Mdahalo waibua udhaifu wa uongozi vijijini

Kutokuwapo kwa uadilifu miongoni mwa watendaji wa vijiji, uelewa mdogo wa wananchi juu ya masuala ya utawala na wanasiasa kutoshiriki katika mikutano ya vijiji ni miongoni mwa mambo ambayo yanafanya dhana ya utawala bora kutofikiwa.

Hayo yameelezwa na wakazi wa kata ya Nanyamba mkoa wa Mtwara walipokuwa wakichangia mada katika mdahalo wa utawala bora na uwajibikaji uliofadhiliwa na The Foundation for Civil Society ambapo zaidi ya wakazi 250 walihudhuria na kutoa maoni yao.

Akichangia mada katika mdahalo huo, Mohamed Mwalimu mkazi wa kijiji cha Namkuku, amesema kuwa wananchi wengi vijijini hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa mikutano ya vijiji au vitongoji, jambo ambalo linafanya washindwe kuhudhuria hata pale viongozi wanapoitisha mikutano hiyo.

Shamte Ahamad  mkazi wa kijiji cha Dinyecha alisema kuwa kutokuwapo na uaminifu kwa baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji ni sababu ya wananchi kuamua kususia mikutano ya vijij na vitongoji na kwamba elimu inapaswa kutolewa kwao na watendaji wawajibishwe pale inapobainika kutumia rasilimali za umma kinyume na utaratibu.

“Utakuta wananchi wanakwenda katika mikutano lakini inapofika ajenda za kusomewa mapato na matumizi mizengwe inaanza na hapo vurugu hutokea na kwasababu hiyo wananchi wanaona haina haja ya kushiriki katika miktano hiyo ingawa ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo yao na utekelezwaji wa dhana ya utawala bora,” amesema Shamte.

Hadija Lyangunde, mkazi wa kijiji cha Nanyamba, anasema kuwa kutoshiriki kwa wanasiasa katika kuhamasisha wananchi kwenda kwenye mikutano ya vijiji na vitongoji ni moja kati ya sababu zinazochangia wananchi kutohudhuria katika mikutano hiyo.

Hadija amesema iwapo wanasiasa watashiriki vema na kutimiza wajibu wao wa kuhamasisha wananchi mahudhurio katika mikutano hiyo yatakuwa mazuri na kasi ya maendeleo vijijini itaongezeka na hivyo ile dhana ya utawala bora kukamilika.


Akitoa mada katika mdahalo ulioandaliwa nashirika la Saidia Jamii Kuishi (SAJAKU), Said Swallah, amesema kutekelezwa kwa dhana  ya utawala bora kunakamilika kwa viongozi kuitisha mikutano na wananchi kushiriki ipasavyo.

Swallah amesema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana mahali ambapo utawala bora hautekelezwi hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kulingana na majukumu aliyonayo kiutekelezaji katika kutimiza dhana ya utawala bora.

Akifungua mafunzo hayo, diwani wa kata ya Nanyamba, Hassan Mauji, amewakumbusha wenyeviti wa vijiji juu ya umuhimu wa kuitisha vikao na mikutano mikuu ya vijiji na kuweka mihutasari ambayo itafikishwa katika vikao vya kamati ya maendeleo ya kata ili kuwezesha mipango ya vijiji kutekelezwa na halmashauri ya wilaya.

Mauji amesema kuwa kutoitisha mikutano si tu ni ukiukwaji mkubwa wa utawala bora, lakini pia kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

“Kimsingi hili jambo limekuwa ni tatizo kubwa katani kwetu, tumeshuhudia wananchi wakiwatimua viongozi wao kwa madai ya kutoitisha mikutano sasa hili si jambo jema.... nimekuuwa nikiendesha mikutano ya maendeleo ya kata mimi kama mwenyekiti wa kamati hiyo, lakini utakuta kijiji hakina mihtasari hii maana yake ni kwamba hawajafanya mkutano” amesema Mauji.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi akifungua mafunzo hayo katibu mtendaji wa SAJAKU, Nashiri Pontiya, amesema kuwa lengo ni kuibua mijadala juu ya dhana ya utawala bora.


Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Mdahalo waibua udhaifu wa uongozi vijijini