AZAKI zaiomba Serikali kuzisaidia wakati wa elimu ya mpiga kura

Baadhi ya wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka Kanda ya Ziwa waimeiomba Serikali kuwa na utaratibu wa kutoa ruzuku kwa AZAKI ili kusaidia katika elimu ya uraia wakati wa chaguzi zijazo kwa kuwa asasi nyingi zilishindwa kutimiza azma yao wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Wakiwakilishwa na Bw. Edwin Soko ambaye ni mmoja wa Wadau wa Asasi zilizohudhuria katika mkutano wa kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Asasi za Kiraia kutathmini zoezi la utoaji wa elimu ya Mpiga Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana, alisema asasi nyingi hazikuweza kuyafikia maeneo mengi, hususani vijijini kutokana na kukosa rasilimali fedha.

Aidha, kutokana na hali hiyo, naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Bw. Ramadhani Kailima alibainisha kuwa hali hiyo ilisababisha mapungufu mbalimbali kujitokeza katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 Mwaka jana.

Kailima alisema katika baadhi ya Kata nchini, kulitokea mapungufu kadhaa katika zoezi la kupiga kura ikiwemo kura

kuharibika kutokana na wapiga kura kuchora michoro na alama zisizostahili katika karatasi ya kupigia kura, huku baadhi yao wakiandika matusi katika karatasi hizo.

Hata hivyo Kailima aliweka wazi kwamba, zoezi la utoaji wa elimu kwa mpiga kura, lilishindwa kufanikiwa zaidi kutokana

na baadhi ya Asasi za kiraia nchini kutoa elimu kinyume na mwongozi wa NEC, ambapo baadhi ya Asasi hizo zilikuwa zikitoa elimu ya mpiga kura kwa kuangazia zaidi matakwa ya wafadhili wake.

FCS yawezesha uzinduzi wa Ilani ya Asasi za Kiraia kuelekea uchaguzi mkuu 2015

Foundation for Civil Society (FCS) imewezesha uzinduzi wa Ilani ya Asasi za Kiraia kuelekea uchaguzi mkuu 2015 ambapo katika tukio hilo vyama vya Siasa vimeaswa kuachana na lugha ambazo zinaweza kuleta uvunjifu wa amani na badala yake vimetakiwa kunadi sera zao kwa wananchi waweze kupewa ridhaa inayotokana na kura.

Tukio hilo lilifanikishwa jijini Dar es Salaam Septemba 6 huku Mwenyekiti wa Tume ya Haki ya binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, akisema kulingana na kipindi hiki nchi ilipo - vyama vya siasa vinatakiwa kunadi sera na sio kutumia lugha ambazo haziendani na Demokrasia wakati wa kuelekea uchaguzi Mkuu.

Mwenyekiti Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora alitaja baadhi ya lugha zinazotumika ni pamoja na “Tutashinda saa Nne Asubuhi”, “Goli la Mkono” zote ni lugha ambazo hazitakiwi katika kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Amesema kuwa vyombo vya dola ikiwemo jeshi la Polisi vinapaswa kuhakikisha vinasimamia wananchi katika mchakato wa kuelekea katika uchaguzi pasipo kutumia nguvu ili wananchi waweze kusikiliza sera za vyama vyote kupitia wagombea wake.

Hata hivyo amesema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zilizosaini kuwepo kwa Mahakama ya ICC hivyo wale wote ambao watashiriki kuvunja amani wakati wa uchaguzi mkuu watahusika na mahakama hiyo kutokana na kufanya uchochezi na kuvuruga amani.

Aidha amesema kuwa wananchi nao wametakiwa kuvumiliana katika kipindi hiki pasipo kudharau chama cha mwenzake, uchanaji wa mabango ya wagombea kwani hiyo sio demokrasia.

Foundation kuongeza ushiriki wa wananchi Uchaguzi Mkuu 2015

Foundation for Civil Society (FCS) hivi karibuni imeitisha maombi ya miradi kutoka kwa asasi za kiraia Tanzania ambapo kwa pamoja zitashirikiana katika kukuza ushiriki imara wa wananchi katika uchaguzi mkuu ujao na kuhakikisha amani inakuwepo wakati na baada ya mchakato huo.

Ruzuku hii ya miradi mipya inalenga makundi maalum kama vile vijana, wanawake na yale ya walemavu.

Akizungumzia maombi haya wakati wa kuanza zoezi la warsha ya upashanaji habari Julai 8 kwa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa FCS,Francis Kiwanga amesema baada ya ruzuku hii maalum kutolewa watahakikisha kuwa wananchi walioko kwenye makundi hayo maalum wanapata haki yao ya kidemokrasia ya kuweza kushiriki katika uchaguzi mkuu.

Kiwanga ameongeza kuwa lengo la kushiriki katika uchaguzi huu nchi nzima ni kuhakikisha kuwa amani iliyopo nchini inaendelea kuwepo wakati wote wa mchakato wa uchaguzi na kuhakikisha kunakuwa na njia sahihi za kumaliza vurugu zozote zinazoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi.

Shuguli maalum zitakazopatiwa ufadhili ni pamoja na ushawishi kwa makundi maalum kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, vipindi katika vyombo vya habari kupitia mitandao ya asasi za kiraia ili kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye uchaguzi mkuu unaokuja na vile vile kuendesha majukwaa ya kulinda amani ambayo yatashirikisha wananchi katika kutatua migogoro wakati na baada ya uchaguzi.

Amesema kuwa ruzuku hii itatekelezwa kwa muda usiozidi miezi 12, na kiwango cha mwisho cha mradi wa wilaya moja ni shilingi milioni kumi na tano na shilingi milioni arobaini na tano kwa mradi wa kitaifa.

Mwisho wakutuma maombi haya ilikuwa tarehe 31Julai 2015.

Wadau waiunga mkono Foundation kuendelea kuimarisha uwezo wa AZAKi

Wadau katika sekta ya asasi za kiraia nchini wamesifu hatua ya  Foundation for Civil Society (FCS) kuendelea kuzijengea uwezo asasi za kiraia kwakuwa ni muhimu na hitajiko bado ni kubwa.

Haya yamesemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bwana Deus Kibamba katika Warsha ya Upashanaji Habari iliyofanyika Julai 8 mwaka huu iliyoandaliwa na FCS kwa wana ruzuku wake na asasi nyingine jijini  Dar es Salaam.

Suala hili lilifuata baada ya Mkurugenzi wa Foundation, Bwana Francis Kiwanga kutoa taarifa ya uamuzi wa Board ya Wakurugenzi wa Fopundartion juu ya kufunga miradi yote ambayo imepitwa na wakati. Uamuzi huu hautaathiri miradi maalum inayopata ruzuku kutoka ILO, IRC (Wekeza) na EQUIPP. Miradi ya ushiriki wa watu  walemavu katika uchaguzi mkuu wa 2015 itaendelea kama kawaida.

“Uwezo wa asasi za kiraia nchini bado ni mdogo. Nawahamasisha Foundation kuendelea kuwekeza katika eneo hili,” alisema Bwana Kibamba mbele ya wadau wengine walioshiriki warsha hiyo.

Wanafunzi waomba somo la haki za watoto liingie kwenye mtaala

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeshauriwa kuanzisha somo la uchambuzi wa sheria na haki ya mtoto katika katika mitaala ya masomo ili liwasaidie wanafunzi kutambua haki na wajibu wa sheria zinazowahusu watoto.

Wito huu umetolewa hivi karibuni na Wicklif Julius, mwanafunzi wa shule ya msingi Mvomero pamoja na Shaiba Juma wa shule ya msingi Hembeti kwenye semina iliyoandaliwa na asasi ya CCIA chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society.

Wamesema kuwa watoto wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili lakini kutokana na kukosa uelewa wa haki zao, vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea siku hadi siku bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Kama wizara ya Elimu itaanzisha utaratibu wa kutoa elimu ya sheria na haki za watoto, wengi wao hasa wanaofanyiwa vitendo vya ukatili watakuwa na sehemu ya kukimbilia wanapopatwa na matatizo hayo,” alisema Julius.

Kwa upande wao wanasheria waliotoa mada katika semina hiyo, Arnold Temba na Michael Mwambanga wamesema lengo la kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi ni kufikisha ujumbe kuwa watoto hawaelimishwi juu ya haki na wajibu wao.

Waesema kuwa mtoto anatakiwa kupata haki na uhuru sawasawa na mtu mzima ambapo haki zote zimeainishwa katika sheria namba 21 ya haki za mtoto ya mwaka 2009.

Wameongeza kuwa, sheria hiyo inaeleza mtoto ana haki ya kuishi, kuheshimiwa, kupumzika, kuwa na uhuru wa mawazo hivyo jamii inapaswa kuambua sheria hiyo na kuifuata.

“Asasi yetu imejikita kutoa elimu hii ili kuokoa maisha ya watoto wetu ambao wengi wao hawazitambui haki zao,”amesema Mwambanga.

Temba amesema kuwa umefika wakati sasa kwa jamii kutambua kuwa watoto wanatakiwa kuwa na maisha bora, kulindwa na kushirikishwa katika mambo muhimu yanayowahusu bila ubaguzi.

 

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari