Asasi zatakiwa kubadili mbinu za uhamasishaji rasilimali kwa kugeukia wahisani wa ndani

Asasi zashauriwa kuwa na mtazamo tofauti wa njia za kutafuta rasilimali kwa kujielekeza kwa wafadhili wa ndani ili kuimarisha utekelezaji  wa miradi ya maendeleo, na hata kupunguza utegemezi uliokifiri kutoka kwa ufadhili wa nje.

Akizungumza katika warsha iliyofanyika Dar es Salaam juu ya ‘Uhamasishaji wa rasilimali kupitia wahisani wa ndani kwa ajili ya maendeleo’ iliyoandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS) pamoja na East African Association of Grant-Makers (EAAG), Evans Okinyi, mkurugenzi wa EAAG, amesema ni muhimu kwa AZAKI kuwa na mikakati tofauti pindi likija suala la uhamasishaji wa rasilimali ili kuimarisha muendelezo wa miradi yao bila kuyumba. 

“Kwa siku za usoni Asasi za Kiraia na mashirika wezeshaji wanatakiwa kubadilisha mbinu ya vyanzo vya yao kupata rasilimali kwa kuanza kuwageukia wahisani na wafadhili wa ndani ili kukuza rasilimali zao na kujihakikishia muendelezo wa miradi yao katika jamii,” aliongeza.

Kwa upande wake, Bw. Francis Kiwanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS) amesema: “kwa sasa hali ya ufadhili kwa Asasi za Kiraia nchini inaonekana kupungua kutokana na wafadhili wa nje nao kupungua. Hivyo asasi zinatakiwa kupiga hatua zaidi ili kuvutia wahisani wa ndani kama mbadala wa kujihakikishia uendelezaji wa miradi yao katika jamii.” 

Akitoa ushuhuda wa namna uhisani wa ndani unavyofanya kazi nchini Tanzania, Bw. Mwadhini Myanza kutoka asasi ya Morogoro Municipal Foundation amesema kuwa asasi yao iliweza kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kupitia wananchi wenye nia njema ili kuweza kuwasaidia wahanga wa mafuriko wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro. Alisema jitihada hizo ziliwawezesha kupata michango mbalimbali inayofikia thamani ya shilingi  milioni 50, zikiwemo pesa taslimu, nguo, mahitaji ya nyumbani na vitu vingine.

Warsha hii tajwa ilikuwa na lengo la kubadilishana mawazo na kuona namna gani Asasi za Kiraia nchini zinaweza kuifanya sekta ikasonga mbele zaidi na kufanikiwa kuhamasisha rasilimali kutoka kwa wahisani, hasa wa ndani.

Asasi zatakiwa kujiimarisha kuvutia rasilimali

Asasi za kiraia Tanzania zimetakiwa kujiimarisha kuanzia kwenye mifumo yao ya ndani ya kiutendaji ili kuweza kujipambanua vizuri na kushawishi wahisani wa ndani pamoja na wafadhili kuzichangia.


Hayo yamesemwa katikati ya mwezi April na mtaalamu wa masuala ya uhisani, Bw. Benjamin Mtesigwa, wakati akiwasilisha mada juu ya “Uhamasishaji wa rasilimali kupitia wahisani wa ndani kwa ajili ya maendeleo” iliyoandaliwa jijini Dar es Salaam na Foundation for Civil Society (FCS) kwa kushirikiana na East African Association of Grant-Makers (EAAG).


Amesema kuwa jambo la msingi katika kuimarisha uwezo wa ndani wa asasi ili kuvutia rasilimali ni kupitia uundwaji wa mipango mkakati imara ya asasi, inayoonesha malengo, maadili, dhima, na dira ambazo zitasimama kuwawajibisha.
“Kuwa na mpango mkakati ni nguzo imara katika kuwezesha uhamasishaji wa rasilimali.  Inasaidia katika kubainisha mahitaji halisi ya rasilimali yanayotakiwa, sambamba na kuainisha mbinu gani stahiki inayofaa kutafutia rasilimali hizo,” alisema.


Amezitaka asasi kuweka wazi orodha ya nini hasa wanaweza kukifanya katika jamii, na kuonyesha uhusiano wao na mahitaji ya jamii. Amesema pia, ujumbe pamoja na simulizi za mafanikio ni muhimu katika kuwalenga wananchi wanaotaka kuwafikia, na hasa vyombo vya habari.


Kwa upande wake, Bi. Philomena Modu, mmoja wa washiriki kutoka Women’s Fund Tanzania amezitaka asasi kutotilia mkazo tu suala la kujipatia rasilimali bila kusheshimu dhima ya mpango mkakati wa asasi na jamii ambayo ndio wana wajibu mkuu kwao.
                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                           
   

Asasi za Kiraia zanufaika na ujuzi mpya katika usimamizi wa fedha

Asasi zaidi ya 30 kutoka mikoa mbalimali Tanzania zimejipatia mtazamo mpya juu ya kusimamia masuala ya fedha ndani ya asasi zao. Shukrani kwa Foundation for Civil Society (FCS) kwa juhudi binafsi ya kuzisaidia asasi hizi kuandaa miongozo yao ya fedha.

Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku tano yaliyoandaliwa na FCS hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Albina Robert ambaye ni mhasibu katika asasi ya Jamii Inayoishi na Virusi vya UKIMWI Kanda ya Muleba amesema, “Sasa tunajivunia kuwa na mwelekeo mpya wa jinsi tunavyokabiliana na usimamizi wa fedha tofauti na ilivyokuwa awali. Kwani sasa tunaweza hata kujitengenezea miongozo yetu wenyewe.”

