Wazee waitaka Serikali kutatua kero Zao

Serikali wilayani Nkasi mkoani Rukwa imesema kuwa inatambua changamoto mbalimbali hapa nchini ambazo wazee wanakabiliana nazo na kuwa kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa za kuhakikisha wazee wanaishi katika mazingira ambayo ni salama na uhakika.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Idd Hassan Kimanta alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wazee wilayani Nkasi na kuijua vizuri katiba yao ya asasi ya Wazee na Maendeleo wilayani Nkasi (WAMANKA) chini ya ufadhili wa The foundation for Civil Society.

Amesema kuwa moja ya changamoto kubwa ambayo wazee wanakabiliwa nayo ni suala la matibabu na kuwa licha ya wazee hao kupewa vitambulisho vitakavyowawezesha wao kutibiwa bila malipo bado mpango huo hauonyeshi tija na kuendelea kuwapatia usumbufu wazee wetu na kutopata matibabu halisi na kuendelea kusumbuliwa na maradhi ambayo kimsingi yangepata tiba ya uhakika wazee wangekuwa salama.

Kimanta amesema yeye kama kiongozi wa serikali wilayani Nkasi amekwishaliona hilo na kuwa sasa atafanya mazungumzo na viongozi wenzake wa Halmashauri akiwemo mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ili kuona namna wanavyoweza kuwasaidia wazee hao kwa kuwakatia bima ya afya ya jamii badala ya vitambulisho hivyo ambapo mwisho wa siku huambiwa kuwa dawa hazipo hospitalini.

Amesema kuwa watakaa na kuangalia kama kuna uwezekano wa wazee hao wakatibiwa na bima ya afya ya jamii na serikali kuwachangia kupitia mpango wa tele kwa telena kuwa hilo ndilo litakalokuwa suluhisho la matatizo ya matibabu kwa wazee.
“Hakuna suluhisho katika matibabu ya wazee kama bima ya afya ya jamii maana bima itawasaidia hata kwenda kupata dawa katika maduka yaliyoidhinishwa na hilo nitalipigania ili wazee wote wawe na bima hiyo,” alisema Kimanta.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa changamoto nyingine ya pensheni ya wazee wote lilikwisha fika serikalini na kulitazama kwa kina na kuwa mchakato wake bado upo na serikali bado inafanya utafiti wa kuona ni  namna  gani wao wanavyoweza kufanikisha zoezi hilo la kuwapatia wazee wote pensheni hiyo.

Amewataka wazee kuendelea kuwa na mshikamano ndani yao kwa kujenga umoja wenye nguvu na kuwa wakiwa na sauti ya pamoja ni rahisi kwa serikali kuweza kusikia kilio chao na kukitafutia ufumbuzi wa haraka.

Awali, mwenyekiti wa asasi ya Wazee na Maendeleo (WAMANKA), Victor Sadala amemweleza mkuu huyo wa wilaya changamoto hizo na kuwa serikali wamekuwa wazito sana katika kutatua changamoto mbalimbali walizonazo na ambazo wameipelekea serikali kiasi cha wao kujiona kana kwamba hawana faida tena katika jamii baada ya kuzeeka wakati wao wamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleoya taifa hili.Contact us

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Tel: +255 22 - 2664890-2
  • Fax: +255 22 - 2664893

Connect with us

We're on Social Networks. Follow us & get in touch.
 

     

You are here: Home News Room Habari & Matukio Wazee waitaka Serikali kutatua kero Zao