASHA) katika kukuza kiwango bora cha elimu wilayani humo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Abdallah Njovu , Kupitia hotuba yake iliyosomwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Peter Nambunga wakati anafungua warsha ya siku tatu katika shule iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa serikali, walemavu, wawakilishi wa asasi za kiraia na wananchi wa kawaida chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society
Amesema wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za miradi ya elimu wilayani humo.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo, Mwenyekiti wa MRASHA, Mbaraka Kanowa, amesema asasi yake ina lengo la kuelimisha makundi mbalimbali katika jamii juu ya sera ya elimu ya mwaka 1995 ambayo ipo ingawa haifahamiki vyema kwa jamii.


 “MRASHA ni mfano wa maendeleo ya elimu wilayani kwetu, sisi kama seriali kwa upande wetu tupo tayari kuwaunga mkono, hivyo basi ni jukumu la wananchi kuhakikisha mnaungana nao ili kufikia lengo kwaajili ya kuboresha sekta ya elimu wilayani kwetu,” amesema Njovu.

Asasi yalalamikia kuendelea kufichwa kwa watoto wenye ulemavu wakusikia

Watoto wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) wanaoishi vijijini katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma, ambao wamastahili kuandikishwa shule wamefichwa majumbani na wazazi wao kwa dhana kwamba watoto hao ni laana.

Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa mradi wa CHAVITA wa elimu ya mawasiliano wa lugha ya alama kwa Viziwi, Pius Chiyenje wakati akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwapeleka watoto shule katika warsha iliyofanyika wilayani Mpwapwa chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society  katika kata 12 za wilaya hizo.

Mratibu huyo amesema kuwa watoto walio wengi ambao wanastahili kuandikishwa shule ndani ya wilaya hizo bado wamefichwa majumbani kutokana na Imani potofu ya kuwaona kama ni laana.

Amesema kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na CHAVITA za kuwapatia elimu wazazi hao pamoja na viongozi wa serikali ngazi za vijiji na vitongoji, bado kuna changamoto kubwa ya ongezeko la watoto wenye ulemavu wa kutosikia wanaofichwa majumbani.

Chiyenje amezitaja kata zilizoshiriki ambazo miongoni mwake kuna changamoto ya kuwepo kwa watoto wenye ulemavu huo kuwa ni pamoja na Ngulwe, Berege, Kimangai, Lupeta, Chunyu, Ng’ambi, Kibakwe, Vinghgawe, Motomoto na Chitema.
 

Wadau waweka mikakati ya kukabiliana na vyanzo vya migogoro ya ardhi

Ukosefu wa elimu na uelewa mdogo wa sheria za ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999 ya vijiji, ni moja ya changamoto inayosababisha kuwepo kwa migogoro isiyoisha katika jamii.

Hayo yameelezwa na wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata wilayani Ruangwa mkoani Lindi, wakati wa mafunzo ya sheria hizo yaliyoendeshwa na Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (LIWOPAC) chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society (FCS).

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Ramadhani Nguruwe, amesema migogoro mingi ya ardhi inatokea kutokana na wananchi na wajumbe wa mabaraza ya ardhi kutotambua kanuni na sheria zinazotumika kumpa mtu nguvu ya kumiliki ardhi na kuuza pale anapohitaji kufanya hivyo.

Alisema kama sheria zote mbili zinazoelekeza tafsiri ya ardhi zingetambulika na kueleweka kwa jamii, wanawake wasingedhulumiwa wala kunyimwa haki ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa baadhi ya makabila.

Amesema ni wajibu wa taasisii, mashirika yasiyo ya kiserikali kuona umuhimu wa kusaidia jamii kutoa elimu mara kwa mara juu ya sheria hizo, ili kuwajengea uelewa wananchi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Ruangwa, Vicent Kilowoko, amewataka wajumbe wa mabaraza ya kata wilayani humo kutumia elimu hiyo kwaajili ya kutatua migogoro katika maeneo yao kwa utulivu bila kuvunja amani.

Amewasisitiza wajumbe kufanya kazi kwa uadilifu na kutenda haki bila upendeleo ili kuepuka kuwa chanzo cha migogoro kutokana na kuwa na tamaa ya fedha na mali.
Naye Mwenyekiti wa Liwopac, Jonaphrey Pebe, amesema mafunzo hayo yameshirikisha zaidi ya wajumbe 180 wa mabaraza ya ardhi kutoka kata kata 20 za  wilayani Ruangwa.     

Wazee wataka utekelezwaji wa Sera ya Taifa Wazee ya mwaka 2003

Wazee wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wameitaka Serikali kutekeleza Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 kwa kuziagiza halmashauri zitenge bajeti ya wazee ili kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazee cha Usa River, Joseph Ndonde ametoa wito huo kwenye semina ya wazee  chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society katika  kata tatu ikiwemo  Maji ya Chai, Kikatiti na Usa River  zote  za Wilaya ya Arumeru na zaidi ya wazee 420 watapatiwa elimu hiyo.

Ndonde amesema Sura ya Tatu ya Sera hiyo inaeleza wazi haki za wezee ni pamoja na kutunzwa, kushiriki na kushirikishwa, kuwa huru na kuheshimiwa, jambo alilodai kuwa halitekelezwi.

“Tunaomba halmashauri zianzishe dawati la wazee katika sehemu zote zinazohudumia wananchi ikiwa ni pamoja na hospiitalini, bajeti ya wazee iongezwe na uwanzishwe utaratibu wa kuwatunza wazee", amesema Ndonde.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arumeru, Frida Kaaya amesema halmashauri  kwa mwaka uliopita ilitenga Sh20 milioni kwaajili ya kuwasaidia wazee na mwaka huu itaongeza fedha”.

Amesema fedha hizo zitatumika katika kuwaandalia vitambulisho vitakavyowasaidia kupata fursa ya ya huduma ya bure ya afya na nyinginezo, pia tayari tumeagiza kuanzishwe dawati la wazee na tuna mpango wa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha tunakuwa na kituo maalum cha kutunzia wazee.

NGONEDO kutoa elimu ya utawala bora kwa wananchi

Mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Dododma, NGO Network for Dodoma (NGONEDO) kutoa elimu ya wakazi wa mkoa wa Dododma juu ya kuimarisha utawala bora na demokrasia.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na mratibu program wa NGONEDO, Edward Mbogo. Anasema kutokana na kuwepo na ombwe kubwa la utawala bora pamoja na wananchi kutokujua haki zao, wamelazimika kuanzisha mradi wa wa utoaji wa elimu kwa raia pamoja na watumishi wa mkoa wa Dodoma ili waweze kufanya mambo kwa kuzingatia utashi wa kidemokrasia.

Kupitia ufadhili wa The Foundation for Civil Society, NGONEDO itatoa elimu kwa kila vijiji sita vya wilaya ya Mpwapwa na Kongwa na baadae kuendelea na wilaya zingine za mkoa wa Dodoma, lengo likiwa ni kuhakikisha wanannchi wanatambua jinsi watumishi wa serikali wanavyotakiwa kutimiza majukumu yao kwa mwenendo wa utawala bora na demokrasia,” amesema Mbogo.

Amesema malengo ya mradi huo ni kuhakikisha wanaimarisha utawala bora na demokrasia kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa serikali za mitaa katika wilaya zote na vijiji katika mkoa mzima wa Dodoma.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari