Pugu waanza kupata taarifa za maendeleo

WAKAZI wa Kata ya Pugu, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, hivi sasa wanapata taarifa za mapato na matumizi ya fedha za maendeleo kupitia mbao za matangazo kwenye ofisi za serikali za mitaa na kata.


Kupatikana kwa taarifa hizo kumetokana na elimu waliyopata ya namna wanavyotakiwa kushiriki katika kupanga bajeti ya serikali na kufuatilia rasilimali za umma zilizopo kwenye kata yao.


Wakazi wa Pugu waliipata elimu hiyo kupitia Asasi ya Hope Deprived People Action in Development (HDPAD) iliyopewa ruzuku na Foundation for Civil Society.Mkurugenzi wa asasi hiyo, Rehema Sembo, alisema mafunzo hayo yamewafumbua macho wakazi wa kata hiyo ambao awali hawakuwa wakifahamu lolote kuhusu fedha za miradi ya maendeleo.


“Tulikwenda Pugu kwa ajili ya shughuli za watoto yatima, tukiwa pale tukagundua kwamba sh milioni 18 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha Shule ya Msingi Pugu Kaijungeni zililiwa na mwalimu mkuu.
“Kwetu ikawa fursa ya kuwaelimisha wakazi wa eneo lile, kwamba serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kata, ambayo lazima wananchi wafahamu na wafuatilie.


“Hivi sasa wamefunguka, kila mtaa umetengeneza kamati ya watu wanne inayoshiriki kupanga bajeti ya mtaa na kufuatilia matumizi ya fedha wanazopewa,” alisema Rehema huku akiishukuru Foundation.
Foundation ilifadhili mradi kwa kutoa ruzuku ya shilingi milioni 44.9 zilizotumika kutekeleza mradi huo katika kipindi cha miezi 18 kuanzia Januari 2012 hadi Septemba, 2013.

Elimu ya ardhi yawaliza wajane

WAJANE katika Tarafa ya Magole, wilayani Kilosa, Morogoro wameangua kilio mbele ya uongozi wa taasisi na asasi ya maendeleo ya elimu na maarifa ya Greenbelt Schools Trust Fund (GSTF) baada ya kuelimishwa kuwa wanaruhusiwa kumiliki ardhi hadi ekari 50 kwa hati ya mila.


Wajane hao walijikuta wakiangua kilio hivi karibuni katika mafunzo yaliyoandaliwa  na GSTF kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society (FCS) baada ya kufafanuliwa sheria za ardhi ikiwemo ya vijiji ya mwaka 1999, ushirikishwaji katika mipango ya usimamizi na matumizi bora ya ardhi vijijini na utatuzi wa migogoro ya ardhi inavyotekelezeka.


Wakitoa mifano mbalimbali, wajane hao akiwemo Anna Chilangilo wa Magole aliyenyang’anywa eneo lake kwa nguvu na uongozi wa kijiji lenye ukubwa wa nusu eka baada ya kufiwa na mumewe, alisema awali alidhani uongozi huo uko sahihi na kwamba sasa anakusudia kuuburuza mahakamani.


“Huku vijijini tunaonewa sana. Mimi ni mjane mwenye watoto wanne, alipofariki mume wangu uongozi wa kijiji ukakata eneo langu na kumpatia mfanyabiashara eti kwa sababu ni kubwa.
“Ilitumika nguvu kwakuwa walijua sina wa kunitetea, lakini sasa kwa elimu hii nasema tutakutana mahakamani, asanteni sana GSTF,” alisema Anna.

Wananchi walalamikia miradi kutelekezwa

Imebainishwa kuwa kukosekana kwa uelewa wa kutosha kuhusu ufuatiliaji wa fedha za umma kwa wananchi wengi, kumesababisha ongezeko la utelekezwaji wa miradi mingi ya maendeleo hasa vijijini na hivo kusababisha, miradi hiyo kuwa chini ya kiwango.

Hayo yalibainishwa jana na baadhi ya wananchi wa Mji mdogo wa Kimamba wilayani Kilosa, Ramadhani Liwest, Aishi Ally na Yahya Mhina ambapo walieleza kuwa ni vyema jamii ikapewa mafunzo ya kuwajengea ufahamu wa kuweza kuhoji mapato na matumizi katika idara mbalimbali hasa zile zinazogusa moja kwa moja jamii, ikiwemo elimu na afya katika halmashauri za wilaya.
 
