Wenye ulemavu watakiwa kufuata sheria

WATU wenye ulemavu nchini, wametakiwa kufuata sheria na taratibu zilizopo wanapofuatilia masuala mbalimbali, badala ya kutumia ulemavu walio nao kushinikiza njia za mkato. Hayo yalisemwa hivi karibuni na Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Flora Masue, wakati wa semina ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika utoaji wa maoni ya Katiba Mpya.

Semina hiyo iliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA)-Mkoa wa Dar es Salaam na kufadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil Society (FCS).

Masue alisema kuna tabia kwa baadhi ya watu wenye ulemavu, wanapofuatilia masuala fulani katika mamlaka husika, kushinikiza washughulikiwe papo hapo bila kufuata taratibu.“Watu wenye ulemavu wana uwezo na hivyo wanapaswa kufuata taratibu na sheria zilizopo sawa na watu wengine wakati wanapofuatilia masuala mbalimbali bila kutumia kisingizio cha ulemavu walio nao,” Masue alisema.

Aliwataka watu wenye ulemavu kutokuwa wachoyo kuwafunza watu wengine wasio na ulemavu masuala mbalimbali yanayowahusu, ikiwamo lugha zao za mawasiliano kama vile lugha ya alama na nukta nundu, ili kupunguza tatizo la mawasiliano.

Naye, Katibu Mkuu wa SHIVYAWATA Mkoa Dar es Salaam, Mohamed Chanzi alilishukuru Shirika la Foundation for Civil Society (FCS), kwa kufadhili semina hiyo.

“Juhudi za FCS za kufadhili matukio kama haya, zimeshuhudia asilimia 70 ya maoni ya watu wenye ulemavu yakijumuishwa katika rasimu ya Katiba Mpya,” alisema Chanzi.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Wenye ulemavu watakiwa kufuata sheria