NGONEDO kutoa elimu ya utawala bora kwa wananchi

Mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Dododma, NGO Network for Dodoma (NGONEDO) kutoa elimu ya wakazi wa mkoa wa Dododma juu ya kuimarisha utawala bora na demokrasia.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na mratibu program wa NGONEDO, Edward Mbogo. Anasema kutokana na kuwepo na ombwe kubwa la utawala bora pamoja na wananchi kutokujua haki zao, wamelazimika kuanzisha mradi wa wa utoaji wa elimu kwa raia pamoja na watumishi wa mkoa wa Dodoma ili waweze kufanya mambo kwa kuzingatia utashi wa kidemokrasia.

Kupitia ufadhili wa The Foundation for Civil Society, NGONEDO itatoa elimu kwa kila vijiji sita vya wilaya ya Mpwapwa na Kongwa na baadae kuendelea na wilaya zingine za mkoa wa Dodoma, lengo likiwa ni kuhakikisha wanannchi wanatambua jinsi watumishi wa serikali wanavyotakiwa kutimiza majukumu yao kwa mwenendo wa utawala bora na demokrasia,” amesema Mbogo.

Amesema malengo ya mradi huo ni kuhakikisha wanaimarisha utawala bora na demokrasia kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa serikali za mitaa katika wilaya zote na vijiji katika mkoa mzima wa Dodoma.

Watendaji wa serikali za mitaa wadaiwa kupinga mradi wa PETS

Watendaji katika idara za kiserikali huona mradi wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma (PETS) kama mwiba kwao ingawa mtandao wa Asasi zisiszo za Kiserikali wilayani Nkasi mkoani Rukwa (NKANGO) umesema utaendelea kutoa elimu ya mradi huo.

Mwenyekiti wa NKANGO, Victor Sadalla amesema watendaji wengi katika idara za Kiserikali, hawaupendi mradi wa PETS kwakuwa wanaamini ni mradi unaolenga kufichua maovu yao kwa jamii wanayoitumikia kwa kuwafumbua macho wananchi.

Haya yamesemwa kwenye warsha ya siku mbili ya mafunzo ya mwongozo wa PETS chini ya ufadhili wa The Foundation for Civil Society, kwa viongozi wa asasi zinazounda mtandao wa NKANGO na Maofisa Watendaji katika ngazi za vijiji na kata za wilaya hiyo. Sadalla amesema mradi huu unalenga kuboresha utendaji kazi wa idara za kiserikali.

Amesema pamoja na changamoto za kutokubalika kwa mradi wa watendaji, mtandao utaendelea kutoa elimu hiyo na kuwataka watendaji katika idara za kiserikali kutambua kama kichocheo cha maendeleo.

Ofisa Tawala wa wilaya ya Nkasi, Mwanaisha Luaga akifungua warsha hiyo, amesema PETS haipo kumuhukumu mtu bali kufichua mambo yasiyo sawa katika utendaji na wanaochukia hawatambui umuhimu wake.

“PETS haimuhukumu mtu, ipo kutoa changamoto kwenye utendaji kazi wetu wa kila siku. Sisi kama watendaji kwenye  Serikali za Mitaa tunapaswa kuona mradi huu kama chombo chenye manufaa kwakuwa kinatukumbusha hata pale baadhi yetu tunapojisahau,” amesema Mwanaisha.

“Ni Imani yangu kuwa kadiri elimu inavyoendelea kutolewa, kama vile wananchi wanavyotambua umuhimu wa kufuatilia matumizi ya rasilimali zilizopo ndivyo na sisi watendaji tutaendelea kutambua umuhimu wa mradi huu na kuanza kutoa ushirikiano,” amesema.

AZAKi zatakiwa kuhamasisha mtangamano wa Afrika Mashariki

Mgeni Rasmi katika Tamasha la tatu la Asasi za Kiraia Tanzania, Dk. Josephat Kweka, amezitaka Asasi za Kiraia (AZAKi) katika ukanda wa Afrika Mashariki kutumia nafasi zao vizuri kuhamasisha mtangamano wa Afrika ya Mashariki kwa kuelimisha wananchi juu ya fursa zinazoweza kupatikana kupitia mtangamano huo.

