Mwanaruzuku wetu asifiwa kwa kuhamasisha jamii kutumia rasimali zao kwa maendeleo

Asasi ya Integrated Rural Development Organisation (IRDO) iliyoko wilayani Ileje, mkoani Mbeya imesifiwa kwa mchango wake wa kuhamasisha jamii kutumia razilimali zao kuibua miradi ya kimaendeleo badala ya kukaa na kusubiria Serikali ama vyavyo vingine.

 IRDO ilipata kupongezi hizo wakati wa ziara ya pamoja ya Foundation for Civil Society (FCS) ya kutathmini utekelezajiwa miradi yake pamoja na Wadau wake wa Maendeleo iliyofanyika mkoani Mbeya mwanzoni mwa mwezi Disemba.

 “Nimefurahishwa na mfumo wenu mnaoutumia wa kuzijengea uwezo jamii zinazowazunguka ili kutumia rasilimali zao binafsi na hivyo kuyaboresha maisha yao. Nafikiri hata Foundation watakubaliana nami kwa hili na kupanua wigo wa mfano mzuri kama huu wa IRDO,” alisema mwakilishi kutoka Shirika la Misaada la Uingereza (DFID) Zabdiel Kimambo, ambaye pia alishiriki katika ziara hiyo ya pamoja ya kutathmini miradi inayofadhiliwa na Foundation.

 Safari hii washiriki katika ziara ya pamoja ya kutathmini miradi inayofadhiliwa na Foundation walikuwa ni baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Foundation, wakuu wa idara mbalimbali za Foundation na wawakilishi kutoka nchi na mashirika ya Wadau wa Maendeleo wa Foundation. Wadau wa Maendeleo waliowakilishwa katika ziara hii ni pamoja na DFID, Ubalozi wa Norway and Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).

 Akifafanua juu ya matokeo yaliyotokana na mradi wao unaofadhiliwa na Foundation wa kuzijengea uwezo Asasi na vikundi vya kijamii wilayani Ileje mratibu wa IRDO, Patrick Mwalukisa, alisema asasi yake imekwisha kuvipatia mafunzo jumla ya vikundi vya kijamii (CBOs) 42 juu ya usimamizi wa mapato na vile vile juu ya kuratibu miradi ya kimaendeleo.

 Alisema kupitia mafunzo hayo moja ya CBOs lengwa iitwayo, Mkombozi, ilipata hamasa na kuanza kuhamasisha jamii ya kijiji cha Mswima wilayani humo kwa kutumia njia ya tumbuizo la ngoma asilia na kuibika na mradi wa kukarabati barabara ndogondogo pamoja na madaraja ya kiasili kwa kutumia rasilimali zao wenyewe.

Mwalukisa alisema kutokana na ujuhudi hizo, wanakijiji cha Mswima wameweza kujinasuru na changamoto za kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda masokoni na pia kuweza kuwasaidia wanakijiji wenzao wanaougua (hasa wajawazito) kusafiri kiurahisi kwenda katika zahanati ya jirani – takribani kilometa 10 au hata kuvuka na kwenda kijiji cha jirani cha Isoko.

 “Kupitia hizi CBOs, mbali na mambo mwngine, tumeweza kuhamasisha jamii kutambua thamani ya rasilimali zao na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo yao na ya wale wote wanaowazunguka,” alisema Simon Mwang’onda, Mkurugenzi Mtendaji wa IRDO.

Wasiliana Nasi

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Namba ya simu: +255 22 - 2664890-2
  • Nukushi: +255 22 - 2664893

Ungana na sisi

Tupo kwenye mitandao ya kijamii. Tufuate na uungane nasi.

Uko hapa: Home Chumba cha Habari Mwanaruzuku wetu asifiwa kwa kuhamasisha jamii kutumia rasimali zao kwa maendeleo