Vijiji kumburuza kortini Kamishna wa Ardhi

MGOGORO wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji unaoitesa Wilaya ya Kilosa kwa muda mrefu unaingia katika hatua nyingine baada ya Kijiji cha Mfulu, Mambegwa na Mbigili kumburuza mahakamani Kamishna wa Ardhi nchini kwa kukaidi amri ya Mahakama ya Rufaa.

Uamuzi wa vijiji hivyo kumburuza mahakamani Kamishna huyo Januari 15 ulitolewa wilayani humo  katika mafunzo ya sera na sheria za ardhi yaliyotolewa na asasi ya Greenbelt Schools Trust Fund-GSTF kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mambegwa, Said Naga, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi katika kesi ya madai namba 23/2006 ilibatilisha hati na usajili wa Kijiji cha Mabwegere cha wafugaji kwa kukiuka njia za upatikanaji wa kijiji, ambapo wafugaji walikata rufaa Mahakama ya Rufani kwa kesi ya madai namba 53/2010 na kushinda.

“Sasa baada ya kukaa vijiji hivi tumeamua Januari 15 kumburuza mahakamani Kamishna wa Ardhi nchini kutokana na kutunyang’anya ardhi bila  kutushirikisha. Alitoa hati juu ya hati na kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi, kapuuza agizo la mahakama la kuchunguza mipaka na kutoa taarifa ndani ya siku 90,” alisema Naga.

Kwa mujibu wa baadhi ya tarifa ambazo gazeti hili limezipitia ikiwemo barua ya Januari 26 kumb. namba KDC/cl.2/4/Vol.1/5 ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwenda kwa mkuu wa wilaya hiyo, kuna mchanganyiko wa taarifa za uhalali wa kijiji hicho kinachokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 10,234 wakati kijiji mama cha Mfulu ni kidogo mara mbili.

Aidha, mgongano mwingine ni kijiji kupewa hatimiliki mwaka 1990 wakati kiliandikishwa mwaka 1999, mkuu wa wilaya kipindi hicho, Sosthenes Kasapila, aliagiza kung’olewa vigingi vya mipaka ya kijiji  bila kuwashirikisha wananchi, nayo Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutoa hukumu kwa ramani ya kijiji iliyofutwa kisheria.

 

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Vijiji kumburuza kortini Kamishna wa Ardhi