Dk. Kweka ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark EastAfrika, amesema taasisi yake inathamini sana mchango wa Asasi za Kiraia katika kuhamasisha kukuza mazingira ya biashara na hatimaye mtangamano wa Afrika ya Mashariki, kwa kuwa zipo karibu zaidi na wananchi.

“Tuna imani sana na kazi za AZAKi kwa kuwa zipo karibu zaidi na wananchi na zina uwezo wa kipekee katika kukuza uelewa hasa inapokuja suala la mtangamano wa Afrika Mashariki,” amesema Dk. Kweka.

Kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ni: “ Nafasi ya Asasi za Kiraia katika Kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Tamasha la AZAKi Tanzania limeandaliwa kwa mara ya tatu mfululizo na Foundation for Civil Society (FCS) chini ya ufadhili wa TMEA na kufanikiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 120 kutoka nchi zote tano za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Waziri Sophia Simba akaribisha ushirikiano bora zaidi na AZAKi

Waziri wa Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Mh. Sophia Simba, amesema Serikali inazitegemea sana Asasi za Kiraia (AZAKi) kusaidia kuleta maendeleo ya jamii nchini ili kufanikisha malengo yanayokusudiwa.

Mh. Sophia Simba ameyasema hayo wakati akifungua Tamasha la 11 la Asasi za Kiraia nchini, linaloandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS) kuanzia Decemba 1 hadi 3, 2014.

“Kazi hii ya kuleta maendeleo ni ngumu, na ni wajibu wetu sote kwa pamoja kati yetu Serikali na AZAKi ili kujenga taifa letu kwa ufasaha,” amesema Waziri Simba.

Mada kuu ya Tamasha hili la 11 la AZAKi nchini Tanzania ni: “Nafasi ya Asasi za Kiraia katika Kuimarisha Umoja wa Kiaifa.”
 
“Wana-AZAKi chukueni nafasi yenu, na hii ni kazi yenu. Waelimisheni wananchi haki na wajibu hasa tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ujao na michakato mingine ya kidemokrasia kama vile kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa,” alisema Waziri Simba.

Aidha, Mh. Sophia Simba ameahidi kwa niaba ya Serikali kudumisha ushirikiano na AZAKi ili wote kwa pamoja kutekeleza vizuri kazi zinazokusudiwa.

Naye Rais wa Foundation for Civil Society (FCS) Dk. Stigmata Tenga amefarijika kwa FCS kuandaa tamasha la 11 mfululizo. “Hii ni heshima kubwa kwetu,” amesema Dk. Tenga.

 

CHAWATA yahimiza wananchi kutowatenga walemavu

Jamii imetakiwa kutowaficha watu wenye ulemavu na badala yake wawasaidie kwa kuwapeleka kwenye vituo husika pale wanapoonekana kushindwa.

Katibu wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Tanzania (CHAWATA) mkoani Mwanza, Vincent Ludomya anasema wadau pamoja na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya vijiji pia wanatakiwa kuwasaidia walemavu na kujua matatizo yao yanayowakabili.

Chama cha Watu wenye Ulemavu Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali linalopigania maslaHi ya watu wenye ulemavu na kwa miaka kadhaa limekuwa likifadhiliwa na The Foundation for Civil Society.

Ludomya anasema kutokana na kikundi cha madaktari kutoka nje kwa kushirikiana na CHAWATA taifa unaonesha kuwa historia kubwa ya watu wenye ulemavu  hapa nchini ipo kwenye kaya maskini.

Anasema kuwa  kaya maskini zipo hatarini kujifungua watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mitindio ya ubongo, matege ulemavu wa akili kutokana na hali ya uchumi kuwa mbaya hivyo kushindwa kuwapeleka hospitalini mapema ili wapate matibabu.

Amezitaja sababu zinazosababisha kuwepo kwa watu wenye ulemavu kuwa ni pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya kwa wazazi, uvutaji wa sigara, magonjwa ya kurithi kutoka kwenye familia au ukoo na kuugua maradhi kama kisonono na kaswendwe kwa mama mjazito.

Anasema takwimu zinaonesha kuwa Zaidi ya watoto 216 kutoka sehemu tofauti mkoani Mwanza kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 wameripotiwa kwenye kituo cha walemavu.
 

Contact us

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Tel: +255 22 - 2664890-2
  • Fax: +255 22 - 2664893

Connect with us

We're on Social Networks. Follow us & get in touch.
 

     

You are here: Home News Room Habari & Matukio