Asasi Bagamoyo yawezeshwa kuibua wanachama hai

Mwana ruzuku wetu, asasi ya Bagamoyo Youth Information Centre (BAYOICE) sasa inajivunia kuweza kujipatia wanachama hai – siri kubwa ikiwa ni kuweza kuwabadilisha wanachama ‘goigoi’ kupitia mafunzo ya kuimarisha uendeshaji wa asasi waliyotoa kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society.

BAYOICE ni asasi inayoongozwa na vijana kwa nia ya kupanua wigo wa fursa za kiuchumi na kuboresha huduma za kijamii ili kuchangia jitihada za kupunguza umasikini na kuongeza kipato kwa wakazi wa wilaya ya Bagamoyo.

BAYOICE iko katika kata ya Magomeni Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, na imekuwa ikijishughulisha katika kusaidia jamii juu ya changamoto mbalimbali zinazosababisha maendeleo kurudi nyuma.

Mwenyekiti wa BAYOICE, Ally Juma anasema: “Mafunzo yaliyofadhiliwa na Foundation yameleta mabadiliko makubwa katika asasi yetu na kuwawezesha wanachama wetu kutambua majukumu yao na kuboresha mfumo wa utendaji wa kazi tofauti na awali ambapo utendaji wao haukuwa mzuri”.

Juma anasema, wengi wao walikuwa hawawezi kujitolea katika utendaji wa kazi kwa ajili ya kuisaidia jamii mpaka kwanza wapewe posho.

Mbali ya kuwa tunafanya kazi na viongozi wa serikali kupitia halmashuri ya Wilaya, tumeweza kushirikiana na taasisi binafsi, shule za sekondari na msingi katika utojia wa elimu ya mafunzo mbalimbali kulingana na changamoto ambazo zinaikabili jamii.
Mwanachama wa asasi hiyo Josephine Jonasi anasema: “Nimeweza kuwa na upeo katika uandishi wa mradi baada ya kuwa nimepata mafunzo, sasa nafahamu namna ya kuandaa mradi bila kutegemea msaada kutoka kwa kiongozi wetu.”
“Pia katika kipengele cha sera ya taifa ya maendeleo ya vijana nimeweza kuitambua sera hiyo - hasa katika vile vipengele muhimu ambavyo vinatetea vijana na kutimiza wajibu wangu kama kijana ili kuisaidia jamii katika kuleta maendeleo,” anasema Josephine.

Juma anasema kutokana na uhamasishaji wa mafunzo wanachama wameweza kubuni miradi mbalimbali na hivyo kuweza kutatua matatizo tofauti kama vile ulipaji wa pango, gharama za umeme, na hata kujipatia nauli wakati wa kwenda kuendesha semina za mafunzo vijijini bila ya kutegemea na kusubiri ruzuku kutoka Foundation.
Anasema wanachama wamekuwa wakichangishana fedha kwa ajili ya kuendeleza mfuko wa asasi ambao pia unasaidia kuwalipia ada ya shule watoto walio katika mzingira magumu.

Asasi pia imeweza kujiendesha yenyewe kwa kuwa tayari imejengewa uwezo katika kuunda mpango mkakati, na wanachama tayari wamefahamu maana yake na wanatumia fursa hiyo kuaandaa mipango kazi mipya pasipo kumsubiri tena mwezeshaji.
Latifa Rashidi, ni mmoja wa wanuifikaji kupitia mafunzo hayo, anasema: “ilikuwa ni kazi ngumu kwangu kusimama na kujielezea mbele ya mkusanyiko wa watu, lakini sasa ninajiamini kwa kile ninachofikiria kuchangia kama mchango wa mawazo yangu”.

Anaongeza kuwa sasa asasi ina uwezo wa kufanya kazi zake katika jamii bila yao kama wanachama kuomba posho. Pia mafunzo yamemfanya atambue kuwa ni wajibu wake kuyaweka maslahi ya jamii mbele kwa kushilia dhana ya uwajibikaji.

Mwanachama wa asasi, Joseph Peter anasema kutokana na mafunzo wanachama wameweza kuondoa tofauti zao na hata kuondoa vijiashiria vya kuwepo kwa migogoro pindi wanachama wengine walipokuwa kukitegea katika utendaji.

Asasi imeweza kuwa karibu zaidi na jamii kutokana na wanachama wake wengi kutambua namna ya kuboresha maelewano na jamii inayowazunguka na hata kuwahamasisha wanachama wapya kujiunga kwa kuzingatia moyo wa kujitolea.

 Dorisi Kalemwa ambaye ni mwanachama asasi anasema mafunzo yamemhamasisha kuisambaza elimu hata kwa vijana wengine ambao hawakupata fursa kama ya kwakwe.


Aidha, BAYOICE sasa imeondokana na wimbi la kujikuta ikiendeshwa na watu wachache tu waliomo katoka jopo la viongozi na kubadilika kuwa asasi jumuishi. Salama Kassimu ambaye pia amenufaika na mafunzo anasema: “Kupitia mafunzo sasa wanachama tumekuwa na uelewa wa kuendesha asasi tofauti na hapo awali ambapo tulikuwa tunategemea viongozi wetu tu ndio wafanye kila kitu kwa niaba yetu. Sasa dhana ya uanachama hai imeweza kijidhihirisha na kujikita miongoni mwetu.”
   

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Asasi Bagamoyo yawezeshwa kuibua wanachama hai