CHAVITA yahimiza matumizi ya lugha ya alama

Serikali mkoani Mtwara imeshauriwa kuanza mchakato wa kuhamasisha jamii kujifunza matumizi ya lugha ya alama ili kuondoa vikwazo vya mawasiliano baina ya viziwi na watu wasio na ulemavu huo hatimaye kundi hilo liweze kutumia vyema fursa za kimaendeleo zinazowazunguka.


Ushauri huo ulitolewa juzi na mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) tawi la Mkoa wa Mtwara, Kasim Mchindula alipokuwa akizungumza na wanachama 30 wa chama hicho kwenye mafunzo  ya siku kumi ya  lugha ya alama, mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kanisa la Lutherani mkoani humo.


Alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano baina ya viziwi na jamii inayowazunguka katika kufanikisha shughuli mbali mbali za maendeleo na kwamba hali hiyo inatokana na jamii na baadhi ya viziwi kutofahamu matumizi ya  lugha ya alama hivyo kufanya kuwepo kwa ugumu wa mawasiliano.


Mchindula alisema CHAVITA mkoani Mtwara imeamua kutoa mafunzo hayo ya siku kumi kwa wanachama wake  kupitia mradi wake wa miaka mitatu unaofadhiliwa na Foundation for Civil SOCIETY ambao unalenga kuwajengea uelewa wa namna ya matumizi ya lugha ya alama ambapo itawasaidia kuondokana na vikwazo vya mawasiliano.


Alisema kutofahamika kwa lugha ya alama kunachangia kurudisha nyuma jitihada za maendeleo kwa viziwi hivyo kupitia mafunzo hayo wanachama hao 30 watakuwa na uelewa wa matumizi ya lugha hiyo ya alama na kuwaondolea adha ya mawasiliano na viziwi wengine.


“Hata kwa upande wa elimu viziwi wengi wamekuwa hawafanyi vizuri katika masomo yao kutokana na kutokuwa na ufahamu wa lugha ya alama.” Tunaomba serikali nayo iwe na utaratibu wa kutoa mafunzo ya lugha ya alama kwa jamii ili kuondoa vikwazo vya mawasiliano baina ya viziwi na wasio viziwi”, alisema Mchindula.


Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Ofisa Elimu mkoa, Mshauri wa utamaduni ofisi ya mkuu wa mkoa, Fatma Mtanda alisema lugha ya alama kwa viziwi ni msingi wa upatikanaji wa haki za msingi katika kuboresha mahitaji ya msingi ndani ya maisha yao ya kila siku.


Alisema matumizi ya lugha ya alama kwa viziwi pia kutawasaidia kuweza kuibua vipaji vyao ambapo kwa sasa havitambuliki katika jamii kutokana na jamii kushindwa kuwasiliana na viziwi kwa kutumia lugha hiyo.
“Serikali mkoani hapa tutahakikisha lugha hii inatambulika kwa jamii nzima ili kuwe na usawa wa mawasiliano rahisi kati ya viziwi na watu wasio viziwi hatua ambayo itasaidia kuleta mabadiliko ya maendeleo kwa kundi la viziwi”, alisema Fatuma.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari CHAVITA yahimiza matumizi ya lugha ya alama