Asasi Busega yasaidia mtoto yatima kuondolewa kwenye ajira mbaya

Huenda mtoto Kaswahili Mathiasi (12) anayeishi katika kijiji cha Busami Wilaya ya Badugu mkoani Simiyu, hubaki akiyakumbuka malezi mazuri aliyowahi kuyapata kutoka kwa marehemu wazazi wake enzi za uhai wao. Ni maisha ambayo hayakudumu sana kwani mambo yalianza kubadilika taratibu baada tu ya wazazi wake kufariki na hatimaye alianza kuuona ulimwengu kuwa katili kwake na maisha kuwa magumu zaidi kutokana na manyanyaso kutoka kwa walezi wake.

Kutumikishwa mashambani na kuchunga mifugo kwa muda mrefu kuliweza kumfanya apoteze haki yake ya msingi ya kujiendeleza na masomo kwa kuwa muda mwingi alikuwa akiutumia katika shughuli hizo.

“Sipendi kukumbuka wakati mateso haya yalipoanza kurindima. Wakati mwingine nilitamani kutoroka na kuondoka kabisa kijiji kwetu, nisirudi tena. Ilikuwa wazi kwamba sikuwa na kitu chochote baada ya ndugu wa marehemu baba kugawana mali za wazazi wetu na kutuacha mikono mitupu,” anasema Kaswahili.

Kaswahili anasema, kitu kilichokuwa kikimpa wakati mgumu ni pale alipokuwa akinyimwa chakula, na wakati mwingine ilimlazimu atoroke shule kwa ajili ya kutafuta ajira ndogondogo ili aweze kujipata chakula.

“Nilikuwa nikilima mashamba ya watu na kulipwa Sh.1000 na wengine waliweza kunipa chakula baada ya kuwa nimemaliza shughuli zao. Kupitia ajira hii niliweza kujipatia kipato kwani sikuwa na mtu wa kumueleza shida zangu wala kunisaidia,” anasema.

“Hapakuwepo na mtu wa kututetea, kwani manyanyaso yalizidi hadi kiasi cha dada yangu kuozeshwa angali akiwa mdogo na mahari kugawana wenyewe kwa wenyewe. Nilikuwa nikijifikiria ninini hasa kilichopo mbele yangu,” anaongeza.

Lakini sasa kuna matumaini mapya katika maisha ya mtoto Kaswahili baada ya kufikiwa na kazi za asasi ya Busega Children & Development Services Assistance (BCDSA) chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS).

Anasema aliweza kukutanishwa na watoto wenzake na kuwa mwanachama wa klabu za watoto zilizoendeshwa na asasi ya BCDSA na kunufaika na huduma mbalimbali zilizorandana na Sera ya Mtoto ya mwaka 1996 na Sheria ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2009.

Kupitia klabu za watoto taarifa zake ziliweza kufikishwa kwa Mtendaji wa Kata ili aweze kuzifanyia kazi. Mtendaji aliweza kufika nyumbani kwao na Kaswahili na kufanya mazungumzo na shangazi yake (jina limehifadhiwa) ambapo walizungumza waziwazi juu ya haki za mtoto, na hatimaye shangazi huyo alikiri makosa na kubadirika.

Wanajamii wengi pia sasa wameanza kulaani vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto na kuonesha kutoridhishwa kwao na vitendo ambavyo  vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wazazi na walezi. Jamii sasa imeanza  kubadilika na kuogopa klabu za watoto ambazo zimekuwa makini kufuatilia watoto wanaonyanyasika.

“Nimejifunza mengi kupitia semina zilizoendeshwa na klabu za watoto. Ushirikiano wa viongozi wa klabu za watoto, viongozi wa asasi na wa Kata katika kuhakikisha wananitembelea katika kijiji ambacho nilikuwa nikiishi ni jambo la kuigwa. Kwa kweli nashukuru kupata mabadiliko katika familia yangu,” anasema kaswahili.