Aliongeza kuwa, awali walikuwa na uelewa mdogo wa mifumo mipya ya usimamizi wa fedha hivyo mafunzo hao yawasaidia kuweka vizuri miongozo yao ya fedha ambayo ndio mhimili muhimu katika kuboresha mfumo wa fedha wakati wa matumizi. 

Maria Komba mshiriki wa mafunzo ya FCS kutoka Nyakitonto Youth Development in Tanzania (NYDT) mkoani Kigoma alisema kuwa mafunzo yamewawezesha kutambua na kuthamini misingi ya uhasibu ambao ni muhimu katika kuimarisha usimamizi wa fedha.

“Tunaamini kuwa kwa kufanya kazi na muongozo sahihi wa fedha utaimarisha ufanisi wetu na kupunguza kasoro mbalimbali,” aliongeza Maria.

Geofrey Isack mratibu wa mafunzo haya amesema malengo ya mafunzo haya ni kuzisaidia asasi kuunda mfumo ambao utawasaidia katika kusimamia masuala ya fedha kwa ufanisi na haraka zaidi.

Amesema kuwa mafunzo yameangalia uhitaji, ambapo inaonyesha kuwa asasi nyingi nchini zilikuwa zinaendeshwa bila kuwa na miongozo sahihi ya fedha. Anaamini kuwa mafunzo haya yaliyoandaliwa na FCS yataziwezesha asasi za kiraia kuweza kuandaa mifumo ya fedha ambayo ni muhimu katika kukuza uwajibikaji na hata kupunguza matumizi mabaya ya rasilimali.

 

 

Mafunzo ya jinsia yachochea kupiga vita mila ya ‘unyago’ kwa wasichana

Kupitia mafunzo yaliyotolewa na Foundation for Civil Society juu ya masuala ya usawa kijinsia, Chama cha Kupambana na Virusi vya UKIMWI Shuleni wilaya ya Tandahimba, mkoani Mwara imepiga hatua mbele zaidi kwa kutoa elimu ya kupiga vita mila ya Unyago ambayo imekuwa sababu ya wanafunzi wengi wa kike kutoendelea na shule.

Akizungumza wakati wa tathmini iliyofanywa na FCS ya baada ya mafunzo hayo, Mwenyekiti wa CHAKUMUMA, Rafael Munanka amesema, asasi yeu imepata muamko wa kupigania haki sawa ya elimu kwa motto wa kike kwa kupiga vita  ‘unyago’  sababu utamaduni huu unachochea kumnyima motto wa kike haki yakuendelea na masomo.

Mila ya unyago hufanyika kipindi ambacho mtoto wa kike amefikia umri wa kuitwa mwanamke au wakati wa ndoa. Wanawake watu wazima huwafundisha wasichana  masuala ya ngono na haki za ndoa.Sherehe hizi za unyago hufanyika kwa siku kadhaa zikiambatana na ngoma na muziki.

 “Kupitia mafunzo haya kutoka FCS tumeweza pia kuzipatia maarifa haya asasi zingine ndani ya mkoa wa Mtwara ili kuunganisha nguvu ya pamoja katika kupiga vita utamadni huu wa unyago ambao unamnyima haki ya kwenda shule mtoto wa kike akifikia kipindi cha kuvunja ungo” alisema Munanka

Munanka amesema, mafunzo haya ya masuala ya jinsia yamewapa njia mpya za namna ya kuendesha asasi yao kwa kuzingatia masuala ya jinsia kwa kuweka fursa sawa kwa wanawake kuweza kuchangia mawazo yao na vile vile kushika nafasi za uongozi.

FCS yajivunia kuvuka uwiano wa 50/50 kwa usawa wa kijinsia

Foundation for Civil Society (FCS) imeungana vyema na dhamira ya dunia katika kuhakikisha jamii inakuwa na usawa wa kijinsia kwa kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya asasi za kiraia Tanzania kuhakikisha utekelezaji wa masuala ya jinsia.

FCS inajivunia kuweza kuvuka vizuri lengo la kuweka usawa wa kijinsia wa 50/50 kwa uwiano wa wafanyakazi wake, wanawake na wanaume.

Katika kuadhimisha siku ya Wanawake duniani tarehe 8 Machi, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Bw. Francis Kiwanga, amesema suala la usawa wa jinsia ni jambo ambalo FCS inalitilia mkazo sana, na kuwahimiza na wadau wengine katika sekta hii kuiga mfano huo. 

“Ukitizama kwa haraka uwiano wetu wa wafanyakazi, utagundua kuwa tumepiga hatua nzuri katika kutekeleza na kuvuka mpango wa 50/50 kwa uwiano wa wanawake na wanaume,” alisema Kiwanga.

Kwa asasi za kiraia ambazo FCS imekuwa ikiwapa ufadhili ambazo ziko kwenye jamii tofauti ni vyema pia sera zao zikahuisha masuala ya jinsia katika mipango yao ya kazi kwa kuangalia usawa kati ya mwanaume na mwanamke. Masuala ya usawa wa jinsia yanatakiwa yaingie kwenye vyombo vya kutoa maamuzi, nafasi za uongozi, mahusiano katika jamii, kwani haya ndio yale ya msingi ambayo jamii inakaribishwa kutilia mkao.

Hivyo katika kukuza usawa wa kijinsia, FCS imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali juu ya masuala ya jinsia kwa asasi za kiraia, ikizitaka kuhuisha sera za jinsia katika mifumo yao ya utendaji ya asasi wakati wa utekelezaji wa miradi kwa jamii.

 

 

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari