Waomba uharakishwaji kanuni Sheria ya Ukimwi 2008

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeombwa kuharakisha kutunga kanuni za Sheria ya Kuzuia na Kumbambana na Ukimwi ya mwaka 2008 ili iweze kutekelezwa kupambana na unyanyapaa na kupunguza maambukizi mapya nchini.

Aidha, baadhi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wametaka elimu zaidi itolewe  kwa jamii kuhusu Ukimwi ili kuiwezesha nchi kufikia malengo sifuri ya unyanyapaa, vifo na maambukizi mapya ya Ukimwi ifikapo 2015.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya siku mbili kwa watu wanaoishi na VVU na wadau wengine kuhusu sheria hiyo ya Ukimwi, Mwezeshaji wa mafunzo, Japhes Baitan, alisema sheria hiyo haiwezi kutekelezwa kwa kuwa mpaka sasa haijatungiwa kanuni.

“Ili itekelezeke, irudishwe kwa wadau wanaoishi na VVU na jamii, ichambuliwe na Waziri mwenye dhamana atungie kanuni, lengo ni kuwezesha mpango wa kufikia sifuri tatu katika unyanyapaa, maambukizi na vifo vitokanavyo na Ukimwi mwakani, alisema Baitani.

Alisema sheria hiyo inavifungu vizuri vinavyokataza watu kujitangaza wanatibu Ukimwi bila kuthibitishwa na mamlaka husika, inakataza usiri wa wana ndoa kuhusu Ukimwi lakini alisema haijamlenga vya kutosha mtu asiye na maambukizi ajilinde, jambo ambalo wadau katika mafunzo hayo wamegundua kuwa ni moja ya changamoto.

Kwa upande wake, Katibu wa Asasi ya Kijamii ya Kupambana na Ukimwi na Kifua Kikuu (Maukita) iliyoandaa mafunzo hayo na kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society, Juma Garaba, alisema watu wanaoishi na VVU wanahitaji kujua sheria ili kutambua wajibu na haki zao na kuendeleza mapambano dhidi ya unyanyapaa.

Kwa Upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wanaoishi na VVU, Maimuna Hamis (49) na Athumani Mwirangi (40) kwa nyakati tofauti walisema unyanyapaa bado ni tatizo katika jamii na kushauri elimu zaidi itolewe na kuhamasisha watu kupima afya zao ili kujua waishije.

Tangu mwaka 2008 sheria ilipotungwa na kusainiwa na Raisi Jakaya Kikwete, Wizara ya Afya imeeleza kuwa katika mchakato wa kutunga kanuni hizo.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Waomba uharakishwaji kanuni Sheria ya Ukimwi 2008