Anaongeza ushirikiano wa klabu hizo na viongozi wa vijiji uliweza kuhakikisha anaweza kwenda shule kama njia moja ya kumpa ahueni kutokana na majeruhi ya kisaikolojia aliyokuwa ameyapata. Wananchi pia walihamasika na kumchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vyake vya shule zikiwemo sare na madaftari.

Hata hivyo uongozi wa kijiji uliamua kufungua kesi katika Baraza la Kata na kuwashitaki walezi wa mtoto Kaswahili juu ya kitendo chao cha kutumia vibaya miradhi iliyoachwa na marehemu wazazi wake pamoja na kutaifisha mahari ya dada yake wakati harusi. Vitu vyote waliweza kuvirudisha yakiwemo mashamba na kulipa fedha za mahari. Viongozi wa kijiji baada ya kuhamasishwa waliweza kupeleka shauri hilo katika Mahakama ya Mwanzo na dada yake Kaswahili akateuliwa kuwa msimamizi wa mirathi pamoja na mali mpaka mdogo wake atakapofikisha umri wa miaka 18.

“Nashukuru klabu za watoto hususani asasi ya BCDSA. Mimi kama yatima sasa naona maisha yangu yamekuwa mazuri kulingana na jamii kuanza kunithamini tena. Najivunia kufika darasa la saba bila matatizo,” anasema mtoto Kaswahili.
Afisa Mtendaji wa kata ya Busame, Mussa Bwiru anasema: “Walezi na wazazi wengi wamekuwa wakiwatishia watoto wao kuwa watawatenga katika ukoo pale wanapobaini kuwa mtoto katoa taarifa juu ya vitendo ya unyanyasaji ambavyo wanamfanyiwa. Hali hii tumeweza kuibadili kwa ushirikiano wa asasi na klabu za watoto baada ya kuwachukulia hatua wale ambao wamebainika kufanya ukatili dhidi yao.”

Kupitia uhamasishaji wa klabu za watoto, watoto 65 wameweza pia kupelekwa shule za sekondari na msingi kutokana na michango ya wananchi pamoja kamati za maendeleo za kijiji na hivyo kufanikiwa kuikabili changamoto kubwa ya tatizo la watoto kutopelekwa mashuleni.

Watoto kutoka kata ya Badugu, wameeleza kunufaika na mradi kutokana na mafunzo waliyofundishwa, wameweza kutambua haki na wajibu wao kwa jamii, sheria zinazomlinda mtoto, wajibu wa wazazi na walezi na pia endapo ukiukwaji wa haki za binadamu utatokea sasa wamejua ni wapi wataanzia kutoa taarifa.

“Mtoto mwenzetu amekuwa akikoseshwa haki kwa muda mrefu. Kupitia klabu hizi zinazosimamiwa na BCDSA tulipata ujasiri wa kuweza kuliripoti jambo hili kwa viongozi wa kata kwa lengo la kumsaidia mwenzetu,” anasema Mtoto Mathias Jackson.
Gadlord Deuli, ambaye ni mratibu wa BCDSA anasema: “watoto 60 waliohudhuria katika semina kupitia klabu zao tayari wamepata haki zao. Sasa wote wanasomeshwa bila ya kuwepo kwa ubaguzi, ndoa za umri mdogo hususani kwa watoto wa kike sasa zimekomeshwa katika eneo letu.”

Mbali na ushawishi uliokuwa ukifanywa, klabu hizo ziliundwa kwa ajili ya kutetea haki ya watoto na kuunda kamati ambazo ziliendeshwa na kusimamiwa na watoto wenyewe ili kupaza sauti za wenzao. Kupitia klabu za wa watoto, watoto sasa wameanza kupata haki zao na wanaweza kushiriki kubainisha kasoro mbalimbali zinazotatiza upatikanaji wa haki zao za msingi.


Contact us

THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

  • Tel: +255 22 - 2664890-2
  • Fax: +255 22 - 2664893

Connect with us

We're on Social Networks. Follow us & get in touch.
 

     

You are here: Home News Room Habari & Matukio Asasi Busega yasaidia mtoto yatima kuondolewa kwenye ajira mbaya