Wanawake watakiwa kugombea uongozi

Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Chamwino (Changonet) umetoa changamoto kwa wanawake wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanajitokeza na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ili kuondoa tatizo la ubaguzi wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi.


Ofisa Ustawi wa jamii Wilaya ya Chamwino, Jaina Msangi alisema hayo wakati wa mdahalo ulioandaliwa ma Mtandao wa Asasi hiyo katika Kijiji cha Majereko huku mada kuu katika mdahalo huo ilikuwa mgawanyo sawia wa rasilimali za nchi unaozingatia usawa wa kijinsia chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society.


Alisema ni vizuri kama wanawake wakagombea nafasi mbali mbali za uongozi katika chaguzi mbalimbali ikiwemo zile za Serikali za mitaa ili kuongeza idadi ya wanawake viongozi.
Alisema vitongoji 12 vya kata hiyo hakuna hata kiongozi mmoja mwanamke hali inayoonesha kuwa wanawake hawajitokezi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.


Pia alisema misingi ya utawala bora inaanzia katika ngazi ya familia ni muhimu kama watoto wakapata fursa ya kupata elimu ili waje kujitegema hapo baadae.
Aidha alisema jamii inatakiwa kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa bila kujali ni wa kike, wa kiume au mlemavu.
Kwa upande wake, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Chamwino, Juliana Kilasara alisema licha ya wanawake kujitahidi kujikwamua katika kujikomboa kiuchumi na kifikra, bado juhudi za makusudi za jamii zinazidi kuonekana kuendelea kuwatafutia wanawake fursa zaidi za kujitawala kwa maendeleo ya jamii.


Alisema ni wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na inayojali utu pasipo na kuwepo tofauti ya kijinsia, hata hivyo ndani ya jamii kuna makabila na makundi ya watu ambayo yanadhani kuwa mwanamke hana haki sawa na mwanaume katika kumiliki rasilimali mbalimbali.


Hata hivyo alisema fikra za aina hiyo ni potofu na hazina tena nafasi katika nchi hivyo inatakiwa kuwa na fikra chanya kuwa wanawake wana haki na sifa zote za kumiliki, kusimamia na kushauri juu ya matumizi bora ya rasilimali za nchi.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Wanawake watakiwa kugombea uongozi