Kauli hiyo ya wananchi imekuja huku tayari asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Kilosa African Youth Organization,(KAYO) ikiwa imeanza kuwawezesha wananchi wa Kilosa juu ya mbinu za ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma (PETS) katika idara ya afya ndani ya halmashauri ya wilaya ya Kilosa.

Kwa upande wake Mratibu wa Asasi hiyo ya KAYO, Ramadhani Nassoro na katibu wake, Juma Mseti kwa nyakati tofauti walisema kuwa wameamua kutoa mafunzo hayo ili wananchi wajitambue na kufahamu wajibu wao katika kufuatilia fedha na rasilimali za umma ili kupeta tija kwa wananchi.

Aidha, walisema kuwa wananchi wanaweza kufanya jukumu hilo kama vikundi na kufuatilia hali hiyo ikiwemo katika vituo vya afya na zahanati na kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia hata ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Mseti alisema walisukumwa kuanzisha asasi hiyo baada ya kubaini wananchi hawana elimu katika kufuatilia miradi na misaada mbalimbali inayowafikia, jambo ambalo limekuwa ni rahisi kutumika vibaya au kutekelezwa chini ya kiwango.

Hata hivyo, alisema mafunzo yaliyoanza kutolewa kwa wananchi katika mji mdogo wa Kimamba chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society, yatasaidia kwa kiasi kubwa kuwawezesha wananchi kuwa na mbinu mbalimbali za kuweza kufuatilia fedha na rasilimali za umma ambazo zinaletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo.

Wenye ulemavu watakiwa kufuata sheria

WATU wenye ulemavu nchini, wametakiwa kufuata sheria na taratibu zilizopo wanapofuatilia masuala mbalimbali, badala ya kutumia ulemavu walio nao kushinikiza njia za mkato. Hayo yalisemwa hivi karibuni na Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Flora Masue, wakati wa semina ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika utoaji wa maoni ya Katiba Mpya.

Semina hiyo iliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA)-Mkoa wa Dar es Salaam na kufadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil Society (FCS).

Masue alisema kuna tabia kwa baadhi ya watu wenye ulemavu, wanapofuatilia masuala fulani katika mamlaka husika, kushinikiza washughulikiwe papo hapo bila kufuata taratibu.“Watu wenye ulemavu wana uwezo na hivyo wanapaswa kufuata taratibu na sheria zilizopo sawa na watu wengine wakati wanapofuatilia masuala mbalimbali bila kutumia kisingizio cha ulemavu walio nao,” Masue alisema.

Aliwataka watu wenye ulemavu kutokuwa wachoyo kuwafunza watu wengine wasio na ulemavu masuala mbalimbali yanayowahusu, ikiwamo lugha zao za mawasiliano kama vile lugha ya alama na nukta nundu, ili kupunguza tatizo la mawasiliano.

Naye, Katibu Mkuu wa SHIVYAWATA Mkoa Dar es Salaam, Mohamed Chanzi alilishukuru Shirika la Foundation for Civil Society (FCS), kwa kufadhili semina hiyo.

“Juhudi za FCS za kufadhili matukio kama haya, zimeshuhudia asilimia 70 ya maoni ya watu wenye ulemavu yakijumuishwa katika rasimu ya Katiba Mpya,” alisema Chanzi.

Shivyawata yaitolea uvivu Serikali

Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania(Shivyawata) wilayani Bahi mkoani Dodoma limesema serikali imeshindwa kutekeleza ahadi zake ikiwemo kuwapatia matibabu bure.


Kuali hiyo imetolwa na Katibu wake, Damaris Ndalu kwenye warsha ya kujadili Sera na haki za watu wenye ulemavu iliyofanyika kijiji cha Kigwe.


Damaris alisema kitendo cha serikali kushindwa kutekeleza ahadi hiyo kimewalazimu kuendelea kununa dawa kwenye vituo vya afya.


Hatahivyo, alisema walemavu hao wanakabiliwa na changamoto ya kutopatiwa ajira na serikali na kusababisha wengi kugeuka omba omba mtaani.


Katibu wa Shirikisho hilo mkoa wa Dodoma, Justus Ng’wantalima aliitaka serikali kuwapatia walemavu nyenzo zitakazowasaidia kuzalisha mali na kujiairi.

Contact us

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Tel: +255 22 - 2664890-2
  • Fax: +255 22 - 2664893

Connect with us

We're on Social Networks. Follow us & get in touch.
 

     

You are here: Home News Room Habari & Matukio